https://play.google.com/store/apps/details?id=com.blog.ya.watanzania


.

.

.
  • Latest News

    .

    WARIOBA ATOA YA MOYONI JUU YA UCHAGUZI MKUU ULIVYOKUWA,APONDA MAMBO HAYA...!!!






    Aidha, Jaji Warioba ameendelea ‘kuililia’ rasimu ya Katiba iliyotayarishwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba aliyokuwa akiiongoza, akieleza maeneo muhimu yanayopaswa kuwapo katika Katiba inayopendekezwa kabla ya kupigiwa kura ya maoni.


    Pia, amebainisha kasoro kadhaa zilizojitokea katika uchaguzi mkuu mwaka jana, ambazo amesema zisipofanyiwa kazi taifa litaendelea kudidimia na kushindwa kuimarisha demokrasia.

    Jaji Warioba alisema hayo jijini Dar es Salam jana, wakati akizungumza katika mkutano wa kitaifa wa tathimini ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana ulioandaliwa na Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (Redet) kwa kushirikiana na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

    Warioba ambaye alikuwa Waziri Mkuu enzi za Mwalimu Nyerere, mbali na kutaja maeneo tisa ambayo anataka yaangaliwe katika Katiba pendekezwa iliyoandaliwa na Bunge Maalum la Katiba kabla ya hatua ya kura ya maoni endapo Tanzania inataka kujipambanua kuwa na demokrasia bora.

    Hata hivyo, Jaji Warioba alisifia uchaguzi mkuu uliopita kuwa ulikuwa huru na haki pamoja na mamlaka husika kuwajibika kutoa hamasa kwa wapigakura.

    Mambo tisa aliyoainisha akitaka yapewe nafasi katika Katiba pendekezwa ni:-

    KURA ZA RAIS, KUHOJI MATOKEO

    Jaji Warioba alisema kwa mujibu wa Katiba, Rais anachaguliwa kwa wingi wa kura hata kama hazikufika nusu ya wapigakura na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ikishatangaza hakuna anayeruhusiwa kuhoji kokote.

    “Haya ni mambo yanayozungumziwa na kulalamikiwa kwa muda mrefu, Rais ni wa taifa hata kama anatokana na chama cha siasa ni vizuri achaguliwe na wengi na siyo wingi wa kura. Ni vizuri apate zaidi ya nusu na iruhusiwe kuhoji matokeo. Katiba mpya ndiyo itakayoondoa vikwazo hivi,” alisema.

    Jaji Warioba ambaye alikuwa mchokoza mada, alisema muundo wa sasa hausaidii vyama vidogo, bali kuvibeba vikubwa ilhali wanawakilisha kundi kubwa kuliko la waliopiga kura.

    VITI MAALUM

    Alisema mapendekezo yao ni kupatikana kwake kuwe kwa uwiano na kusiwe na makadirio ya theluthi moja ili kuondoa kuwa wa daraja la chini na kukosa nguvu ya moja kwa moja kwa wananchi.
    “Madhara ni kuwa na Bunge kubwa kila mwaka, tunaogopa nini kwenda kwenye kura ya uwiano?” alihoji.

    Kwa upande wa Zainzibar, alisema Katiba yao imeeleza kuwa chama kitakachopata asilimia 10 kinakuwa sehemu ya serikali na kwamba kuna umuhimu wa kura ya uwiano ili vyama vidogo, wanawake na makundi mengine yawakilishwe vyema.

    Alisema kikwazo kingine kwa viti maalum ni kutengwa kikatiba, kama kutokuwa waziri mkuu.

    TUME HURU YA UCHAGUZI

    Jaji Warioba alisema licha ya Nec kufanya vizuri katika uchaguzi wa mwaka jana, lakini baadhi ya wadau wa uchaguzi hawana imani na tume hiyo na wana malalamiko mengi.

    "Lazima tufanye namna ya kuifanya iaminike kwa wadau wote. Ndiyo maana kwenye rasimu ya wananchi tulipendekeza kuwe na kamati maalum, mwenyekiti wake awe Jaji Mkuu itakayopeleka majina kwa Rais kwa ajili ya kuteua na majina ya wajumbe yapelekwe bungeni kwa uthibitisho,” alisema.

    Kuhusu watumishi wa tume mikoani wanaotumika watumishi wa umma ambao mara kwa mara wamelalamikiwa kuharibu uchaguzi, alisema rasimu ilipendekeza kuwapo kwa wasimamizi wa kanda watakaowajibika katika eneo husika ambao watakuwa watumishi wa Nec.

    GHARAMA ZA UCHAGUZI

    Alisema sheria ya uchaguzi ipo lakini haiwezi kutekelezwa kwa kuwa vyama vikubwa vina nafasi ya kupata fedha nyingi kuliko vidogo.

    “Uchaguzi wa mwaka jana waliweka fedha mbele, moja ya kitu kinachoumiza uchaguzi ni matumizi makubwa ya fedha. Uchaguzi umekuwa biashara, wanaotafuta nafasi kwa kununua ni lazima waangaliwe.

    TUME HAKI ZA BINADAMU

    Alisema katika rasimu walipendekeza kuwapo kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, lakini Bunge lilitupa.

    “Tuanze kujenga misingi tuwe na tume za kitaifa. Cha kwanza ni utu ukishasema binadamu wote ni sawa hutawabagua, mtaona wote ni sawa, uwazi na uwajibikaji.”

    TUME YA MAADILI

    Alisema wakati wa mchakato wa mabadiliko ya Katiba walipokea maoni ya wananchi mengi yakizungumzia maadili yameporomoka sana ndani ya jamii na kwa viongozi.

    “Tuliona haitoshi tukaona tuweke misingi na miiko ya uongozi na kuwe na utaratibu wa kusimamia na tulisema kuwe na tume yenye madaraka badala ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora isimamie haki za binadamu. Ya Uwajibikaji iwe na tume ya maadili na siyo sekretarieti iliyopo sasa ,” alisema na kuongeza:

    “Kama kuna kitu kimeniumiza sana kwenye rasimu ni kuondoa hili (Tume ya Maadili), yaani ilivyovurugwa nilikuwa nashangaa sana na kusema uzalendo ni sifa ya uongozi ya utawala bora, uzalendo unataka mtu mwenye utawala bora, ni hazina. Hili tulifanyie kazi tutahangaika sana tusipokuwa na utamaduni huu ni bure,” alisema. 

    RUSHWA

    Jaji Warioba alisema bado kuna kazi kubwa ya kufanya ndani na nje ya vyama kwani matatizo ya rushwa yanaanzia kwenye vyama, viongozi kutumia madaraka yao vibaya, viongozi kuwa wepesi kuinyooshea Nec vidole na kutaka ibadilishe badhi ya mambo ambayo ndani ya vyama vyao wameshindwa kuyafanya.

    Alisema kukiwa na vyama ambavyo havina demokrasia hukuwezi kuwa na uchaguzi wa kidemokrasia, hivyo ni lazima kupiga kelele kuhakikisha demokrasia inakuwapo.

    MUUNGANO

    Aidha, Jaji Warioba ambaye hakueleza kwa undani suala hilo, alisema mambo ambayo Mwalimu Nyerere aliyawekea mkazo mkubwa ni kupinga rushwa na ufa katika Muungano ambao ni lazima ushughulikiwe na kwamba ni moja ya mambo ya msisitizo kwenye Katiba.

    MGOMBEA HURU

    Alisema wakati wa mchakato wa maoni ya wananchi, wengi walitaka kuwapo kwa mgombea binafsi na kuondokana na utaratibu wa vyama pekee kuwa na nguvu, lakini Bunge Malum liliweka mapendekezo hayo na masharti magumu katika sheria ngumu ambayo haiwezi kubadilishwa kwa haraka huku wagombea wengine wakiongozwa na sheria ya uchaguzi.

    “Uchaguzi ulikwenda vizuri, lakini kuna mambo yalijitokeza ambayo lazima tuyaboreshe ili tuendako uwe mzuri zaidi wa haki zaidi na kuimarisha demokrasia. Katika mchakato wa Katiba mpya kuna mambo ya jumla ambayo lazima yaangaliwe vinginevyo yataleta matizo makubwa katika nchi,” alisema. 

    AMFAGILIA MAGUFULI

    Mbali na kuelezea mambo hayo, pia Jaji Warioba aliisifu serikali ya awamu ya tano nayoongozwa na Rais Jaohn Magufuli kuwa mwanzo wake ni mzuri kwani imeweka msisitizo katika maadili , uadilifu, kubana matumizi, kupiga vita rushwa, kupeleka fedha mahali wananchi watanufaika na kupiga vita ufisadi.

    Alisema mwenendo huo unapaswa kuwa mwitikio nchi nzima pamoja na kuangalia namna ya kuwa sehemu ya Katiba.

    KSORO CHA UCHAGUZI 2015

    Alisema katika uchaguzi wa mwaka jana lugha za kejeli, matusi na kebehi vilitawal, huku vyombo vya habari vikitumika na kutia doa na kwamba umeacha majeraha makubwa kwani kwenye siasa lugha za kupingana kwa hoja zinakubalika ila za kujeruhi moyo ni ngumu kutibu.

    Alisema lugha mbaya inaleta uhasama kati ya wananchi na kwamba lugha iliyotumika katika uchaguzi huo imeacha makovu na kwamba sasa viongozi waliotumia lugha hizo dhidi ya wengine wanashindwa kusalimianana, hivyo ni vyema kukosoa kwa ustaarabu.

    Jingine ni ubaguzi wa dini, ukabila, uvyama na ukanda ambavyo vinaendelea hadi sasa kwenye mitandao ya kijamii, hivyo visipo shughulikiwa taifa litafika pabaya. 

    VYOMBO VYA HABARI

    Jaji Warioba alisema hakuna chombo cha habari ambacho hakikuonyesha upande kisiasa, huku baadhi vikiwa na ushabiki wa wazi na kwamba waliotoa tathimini ya utendaji wa vyombo vya habari wakati wa uchaguzi walijikita katika idadi ya habari tuna si maudhui.
    https://play.google.com/store/apps/details?id=com.blog.ya.watanzania

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Post a Comment

    Item Reviewed: WARIOBA ATOA YA MOYONI JUU YA UCHAGUZI MKUU ULIVYOKUWA,APONDA MAMBO HAYA...!!! Rating: 5 Reviewed By: Unknown
    Scroll to Top