BARAZA
la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limeanza kung’ata
kwa kutumia kanuni ili kudhibiti uchafuzi wa mazingira kwa kelele na
mitetemo.
Kwa
sasa mtu akitaka kufanya sherehe mtaani, kupiga muziki kwa kelele,
kuendesha ngoma za kukesha za nusu uchi (vigodoro) au ‘bai koko’ au
kufanya ibada kwa kelele mitaani, atapaswa kulipa Sh milioni 10.
Pia, baa na kumbi za starehe za usiku zitakazopiga kelele, zitapaswa kulipa kiasi hicho.
Aidha,
NEMC imesema pia kuwa wale watakaohusika na kelele za migodini za
kutumia baruti, kupasua miamba zilizo zaidi ya matakwa ya sheria ya
mazingira ya kelele na mitetemo, watapaswa kulipa Sh milioni tano ili
kupata kibali.
NEMC
imetaka watu kuheshimu kanuni za viwango vya kelele na mitetemo katika
maeneo mbalimbali nchini. Imeonya kuwa watakaokiuka, hatua kali
zitachukuliwa dhidi yao. Kanuni hizo zimeanza kutumika mwaka jana
(2015).
Mkurugenzi
Mtendaji wa NEMC, Bonaventure Baya alisema hayo Dar es Salaam jana.
Alisisitiza kuwa uchafuzi wa mazingira, unaosababishwa na kelele na
mitetemo, umekuwa ukifanyika bila kujali sheria za nchi na sasa
watashughulikia suala hilo ipasavyo.
Alisema
hivi sasa kanuni za kudhibiti suala hilo, zimekamilika na zimeanza
kutumika kikamilifu. Mtu yeyote atakayekwenda kinyume cha kanuni na
sheria, atachukuliwa hatua kali. Baya alitoa ufafanuzi kuwa yapo maeneo
yenye kelele zaidi ya viwango vinavyoruhusiwa kisheria, ikiwamo maeneo
ya migodini.
Alieleza
kwamba kanuni zimeweka vigezo na tozo maalumu la kuanzia Sh milioni
tano hadi Sh milioni 10, kulingana na eneo na aina ya kelele na mtetemo.
Alisema mambo mengine ambayo kanuni zimeweka ni faini kwa kila kanuni
itakayovunjwa na kusisitiza kuwa hatua hizo zitachukuliwa ipasavyo.
Kulingana
na hatua hiyo ya NEMC, sasa mtu mwenye kutaka kufanya sherehe mtaani,
itakayohuisha kelele zitakazosumbua jamii pamoja na majirani zake,
ikiwamo muziki maarufu wa ‘kigodoro’, ibada za makanisani zinazozidi
matakwa ya kisheria ya uanzishwaji wa makanisa hayo katika jamii,
atapaswa kulipa Sh milioni 10 ndipo aruhusiwe kuendelea na shughuli
yake.
Kwa
mujibu wa NEMC, ruhusa hiyo inayo lipiwa, pia ina muda na viwango
vyake, ambapo kila muda husika unapoisha, kelele zinapaswa kupunguzwa
ama kuzimwa. Hii inahusisha pia baa na kumbi za starehe za usiku.
Baya
aliitaka jamii kuepuka uchafuzi huo wa mazingira wa kelele na mitetemo,
ambao watu wengi wamekuwa wakidhani si tatizo. Alitaka watu kuheshimu
matakwa ya sheria na kanuni kwa nyakati za mchana na usiku.
“Tumekuwa
tukipokea malalamiko kutoka kwa watu wengi, wakilalamikia usumbufu wa
kelele na mitetemo kutoka kwa watu wanaoendesha shughuli mbalimbali za
kiuchumi na kijamii katika jamii,” alifafanua Baya.
Alitoa
angalizo kwa wanaotumia vyombo vya muziki na sauti katika maeneo ya
makazi, ambavyo vimeleta madhara kwa afya za watu. Alisema matumizi ya
vipaza sauti na vyombo vya sauti kubwa, wanapaswa kuwa na kibali
maalumu.
Alieleza
kuwa kanuni za kelele na mitetemo, zimeweka vigezo na viwango vya sauti
kwa ajili ya kudhibiti uchafuzi wa mazingira katika maeneo ya
hospitali, makazi, migodini, kumbi za kijamii, kumbi za usiku za
starehe, matangazo, baa na maeneo mengine.
Baya
alisema baraza limepata changamoto kadhaa, ikiwamo uelewa mdogo wa
jamii kuhusu kiwango cha sauti kinachotakiwa na kisichoruhusiwa na
baadhi ya watu kwa makusudi huvunja sheria.
Kuhusu
faini, alisema sheria ya mazingira imeweka wazi faini kwa wanaokiuka na
kuchafua mazingira kwa kelele na mitetemo. Faini hiyo haiingiliani na
tozo la Sh milioni tano hadi Sh milioni 10 lililoelezwa, ambapo mtu
anapaswa kulipa si chini ya Sh milioni 50 na si zaidi ya Sh milioni 50
ama kifungo jela.
Kaimu
Mkurugenzi wa Usimamizi wa Sheria za Mazingira wa NEMC, Ruth Lugwisha
alisema tatizo la kelele na mitetemo, limekuwapo kwa muda mrefu. Alisema
tangu kupitishwa kwa kanuni, tayari watu kadhaa wamewajibishwa.
Alisema
miongoni mwa waliowajibishwa ni makanisa, kumbi za starehe na baa. Hata
hivyo, hakuwa tayari kuwataja wahusika wala maeneo. Alisema
uwajibishwaji huo ulihusisha faini, kufungiwa na onyo.
0 comments:
Post a Comment