https://play.google.com/store/apps/details?id=com.blog.ya.watanzania


.

.

.
  • Latest News

    .

    Waziri Mkuu Aagiza Daktari Hospitali ya Ligula Mtwara Asimamishwe Kazi Kwa Kuomba Rushwa Ya Sh. 100,000



    WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameagiza kusimamishwa kazi kwa Dk. Fortunatus Namahala wa kitengo cha upasuaji katika hospitali ya Ligula ambayo ni hospitali mkoa wa Mtwara kutokana na tuhuma za kumdai mgonjwa rushwa ya sh. 100,000/-.
     
    Pia ametoa agizo la kufungwa kwa maduka yote ya dawa yaliyo nje ya hospitali hiyo kuanzia leo na kumtaka Katibu Tawala wa Mkoa huo, Bw. Alfred Luanda asimamie zoezi hilo mara moja.

    Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Februari 29, 2016) kwenye kikao cha watumishi wa hospitali hiyo alichokiitisha baada ya kutembelea maeneo kadhaa ya hospitali hiyo na kupokea malalamiko kutoka kwa wagonjwa na ndugu wenye wagonjwa waliolazwa.

    Mara baada ya kuwasili, Waziri Mkuu aliamua kwenda mojamoja mapokezi badala ya wodini kama alivyopangiwa na kuuliza maswali ni kwa nini wana dirisha moja la kupokelea wagonjwa wote. “Dirisha la wazee lipo?” akajibiwa hakuna. “Dirisha wa watu wa Bima ya Afya (NHIF) lipo” nalo pia akajibiwa halipo. “Je wazee wana daktari wao”, hakupata jibu.

    “Mganga Mkuu ni kwa nini hujatenga dirisha la wazee wakati haya maelekezo yalishatolewa siku nyingi? Tengeni dirisha la wazee  na uhakikishe wana daktari wao. Siyo kuwaleta huku ili waje kusukumana na wagonjwa vijana,”  alisema wakati akimwagiza Mgaga Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Shaibu Maarifa.

    Akiwa njiani kuelekea wodi aliyopangiwa kuiona, Waziri Mkuu alikutana na kundi la wagonjwa waliokuwa wakiimba “tuna jambo, tuna jambo” wakiashiria kutaka kusikilizwa. Kati ya wauguzaji watatu aliowasikiliza, Waziri Mkuu alipokea kero za kuuziwa dawa kwa bei za juu kwenye maduka ya dawa binafsi, lugha mbaya za madaktari na wauguzi, uchafu wa vyoo na uhaba wa maji.

    Lakini kero ya Bi. Tatu Abdallah aliyelazimika kuuza shamba la baba yake ekari 2.5 ili apate fedha za kulipa gharama za kufanya upasuaji kwenye hospitali binafsi baada ya baba huyo kutimuliwa kutoka hospitali ya Ligula ndiyo ilimgusa zaidi Waziri Mkuu.
     
    “Februari mosi nilimleta baba yangu hapa nikaambiwa anatakiwa kufanyiwa upasuaji. Nikaandikiwa ninunuue dawa za sh. 85,000/- hapo nje (pharmacy haikumbuki jina) pia uzi wa kushonea kwa sh. 25,000/-. Lakini pia daktari akasema anataka sh. 100,000/- ya kwake. Lakini hadi Februari 7 hakufanyiwa huo upasuaji.”

    “Tarehe 12 Februari  baba alitolewa wodini na kuambiwa arudi tarehe 16 Februari. Niliumia sababu kijiji tunachotoka ni mbali na hali ya baba ilizidi kuzorota. Ndipo baba akaniambia nirudi kijijini kwetu Kilomba nikauze ekari 2.5 za shamba lake ili tulipie matibabu. Niliuza na kumpeleka baba katika zahanati ya Sajora. Huko nililipa sh. 560,000/- na baba akafanyiwa upasuaji sasa hivi yuko nyumbani”.

    “Leo nataka huyu daktari aje achukue boksi hili la dawa alizoniandikia na pia anirudishie hela yangu iliyopotea bure. Mie sijazitumia, ni kwa nini aliniandikia wakati baba hajampa huduma yoyote?” Alipoulizwa kama anaweza kumtambua akimuona, mama huyo alikiri kuwa anaweza.

    Waziri Mkuu alitembelea pia wodi ya akinamama waliojifungua na kukuta wakiwa wametandikiwa shuka moja na wagonjwa kulazimika kuweka khanga juu ya mipira wanayolalia wodini ambayo pia wanaambiwa wajinunulie kabla ya kwenda hospitali kujifungua.

    Akiwa njiani kuelekea theatre, Waziri Mkuu alipata kilio cha wagonjwa wengine ambao walisema hospitali hiyo haina maji, choo kinachotumika ni kimoja na kwamba usafi umefanyika leo waliposikia kuwa atatembelea hospitali hiyo.

    Akiwa katika kikao na watumishi hao, Waziri Mkuu aliwainua madaktari wote ili wajitambulishe ndipo akamuomba mama aliyedaiwa rushwa aende kumshika mkono daktari mhusika.
     
    “Gwaride la utambuzi ni jambo la kawaida. RPC hakikisha huyu mama hasumbuliwi. Lakini leo nitaanza na huyu Daktari kwa sababu rushwa haivumiliki. RAS simamia suala lake lakini pia shirikiana na TAKUKURU na Polisi kufanya uchunguzi wa jambo hili hadi mwisho,” alisema.

    Kuhusu madai na stahili za watumishi, Waziri Mkuu amemwagiza RAS, RMO na Afisa Utumishi wa mkoa wafanye kikao na watumishi wote wa hospitali hiyo leo saa 9 alasiri na kisha wamletee taarifa.

    Kabla ya kufikia uamuzi wa kumsimamisha Dk. Namahala, Waziri Mkuu alitumia muda mwingi kuwaelezea watumishi hao jinsi walivyo na umuhimu katika huduma zao na kwamba nafasi yao ni nyeti kwa maisha ya binadamu hivyo wanapaswa kuwa na huruma na siyo kuwaumiza wananchi wa kipato cha chini ambao hawana uwezo wa kumudu gharama za matibabu.

    Aliwataka waache tabia ya kuwatoza fedha watoto wanaolazwa hospitalini hapo na wanawake wanaojifungua kwani wanapaswa kutibiwa bure kwa mujibu wa sera ya Serikali.

    Sakata la hospitali ya Ligula lilianza juzi (Jumamosi, Februari 27, 2016) wakati Waziri Mkuu akiwahutubia mamia ya wakazi wa Mtwara kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa mashujaa ambapo baadhi yao walikuwa wakichomekea kuwa aende hospitalini hapo kwa kuwa kuna majipu ya kutumbua.

    Waziri Mkuu aliwajibu kuwa amesikia ujumbe wao na ataenda huko lakini alishindwa kutokana na ratiba za siku hiyo kumalizika jioni sana.

    Waziri Mkuu amerejea Jijini Dar es Salaam mchana leo.
    https://play.google.com/store/apps/details?id=com.blog.ya.watanzania

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Post a Comment

    Item Reviewed: Waziri Mkuu Aagiza Daktari Hospitali ya Ligula Mtwara Asimamishwe Kazi Kwa Kuomba Rushwa Ya Sh. 100,000 Rating: 5 Reviewed By: Unknown
    Scroll to Top