Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimesema, kitampa ushirikiano mkubwa, Rais Dk. John Magufuli, ili aweze kwa ufanisi zaidi mapambano yake dhidi ya mafisadi na mikakati mingine ya kuinua uchumi wa Watanzania.
Kimesema,
kitampa ushirikiano huo Rais Dk. Magufuli, kwa sababu, aliyoanza
kuyafanya na atakayoyafanya baadaye katika uongozi wake wa Urais
anatekeleza yale yaliyomo katika ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2015-2020.
Hayo
yalisemwa na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alipokuwa
akijibu maswali kadhaa yaliyoulizwa na baadhi ya wahariri, aliokuwa
akizungumza nao, katika ziara aliyofanya leo, katika Kampuni ya New
Habari Corporation, Sinza jijini Dar es Salaam.
Baadhi
ya wahariri, waliohoji ni kwa nini CCM haijitokezi kumpongeza Dk.
Magufuli katika juhudi ambazo ameanza kuonyesha katika kupambana na
ufisadi ikiwemo kubana fedha za walipa kodi ambazo zingepotea bure
katika masuala yasiyo ya lazima na wakati huohuo kuanza kuwabana
wafanyabiashara wanaodaiwa kukwepa kulipa ushuru.
"Yapo
mengi tuliyoanisha katika ilani yetu ya Uchaguzi, na yote yahahusiana
sana na haya mnayoyaona yanafanywa na Rais Dk. John Magufuli, tena Ilani
hii tumeitunga hata kabla ya kumteua kugombea Urais, Sasa anachofaya ni
kuitekeleza ilani hii, isipokuwa mbinu anazotumia ni ubunifu wake na
hili hatuna tatizo nalo kama Chama maana kiongozi wa aina hii ndiye
tuliyemtaka", alisema Nape.
"Najua
wapo wanaojaribu kutengeneza magingira ya kumtaka kumtenganisha Dk.
Magufuli na CCM, nawambieni Dk. Magufuli ni zao la CCM na mwana CCM
Kindakindaki, hivyo ni upotoshaji wa hali ya juu kujaribu kuuaminisha
umma kwamba anayofanya Dk. Magufuli hayana uhusiano na maelekezo ya
CCM", aliongeza Nape.
Alisema,
baada ya kutengeneza ilani yake, CCM, ilidhamiria kwamba, awamu hii ya
tano ni ya kutafsiri uchumi katika nyanja za huduma za Jamii, ikiwemo
miundomboni, maji, afya na elimu.
"Ni
kutokana na lengo hili, ndiyo sababu tukakaa kwa makini na kuhakikisha
ilani hii ya sasa tunamkabidhi mwana CCM ambaye utekelezaji wake
hautakuwa wa mashaka mashaka, Ndiyo huyo Dk. Magufuli, bila shaka sasa
na ninyi ni mashahidi mmeanza kuuona utekelezaji wake wa ilani", alisema Nape.
Akizungumzia
kuhusu Rais Dk. Magufuli kuchelewa kutangaza Baraza lake la Mawaziri,
Nape alisema, Chama Cha Mapinduzi kimeshaunda serikali kwa kumpata Rais,
kilichobaki sasa ni kwa Rais mwenyewe kuteua watendaji wake, lakini
katika kufanya hivyo hakuna mda aliopangiwa kuanza kufanya hivyo na
hashurutishwi na Chama wala sheria.
Nape
alisema, Dk. Magufuli hachelewi kuteua Baraza la Mawaziri kwa sababu
anakosa wakuwateua, isipokuwa, anayo namna na mda ambao mwenyewe Kama
Rais amejipangia, na mda huo ukijiri wa kuamua kufanya hivyo atafanya.
"Tatizo
hapa ni kwamba mnayo kiu kubwa ya kutaka kujua nani atawateua, sasa kiu
yenu imepita kiasi, ndiyo maana mnaanza kuhoji, lakini mimi naamini Dk.
Rais Magufuli ataikata kiu yetu, wala msipate taabu ya kuhoji kila
kukicha", alisema Nape.
Nape
alisema, mbali na Chama kutengeneza ilani ambayo italeta mageuzi
makubwa ya kiuchumi hapa nchini, pia Watanzania watarajie kuona mageuzi
makubwa ndani ya CCM, kwa sababu yapo njiani kuwadia.
"Kama
ilivyo kawaida yetu, kila baada ya uchaguzi mkuu huwa tunafanya
tathmini, baada ya tathmini hiyo, huwa lazima tufanye mageuzi kwa yale
ambayo tumebaini kuwa ni kikwazo kwa uhai na maendeleo ya Chama katika
nyanja mbalimbali, na mageuzi haya tunayafanya kuzingatia mahitaji ya
sasa na wakati ujao", alisema Nape.
Kuhusu
Mwenyekiti wa sasa Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete kumwachia Ueneyekiti
Rais Dk. Magufuli, Nape alisema, hayo si mambo mageni kwa CCM, imekuwa
ikifanyika katika awamu zote za Urais, hivyo Kikwete anaweza akaamua
kumwachia kabla ya uchaguzi mkuu wa CCM utakaofanyika mwaka 2017 au
kabla ya hapo akiona inafaa.
Zanzibar
Akizungumzia
mgogoro wa Zanzibar uliotokana na kufutwa uchaguzi mkuu wa Rais wa
Zanzibar, Nape alikiri kamba ni mbaya na unaitia doa Tanzania, lakini
akasisitiza kwamba njia pekee ya kuumaliza ni kwa mazungumza baina ya
viongozi wa ndani bila kushirikishwa mataifa ya nje.
Alisema,
msingi wa mgogoro uliojitokeza Zanzibar, si wa kisheria, bali ni wa
kisiasa zaidi, hivyo juhudi ziwekwe kwenye mazungumzo kuutatua, na baada
ya kuutatua yaendelee kufanyika mazungumzo ambayo yataleta suluhisho la
kudumu kwa kuwa imekuwa ni kawaida kwa Zanzibar kuzuka migogoro kila
baada ya uchaguzi mkuu jambo linaloonyesha kuwa tatizo ni la asili zaidi
kuliko inavyodhaniwa.
Katika
mazungumzo yake na wahariri hao wa New Habari Corporation Ltd,
Wachapishaji wa magazeti ya Rais, Mtanzania na Dimba, alivitaka vyombo
vya habari nchini, sasa kushirikiana na Serikali kulijenga taifa.
"Tunajua
wakati wa kampeni kulikuwa na mambo mbalimbali ambayo wakati mwingine
vyombo vya habari vililazimika kukampenia vinaowaona kuwa wanafaa
kutokana na sababu mbalimbali, lakini kama tulivyokuwa tukisema, kwamba
baada ya uchaguzi maisha yataendelea, sasa umefika wakati wa kuendelea
na maisha tuwe kitu kimoja", alisema Nape.
Alivitaka
vyombo vya habari, kusaidia kuishauri Serikali na CCM, katika
kutekeleza yaliyo bora kwa taifa na hata pale vyombo hivyo vitakapoona
kwamba Chama au serikali vinaenda kinyume, visihofu kukosoa.
Kwa
upande wao, Mtariri Mtendaji wa Habari Corporation, Absalom Kibanda
akimpongeza Nape kwa ushirikiano ambao amekuwa akivipa vyombo vya
habari, na kumtaka aendelee kuwacha milango wazi kwa waandishi wa habari
kama ambavyo amekuwa akifanya.
Ziara
hiyo ya Nape aliyoianza jana, kwenye vyombo vya habari inatarajiwa
kuendelea kesho kwa kutembelea vyombo vingine vya habari vyenye makao
yake makuu jijini Dar es Salaam.
0 comments:
Post a Comment