Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (wa pili
kushoto), akipata ufafanuzi kuhusu namna ya kuhifadhi makontena kutoka
kwa Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania Aloyce Matei
(kushoto), mara baada ya kukagua Mamlaka hiyo leo jijini Dar es Salaam.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa
maelekezo kwa Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania Aloyce
Matei (wa tatu kushoto), huku Naibu Waziri wa wizara hiyo Mhe. Eng.
Edwin Ngonyani (wa pili kulia), akifatilia.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akiwa na
Naibu wake wakikagua mtambo wa kuchunguza makontena (scanner) katika
eneo la TPA.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akikagua
mtambo wa madai na malipo wa Mamlaka ya Bandari Tanzania alipotembelea
Mamlaka hiyo leo.
Akizungumza na watumishi wa wizara hiyo mara baada ya kuapishwa, Profesa
Mbarawa amesema kipaumbele chake kwa wafanyakazi hao ni kufanya kazi
kwa uadilifu, weledi na kwa kuzingatia matokeo chanya kwa haraka.
“Tuwe tayari kubadilika, tufanye kazi ya kuwahudumia watanzania kwa
moyo, tuendeleze taswira nzuri ya Wizara kwani Wizara hii ina sifa nzuri
tangu ilipoanza hadi sasa’, amesisitiza Waziri Mbarawa.
Profesa Mbarawa amefafanua kuwa uwazi na uhusiano mzuri kwa wafanyakazi
ni ngao kubwa katika kusukuma gurudumu la maendeleo kati ya watendaji na
watumishi.
Aidha, amewataka watendaji na watumishi wa Wizara hiyo kushirikiana na
kutokuwa wanyonge kutokana na mfumo wa mabadiliko ya kiutendaji wa
iliyokuwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwani Wizara hizo
zina uhusiano mkubwa katika kumhudumia mwananchi hivyo kuungana kwake
kutaleta tija na ufanisi kwa haraka.
“Jambo la msingi ni kufuata kanuni na sheria katika utendaji wenu pamoja
na kusimamia miongozo iliyopo, utendaji wenu lazima uwe na malengo
yanayotekelezeka kwa haraka”, amesema Prof. Mbarawa.
Akizungumza na watumishi wa Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), Waziri huyo
amehimiza matumizi ya teknolojia katika huduma za bandari ili kuweza
kuwahudumia wateja kwa haraka hata wakiwa mbali.
Amewataka watumishi wa bandari kuwa waadilifu na kufanya kazi kwa
ushindani ili kuvutia wadau wengi kupitisha mizigo yao katika bandari za
Tanzania.
“Fanyeni kazi kwa maslahi ya nchi, acheni kufanya kazi kwa maslahi
binafsi, tambueni Serikali na wananchi wanahitaji huduma bora
zitakazokuza uchumi wa taifa kutoka katika bandari zenu”, amesisitiza
Waziri Mbarawa.
Naye, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Eng. Edwin
Ngonyani amewataka watumishi wa bandari kuacha tamaa, kuishi kwa
uaminifu ili kujenga taswira mpya ya taasisi hiyo ambayo ni muhimu kwa
uchumi wa taifa na jamii kwa ujumla.
Katika ziara hiyo Waziri Mbarawa na Naibu Waziri Ngonyani waliambatana
na viongozi mbalimbali wa iliyokuwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano.
0 comments:
Post a Comment