MAKABIDHIANO YA TAARIFA RASMI IKULU.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli, leo katika Ikulu ya Dar es Salaam amepokea taarifa rasmi ya
makabidhiano ya Ofisi kutoka kwa Rais Mstaafu Mheshimiwa Jakaya Mrisho
Kikwete.
Makabidhiano
hayo yamefanyika leo mchana na kushuhudiwa na Makamu wa Rais Mhe.
Samia Suluhu Hassan, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue na
Maafisa wa Ofisi Binafsi ya Rais.
Utaratibu
wa kukabidhiana Ofisi katika Ofisi Kuu hapa nchini ni jambo la kawaida
na hivyo imebidi makabidhiano hayo kati ya Rais anayeondoka na anaye
ingia madarakani kufanyika.
“Umeanza
vizuri, baki na msimamo huo huo utasaidia sana wananchi” . Mhe. Rais
Mstaafu wa Awamu ya Nne amemueleza Mhe. Rais Magufuli wakati wa hafla
hiyo ya makabidhiano.
Mhe.
Rais Mstaafu amekabidhi taarifa rasmi yenye kurasa 53, ambayo kwa
ujumla inaelezea kazi zilizokwisha kufanyika, ambazo zinasubiri
kukamilika na zile ambazo zinasubiri maamuzi ya utekelezaji. Mengine
ni hali halisi ya nchi katika nyanja zote za kiuchumi, kisiasa na
kijamii.
Mhe. Rais Dkt. Magufuli amemshukuru Rais Mstaafu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi kwa muongozo wake siku zote .“Nikushukuru kwa kuiacha nchi salama na itaendelea kuwa salama, nikushukuru kwa muongozo wako, na taarifa ya muelekeo na ninaahidi kuwa Hapa ni Kazi Tu”.
Mhe. Rais amesema
na kumueleza Rais Mstaafu kuwa ametengeneza mazingira mazuri ambayo
nchi nyingi zimeshindwa kufanya na hivyo basi kuahidi kuendelea kuchota
hekima na busara kwa Marais wote wastaafu wakiwemo Mhe. Benjamin William
Mkapa wa Awamu ya Tatu na Mzee Ally Hassan Mwinyi wa Awamu ya pili.
Wakati
huo huo Mhe. Rais Magufuli ameendelea kupokea salamu za pongezi kutoka
Kwa Msimamizi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Bibi
Helen Clark.
“Chini
ya uongozi wako, tunatarajia kuzidi kuimarisha ushirikiano baina yetu,
demokrasia, kushughulikia masuala ya umaskini na ajira kwa vijana ,
kukuza uchumi, na kulinda na kuhifadhi mazingira, masuala ambayo
Tanzania na UNDP tumekuwatukishirikiana kuyaendeleza na kuyatimiza” amesema Bi Clark.
Salamu
zingine ni kutoka kwa Rais wa Shirikisho la Uswiss, Mhe. Simonetta
Sommaruga, Rais wa Jamhuri ya Italia Mhe. Sergio Mattarella, Rais wa
Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani Mhe. Joachim Gauck na pia kutoka kwa
Rais wa Finland Mhe. Sauli Niinisto.
Pongezi
zingine zimetoka kwa Rais wa Jamhuri ya Urusi, Mhe. Vladimir Putin,
Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini, Mhe. Salva Kiir Mayardit, Rais wa
Jamhuri ya Korea Mhe. Park Geun-hye na kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya
Watu wa China, Mhe. XI Jinping.
Salamu pia
zimemfikia Mhe. Rais Dkt. Magufuli kutoka kwa Rais wa Taifa la Eritrea
Mhe. Isaias Afwerki na kutoka kwa Rais wa Ufaransa Mhe. Francois
Hollande.Katika ujumbe wao, viongozi hao mbali na kumpongeza Mhe. Rais
Dkt. Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, wamesisitiza kuendeleza na kuimarisha ushirikiano baina ya
Tanzania na nchi zao.
Pia
wameipongeza Tanzania kwa kudumisha demokrasia imara na Watanzania kwa
ujumla kwa kuimarisha amani na utulivu wakati wa Uchaguzi Mkuu.
Imetolewa na:
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi.
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
12 Novemba, 2015
0 comments:
Post a Comment