Sakata la utoaji makontena bila kulipia tozo ya bandari, limechukua sura mpya baada ya Chama cha Mawakala wa Forodha (Taffa) kufungua kesi Mahakama Kuu, kupinga kitendo cha Mamlaka ya Bandari (TPA) kuwadai fedha za tozo hiyo ambazo wamesema wameshalipia.
Taffa
imefungua kesi hiyo kwa hati ya dharura, ikipinga TPA kutaka kufungia
kampuni zinazojihusisha na masuala ya forodha, kuwakamata watendaji
wake, na kutaka iache kushinikiza walipe tena tozo hizo.
TPA imezitaka taasisi 284 kuwasilisha nyaraka za malipo ya tozo hizo za kuanzia mwaka 2014, kuthibitisha kama zilikuwa zikilipa.
Tangu
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa afanye ziara mbili za kushtukiza bandarini
na baadaye Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame
Mbarawa, zimeibuliwa kashfa nyingi za ufisadi, na hasa upitishaji wa
makontena bila ya kulipia kodi na mengine kutoweka.
Akizungumza
katika mkutano mkuu wa dharura wa chama hicho uliofanyika jana jijini
Dar es Salaam, wakili anayesimamia kesi hiyo, Lambaji Madai aliwataka
wanachama wa Taffa kuendelea kuwasilisha ushahidi wa malipo ya tozo hizo
wanayofanya kupitia benki, ili yaweze kutumika kama kidhibiti
mahakamani.
“Tunapaswa
kuwa kitu kimoja katika hili na tuache kurushiana maneno wenyewe kwa
wenyewe. Si wakati wa kuangalia nani msafi na nani mchafu kati yetu.
Mawakala wa forodha ndiyo tunatuhumiwa na sehemu pekee ya kusikilizwa
sisi na TPA ni mahakamani,” alisema.
Alisema
kuanzia Jumatatu ijayo watapata mrejesho wa kesi hiyo, na kwamba lengo
ni kuhakikisha kuwa haki inatendeka kwa kuwa mawakala wa forosha
wanaonekana kuhusishwa na mambo ambayo hawayafanyi.
Rais
wa Taffa, Stephen Ngatunga alisema TPA imekuwa ikiwatuhumu mawakala wa
forodha wanaolipa tozo hiyo kwa niaba ya wateja wao, kuwa ndiyo
wahusika, wakati inajulikana wazi kuwa mzigo hauwezi kutoka bandarini
bila kuonyesha stakabadhi za malipo yaliyofanywa kwenye benki zenye
mikataba na mamlaka hiyo.
“Jumatatu
(kesho) tutakwenda Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
kuwasilisha malalamiko yetu na kueleza jinsi TPA na benki
wanavyoshirikiana kufanya wizi huu. Tuna ushahidi na hawa watu wanaiba
hata ukifanya malipo kwa fedha taslimu au hundi,” alisema Ngatunga, huku baadhi ya mawakala wakionyesha ushahidi wa malipo.
Alisema
ili kutatua tatizo hilo, wadau wote wa usafirishaji wanapaswa kukutana
na kujadili ili kuwabaini wahusika, si kuwatupia mpira mawakala wa
forodha.
“Jiulizeni
iweje TPA wazitake kampuni za forodha ziwapelekee ushahidi wa malipo
wakati wao ndio wanaotoza malipo hayo na wana kumbukumbu,” alisema Ngatunga.
Baadhi
ya mawakala waliozungumza katika mkutano huo walipendekeza masuala
mbalimbali, ikiwamo kutaka kufanya malipo hayo kwenye Mamlaka ya Usafiri
wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) na Mamlaka ya Mapato (TRA), badala ya
kutumia benki.
0 comments:
Post a Comment