https://play.google.com/store/apps/details?id=com.blog.ya.watanzania


.

.

.
  • Latest News

    .

    Taarifa Fupi Kuhusu Ziara Ya Rais Wa Vietnam Nchini Tanzania Tarehe 9-10 Machi 2016


    Utangulizi
    Rais wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam Mheshimiwa Truong Tan Sang anatarajiwa kufanya ziara rasmi nchini tarehe 9 Machi 2016.  
    Madhumuni ya  ziara hiyo ni kukuza uhusiano baina ya Vietnam na Tanzania mbao umedumu kwa zaidi ya miaka hamsini tangu kuanzishwa kwake pamoja ‎Kufungua maeneo mapya ya Ushirikiano wa kiuchumi baina ya Tanzania na Vietnam. 
    Hii ni ziara ya kwanza ya kiongozi huyo Barani Afrika tangu aingie madarakani mwaka 2011, ambapo nchi nyingine anayotarajiwa kutembelea ni Mozambique. 
    Rais Truong anatarajiwa kufuatana na mke wake Bi Mai Thi Hahn, mawaziri 4 wanaoshughulika na sekta za  Kilimo, Mawasiliano Uwekezaji, Afya,Viwanda na Biashara.  Aidha mgeni huyo atafuatana na ujumbe wa wafanyabiashara 30 kutoka Vietnam. 

    Shughuli za msingi zitakazofanyika kwenye ziara
    Wakati wa ziara hiyo Rais Truong Tang San atafanya mazungumzo rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. John Pombe Joseph Magufuli Ikulu jijini Dar-es-Salaam.
     
    Aidha, Rais Truong pia atapata fursa ya kutembelea eneo la EPZ la Ubungo kuangalia viwanda mbalimbali vinavyozalisha bidhaa za kuuza nje
     
    Baada ya kutembelea EPZA Rais Truong atahudhuria mkutano wa biashara na uwekezaji katika ukumbi wa mikutano wa Julius Nyerere. Mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na taasisi za umma na sekta binafsi kutoka Tanzania na Vietnam.
     
    Rais Truong atamaliza ratiba yake kwa kuhudhuria dhifa ya Taifa itakayoandaliwa kwa heshima yake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk.John Pombe Joseph Magufuli.

    Wasifu wa Rais wa Vietnam‎
    M‎heshimiwa Truong Tan Sang amezaliwa tarehe 21 January 1949 katika Jimbo la Long An nchini Vietnam. Amepata Elimu ya Juu kutoka taasisi ya national Academy of Public Administration ya Vietnam ambako alipata Shahada ya kwanza ya Sanaa na Sheria.
     
    Kutokea mwaka 1966 hadi 1996 Mheshimiwa Truong ameshika nafasi mbalimbali za utendaji  katika Chama Tawala cha kikomunisti cha Vietnam.
     
    Mwaka 1996 Mhe Truong alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Tawala na Katibu wa Chama hicho katika Jimbo la Ho Chi minh hadi mwaka 2000 ambapo aliachia wadhifa wa katibu Mkuu wa Jimbo na kuendelea na nafasi ya ujumbe wa Kamati kuu ya Chama tawala hadi tarehe 25 Julai 2011 alipochaguliwa na Bunge la Vietnam kuwa Rais wa Vietnam.
     
    Mhe Truong amemuoa Bi mai Thi Hanh  na wamejaaliwa mtoto mmoja.

    Taarifa Muhimu Kuhusu Vietnam‎
    Historia fupi ya Vietnam
    Vietnam ilifanya mapinduzi tarehe 14 Agosti 1945 na hatimaye kupata uhuru tarehe 2 Septemba 1945 ikijulikana kwa jina la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Vietnam. 
    Pamoja na kupata uhuru nchi hiyo iliendelea kuwa na migongano baina ya Vietnam ya Kaskazini na Kusini iliyopelekea vita iliyodumu kwa muda mrefu na kuhusisha mataifa ya nje. 
     
    Kufuatia kumalizika kwa vita, Vietnam ya Kaskazini na Kusini ziliungana tena na kuunda Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam tarehe 2 Julai 1976. 
    Nchi hiyo yenye kilomita za mraba 329,560 iliyopo kusini mashariki mwa Asia ina watu milioni 91.7 na inaongozwa na Chama cha Kikomunisti cha Vietnam.

    Mafanikio ya Uchumi ya Vietnam
    ‎Vietnam ni moja ya nchi zilizopiga hatua kubwa ya maendeleo barani Asia.
    Mwaka 1986 Serikali ya Vietnam ilianzisha mageuzi makubwa ya uchumi yaliyopelekea kuitoa nchi hiyo kwenye kundi la nchi masikini yenye kipato cha Dola za Kimarekani 100 kwa kila mtu hadi kufikia kuwa nchi yenye uchumi wa kati yenye kipato cha Dola za kimarekani 2000 kwa kila mtu mwaka 2014. Katika mageuzi hayo,Vietnam imefanikiwa kupunguza umasikini wa wananchi wake kwa asilimia 50.

    Mafanikio katika Sekta ya Kilimo
    Sifa kuu ya Vietnam ni uthubutu na uwezo wa kusimamia mipango yake. Mfano mwaka 1980 nchi hiyo iliamua kuingia kwenye uzalishaji mkubwa wa kahawa. 
    Ndani ya miaka 10 iliweza kufikia uzalishaji wa tani 300,000 kwa mwaka na hatimaye kuwa nchi inayoongoza ulimwenguni katika uzalishaji na uuzaji wa kahawa aina ya Robuster. 
    Vilevile miaka ya 1990, Vietnam ilikuwa ikiagiza mchele kutoka nje, kufuatia hatua madhubuti walizochukua mwaka 2004 ilishika nafasi ya pili duniani katika uzalishaji wa mchele kwa kuwa na misimu mitatu ya mavuno.
     
    Hivi sasa Vietnam imejiwekea malengo ya kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa sukari duniani ambapo mwaka 2015 uzalishaji wake umefikia tani milioni 2 kwa mwaka.‎ 
    Mbali na mazao hayo, Vietnam inaongoza ulimwenguni kwa kuuza korosho na pilipili manga. Vilevile,Vietnam ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwenye kilimo cha muhogo na mpira. 
      ‎
    Mafanikio makubwa ambayo Vietnam imeyapata katika kuongeza uzalishaji katika sekta ya kilimo, yamekuwa chachu ya ukuaji wa sekta ya viwanda ambayo kwa sasa ndio imeshika hatamu ya uchumi wa Vietnam‎.
     
    Mkakati wa Mageuzi ya Kijamii na Kiuchum 2011-2020
    Aidha, Vietnam inatekeleza mkakati wake wa kuwezesha mageuzi ya kijamii na kiuchumi wa mwaka  2011-2020 ambao umejikita kwenye kuwapatia wananchi elimu na stadi za ufundi‎ kwa ajili ya kufanya kazi kwenye viwanda vinavyotumia teknolojia ya kisasa na ubunifu; kuboresha taasisi zinazoshughulika na masoko; na kuendelea na ujenzi wa miundombinu.
     
    Mkakati huo unaendana na utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa nchi hiyo ambao kwa sasa umelenga kufanya mageuzi makubwa katika taasisi za kibenki ili kuwezesha wananchi kupata mitaji ya kufanya shughuli za uchumi na maendeleo; na mageuzi ya makapuni ya biashara ya Serikali ili yaweze kushindana katika uchumi wa soko ndani na nje ya nchi pasipo kutegemea ruzuku kutoka Serikalini.‎
     
    Ni dhahiri kwamba yapo mambo ambayo Tanzania inaweza kujifunza kutoka Vietnam katika safari yake ya kuwa nchi ya uchumi wa Kati ifikapo mwaka 2025. Tanzania inayo nafasi kubwa ya kuongeza uzalishaji katika mazao ya miwa,mpunga na uvuvi kwa kupitia ushirikiano na Vietnam.

    Mahusiano ya Vietnam na Tanzania‎
    Mahusiano ya Tanzania na Vietnam yaliyojengwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Kiongozi wa Vietnam Ho Chi Minh mwaka 1960 na kupelekea kuanzishwa rasmi kwa mahusiano ya kidiplomasia mwaka 1965. Kwa muda mrefu mahusiano hayo yalikuwa ya kisiasa zaidi ambapo Tanzania iliunga mkono harakati za Vietnam za kupinga uwepo wa majeshi ya kigeni kwenye ardhi yake.

    Ziara za Kukuza Mahusiano za Viongozi Wakuu
    Aidha katika kipindi cha miaka 50 ya mahusiano ya kidiplomasia baina ya Vietnam na Tanzania, viongozi wa kitaifa wa nchi hizi mbili wamefanya ziara za kudumisha mahusiano baina ya nchi hizi mbili. Tarehe 25 Septemba 1973, Rais wa Vietnam Mheshimiwa Nguyen Huu Tho alifanya ziara nchini Tanzania. 
     
    Kwa upande wa Tanzania, viongozi waliofanya ziara nchini Vietnam ni pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa (2004); Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Awamu ya Nne Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete (2014), Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk Ali Mohamed Shein (2012); Mawaziri Wakuu wa Serikali ya Awamu ya Nne ya Jamhuri ya Muungano‎ Mhe.Edward Lowassa (2006); na Mhe. Mizengo Kayanza Pinda (2010).

    Mikataba ya Mahusiano baina ya Tanzania na Vietnam
    Katika jitihada za kuimarisha mahusiano, mwaka 2001 Tanzania na Vietnam zilisaini Mkataba wa Ushirikiano wa Kuichumi na ufundi‎.  Mkataba huo uliainisha maeneo ya ushirikiano yafuatayo:
    1. Kubadilishana uzoefu katika sekta ya kilimo na maendeleo vijijini;
    2. Kubadilishana uzoefu katika matumizi ya sayansi na teknolojia katika kuendeleza kilimo cha umwagiliaji, uvuvi na misitu;
    3. Kupeana taarifa za fursa za masoko ya bidhaa za kilimo
    4. Vietnam kuipata Tanzania utaalam na teknolojia ya uvunaji na utunzaji wa maji
    5. Mwaka 2014 Tanzania na Vietnam zilisaini Mkataba wa ushirikiano katika sekta ya mawasiliano ambapo kupitia mkataba huo kampuni ya Vietel  inayomilikiwa na Jeshi la Vietnam imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya mawasiliano nchini na kuzalisha ajira za moja kwa moja kwa watanzania 1600 na fursa za kujiajiri kwa watanzania 20,000. Vilevile,kampuni hiyo kupitia mkataba uliosainiwa,itatoa huduma za internet bure kwenye mashule na mahospitali ya Serikali vijijini.

    -Mwisho-
    Imetolewa na:
    Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
    Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dar es Salaam
    03 Machi, 2016

    ==
    https://play.google.com/store/apps/details?id=com.blog.ya.watanzania

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Post a Comment

    Item Reviewed: Taarifa Fupi Kuhusu Ziara Ya Rais Wa Vietnam Nchini Tanzania Tarehe 9-10 Machi 2016 Rating: 5 Reviewed By: Unknown
    Scroll to Top