Mkurugenzi
Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Ian Ferrao akisisitiza jambo kwa
waandishi wa habari alipokuwa akitangaza mikakati ya kampuni hiyo
kuipeleka Tanzania katika ulimwengu wa teknolojia na itakavyotumia
kubadilisha maisha ya watanzania na kuwa bora zaidi.Hafla hiyo
ilifanyika jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya
waandishi wa habari na wafanyakazi wa Vodacom Tanzania, wakiwa katika
mkutano wa waandishi wa habari na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo,
Ian Ferrao (hayupo pichani)alipokuwa akitangaza mikakati ya kampuni hiyo
kuipeleka Tanzania katika ulimwengu wa teknolojia na itakavyotumia
kubadilisha maisha ya watanzania na kuwa bora zaidi.Hafla hiyo
ilifanyika jijini Dar es Salaam.
(Picha na Mpigapicha Wetu).
Yawekeza zaidi ya Dola bilioni 1 nchini
Mtandao wake wa 2G na 3G umewafikia wananchi kwa 87%
Inao mtandao wa mawakala zaidi ya 85,000 wa M-Pesa nchini kote.
Biashara zaidi ya 10,000 nchini kote wanatumia huduma ya Lipa kwa M-Pesa
Ni kinara wa kulipa na kukusanya kodi za serikali katika sekta ya mawasiliano
KAMPUNI
ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania ambayo inaongoza kwa kuwa na mtandao
mkubwa nchini na mtandao wenye kasi zaidi wa 3G leo imetangaza mikakati
yake ya kuipeleka Tanzania katika ulimwengu wa teknolojia na
itakavyotumia teknolojia kubadilisha maisha ya watanzania kuzidi kuwa
bora.
Akitangaza
mkakati huo kwa waandishi wa habari leo katika hoteli ya Hyatt Regency
jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Ian
Ferrao, alieleza mikakati hiyo mbalimbali “Tunafurahi kuona mchango wa
Vodacom katika kuleta maendeleo nchini na kubalisha maisha ya watanzania
kuwa bora, Hivi sasa tumejizatiti kuboresha huduma za mawasiliano
nchini na pia tutaendelea kubuni huduma mbalimbali za kutumia teknolojia
ya simu kurahisisha maisha ya wananchi.
Tutaendelea
kuboresha na kusambaza huduma zetu za internet nchi nzima na kutoa
huduma za kifedha na malipo kwa kutumia teknolojia,kuuganisha biashara
mbalimbali kwa kutumia teknolojia tukiwa tunaenda sambamba na mkakati wa
serikali wa kuleta mapinduzi ya matumizi ya teknolojia katika kupata
huduma mbalimbai nchini”
Mpaka
sasa Vodacom imewekeza kiasi cha zaidi ya Dola bilioni 1 za kimarekani
nchini Tanzania,imejenga mtandao wa kutoa huduma za internet ya 2G na 3G
na mtandao wake unawafikia asilimia 87 ya watanzania nchini kote.Ikiwa
inajivunia kufanya kazi na mtandao mkubwa wa mawakala wake zaidi ya
85,000 wa kutoa huduma ya kifedha ya M-Pesa. Vodacom inayo wateja zaidi
ya milioni 12 na pia ni kinara wa kukusanya na kulipa kodi za serikali
katika sekta ya mawasiliano nchini.
Ferrao
alisema licha ya changamoto mbalimbali zilizopo katika uwekezaji kwenye
sekta ya mawasiliano nchini kama vile kodi kubwa na ushindani katika
bei za kutoa huduma, Vodacom itaendelea kuwekeza na kubuni huduma za
kuleta ushindani kwenye mapinduzi ya matumizi ya teknolojia nchini.
Kuhusiana
na ushindani wa bei za kutoa huduma Ferrao alisema “Ushindani huu wa
makampuni katika bei za kutoa huduma unawanufaisha wateja kwa muda
mfupi,kinachotakiwa ni kuendelea kufanya uwekezaji endelevu kama vile
kusambaza zaidi huduma ili ziweze kuwafikia wananchi wengi hususani wa
maeneo ya vijijini.
Tukiwa ni
moja ya nchi inayotoza viwango vya juu vya kodi katika seka ya
mawasiliano duniani tunachopaswa kufanya ni kutumia huduma hizi kuleta
mapinduzi yatakayoleta mabadiliko kwa wananchi kuwa bora na kujenga
uchumi imara na wenye ushindani”Alisema
Katika
kufanikisha mchango wa sekta ya mawasiliano kuleta mapinduzi nchini
alisema kuna mambo yanapaswa kuangaliwa “Tumekuwa tukishuhudia ongezeko
la kodi hususani kodi ya zuio, katika sekta ya mawasiliano ambapo kodi
zinazotozwa hapa nchini ni kubwa katika nchi zote za Afrika Mashariki na
nchi za SADC.
Utafiti
wa Taasisi ya Deloitte Consulting katika mkutano wa makampuni ya
mawasiliano uliofanyika jijini Dar salaam mapema mwaka huu inaonyesha
kuwa sekta ya mawasiliano inachangia asilimia 3.8% ya pato la Taifa na
asilimia 11 ya mapato ya serikali kupitia kodi na kodi hizo zinaongeza
gharama za uendeshaji kwa kampuni ambapo mzigo wote humwangukia
mtumiaji kutokana na gharama za huduma kupanda.
Kwa mfano
serikali ikipunguza kodi ya zuio katika huduma ya muda wa maongezi
kutoka asilimia 17 mpaka asilimia 10 itawezesha wateja wapya 1.7
millioni kujiunga na huduma za simu na kwa kufanya hivyo zitawanufaisha
katika shughuli zao mbalimbali za uzalishaji na kutakuwepo ongezeko la
mapato linalofikia Dola 0.5 bilioni katika pato la taifa hadi kufikia
mwaka 2020”.
Kuhusiana
na suala la masafa yaliopo kwa makampuni ya simu nchini alisema leseni
zake zimetolewa kwa makampuni zaidi ya 14 ambayo mengi yao
yanashikilia masafa bila kuyatumia lakini leo hii wateja zaidi ya
asilimia 99 wanahudumiwa na makampuni yenye masafa ya mawimbi ya mtandao
ya asilimia 53 ambapo makampuni yanayotoa huduma za mawasiliano hivi
sasa hayapati masafa ya kutosheleza mahitaji ya kusambaza huduma zake
kwa ufasaha.
Ferrao
alisema wakati umefika kwa masafa ya makampuni kuongezwa hadi kufikia
700Mhz kuwezesha makampuni kuwekeza kwa kutumia teknolojia za kisasa
zaidi na zenye gharama nafuu ambazo zinaweza kuwezesha kuzinduliwa
interneti mpaka ya 4G nchini.
Alisema
pamoja na changamoto mbalimbali zilizopo Vodacom imewekeza zaidi
shilingi Bilioni 180 kwa muda wa miezi sita iliyopita katika kuboresha
mtandao wake wa internet na imejipanga kuboresha huduma zake mbalimbali.
Ferrao
aliongeza “Wakati Vodacom inajizatiti kuboresha huduma zake taasisi yake
ya kuboresha huduma za jamii ya Vodacom Foundation imejikita kuendelea
kutoa misaada mbalimbali kwa jamii hususani kwa ajili ya kuendeleza
akina mama na makundi mbalimbali yenye mahitaji.
Mwaka huu
imewezesha operesheni kwa ajili ya wanawake 2,274 walioathirika na
fistula , na kuwezesha wasichana 7,077 kubaki shuleni kupitia mradi wa
Hakuna Wasichoweza na imewezesha zaidi ya wanafunzi 6,000 kusoma elimu
ya kompyuta kwa vitendo mashuleni.Vodacom Foundation imekwishatumia
shilingi bilioni 12 kusaidia jamii tangu ianzishwe mwaka 2006 na
itaongeza zaidi kiasi hicho cha fedha kusaidia miradi mbalimbali katika
mwaka wake wa fedha ujao”
Alimalizia
kwa kusema “Hatutaacha kubuni na kutoa huduma bora lengo kubwa likiwa
ni kuhakikisha watanzania wote wameunganishwa na huduma ya mtandao wa
intaneti”
0 comments:
Post a Comment