MAHAKAMA
Kuu Kitengo cha Ardhi imezuia nyumba anayoishi Mchungaji wa Kanisa la
Assemblies of God Mikocheni, Dk. Getrude Lwakatare kubomolewa.
Uamuzi huo wa mahakama ulitolewa juzi
na Jaji John Mgeta, baada ya Wakili wa Lwakatare, Emmanuel Muga
kuwasilisha maombi ya kupinga ubomoaji huo chini ya hati ya dharura.
Jaji Mgeta alizuia ubomoaji wa jengo hilo ama kuchukua hatua yoyote kuhusu jengo hilo lililopo Kawe Beach.
Muga aliwasilisha maombi akimwakilisha
mdai ambaye ni mtoto wa Mchungaji Lwakatare, Robert Brighton dhidi ya
wadaiwa NEMC, Manispaa ya Kinondoni na wadau wengine wote.
“Mheshimiwa jaji, nawasilisha
maombi ya zuio la kubomoa nyumba ya mteja wangu chini ya kifungu namba
95 cha Sheria ya Mwenendo wa Madai na kifungu namba 2(3) cha JALA
vinavyotoa mamlaka kwa mahakama kutoa nafuu stahili pale kunapokuwa na
ukiukwaji wa kuvunja haki ya wazi,” alidai.
Akitoa uamuzi huo alisema tayari pande
husika zilikuwa na kesi namba 70 ya mwaka 2012 na ikamalizika kwa kutoa
hukumu na kukazia hukumu iliyompa haki ya ushindi mdai.
“Mahakama ilimpa haki mdai, lakini
chakushangaza mdaiwa anakiuka matakwa ya hukumu na kutaka kubomoa
nyumba, kwa hali isiyokuwa ya kawaida mdai anahitaji ulinzi wa mahakama
hii ya haki,”alisema Jaji Mgeta.
Alisema nyumba hiyo ipo katika kiwanja namba 2019 na 2020 ambapo hati yake ilitolewa mwaka 1979.
Inadaiwa mwaka 2011 NEMC ilitoa notisi
ya kuvunja nyumba hiyo baada ya kushinikizwa na wakazi wa eneo hilo
wakidai ujenzi wake unaziba Mto Ndumbwi na uko jirani na mikoko.
Wakili Muga aliwasilisha maombi ya
kuzuia nyumba ya mteja wake kubomolewa baada ya Wizara ya Maliasili
na Utalii kupitia wakala wa misitu Tanzania (TFS ), kuweka alama
ya X wakidai imo katika hifadhi ya bahari
0 comments:
Post a Comment