Hatimaye mjane aliyemwaga machozi mbele ya Rais John Magufuli akidai
kudhulumiwa mali ya urithi, amepewa nyumba na shamba baada ya Mkuu wa
Wilaya ya Babati mkoani Manyara, Crispin Meela kusuluhisha mgogoro wa
umiliki wa mali hizo.
Hivi karibuni akiwa mjini Babati, Rais Magufuli alimuagiza Meela
ahakikishe mjane huyo, Mwanaidi Mussa anapewa mali zake ikiwamo nyumba
na shamba zilizokuwa zinadaiwa kuchukuliwa na mke mdogo kinyume cha
sheria.
Meela alimkabidhi nyumba na shamba la ekari 2.5 mjane huyo juzi na
kuagiza mke mdogo kama hakuridhika na uamuzi, akakate rufaa mahakamani.
Meela pia aliwataka wananchi kuacha kurubuniwa na watu wachache wenye
maslahi binafsi na badala yake wafuate maelekezo yanayotolewa na vyombo
vya sheria.
“Migogoro ya mirathi imeendelea kukithiri katika maeneo mengi nchini
kutokana na watu kutofuata sheria za mirathi na wengine wakitaka
kunufaika na mali zinazoachwa na marehemu,” alisema Meela.
Mwanaidi ambaye amezeeka, alidai kwa muda mrefu amewaomba viongozi wa
Serikali ya mtaa anaoishi wamsaidie, kutatua tatizo lake lakini
walimpuuza.
Mke mdogo, Asia Musa alidai kuwa nyumba hiyo aliyokabidhiwa Mwanaidi,
aliijenga na mumewe kauli ambayo ilikinzana na ya mke mkubwa aliyedai
kuwa wakati Asia anaoelewa alikuta nyumba ameshaijenga na mumewe.
0 comments:
Post a Comment