MKUU
wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo, amepinga hatua za Mamlaka ya Maji
Safi na Usafi wa Mazingira (Mwauwasa) kuongeza bei ya maji kwa madai
ongezeko hilo litasababisha wananchi wengi kukosa huduma.
Mulongo
alitoa kauli hiyo juzi wakati akizungumza na wafanyakazi wa Mwauwasa,
namna wanavyotoa huduma kwa wananchi, changamoto zinazowakabili pamoja
na mafanikio ya mamlaka hiyo.
Hivi
karibuni Mwauwasa, ilitangaza kuomba kuongeza bei ya maji kwa kile
ilichodai kupanda kwa gharama za mita za maji hivyo wanapendekeza
kuongeza bei ya maji kitendo ambacho wananchi wengi jijini hapa
walikipinga.
Mulongo
akizungumza na wafanyakazi hao amesema kuwa katika ufuatiliaji
alioufanya amebaini kwamba kuna mchezo uliandaliwa na mamlaka hiyo kwa
lengo la kujinufaisha wao wenyewe na sio wananchi hivyo haungi mkono
hatua hizo.
“Mimi
ninafahamu kwamba hawa watu ambao mliwaleta na wakakubaliana na nyie
kuongeza bei ya maji ni wa kwenu ambao mliwaaandaa ili kuwaaminisha
wananchi, sasa suala hilo siliungi mkono.
“Utaratibu
wa kuongeza bei ya maji ambao nyie mnadai kupanda kwa gharama za mita
za maji kaeni muangalie upya namna ambayo mtafanya,” amesema Mulongo.
Hata
hivyo Mulongo aliwataka wafanyakazi hao kuwajibika kwani ni wajibu wao
kuhakikisha wananchi wanafikiwa na huduma ya maji safi hususani
wanaoishi katika maeneo ya miinuko.
0 comments:
Post a Comment