Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amempongeza
Mufti wa Tanzania Sheikh Aboubakar Zubeir bin Ali kwa juhudi zake za
kuwaunganisha waislamu wote na kupanua uwigo wa Baraza Kuu la Waislamu
Tanzania (BAKWATA) kutoa huduma za kijamii na ameahidi kuwa serikali ya
awamu ya tano itaunga mkono juhudi hizo.
Rais
Magufuli ameyasema hayo leo tarehe 06 Julai, 2016 wakati akihutubia
Baraza la Eid el-Fitr kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe kuwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lililofanyika kitaifa katika viwanja
vya Karimejee Jijini Dar es salaam.
Dkt.
Magufuli amesema kitendo cha kuwaunganisha waislamu wote katika Baraza
la Eid el-Fitr kinafungua ukurasa mpya na ni moja ya hatua muhimu za
kuimarisha amani, umoja na mshikamano miongoni mwa waislamu wa makundi
mbalimbali pamoja na watanzania wengine waisio waislamu.
Aidha
Rais Magufuli amezungumzia juhudi zinazofanywa na BAKWATA katika
kuimarisha taasisi zake zinazotoa huduma za kijamii na kulinda mali zake
akisema serikali itahakikisha mali zote za waislamu zinakuwa salama na
kwamba wote waliodhulumu mali za waislamu watazirejesha.
Awali
akisoma taarifa, Katibu Mkuu wa BAKWATA Alhaji Suleiman Said Lolila
amesema BAKWATA inakusudia kupanua huduma za kijamii kwa lengo la
kuwahudumia wananchi ikiwemo kujenga chuo kikuu Mkoani Dodoma na pia
amempongeza Rais Magufuli kwa juhudi zake za kuondoa umasikini huku
akimtaka asikatishwe tamaa na wachache watakaoudhika kwa kuguswa na
hatua zinazochukuliwa.
Nae
Mufti wa Tanzania Sheikh Aboubakar Zubeir Ali pamoja na kumshukuru Rais
Magufuli kwa kuongoza bila ubaguzi amewataka watanzania kuungana na
juhudi za serikali kupinga matendo maovu ikiwemo rushwa na ufisadi na
pia amelaani ndoa za jinsia moja akisema ni kinyume na maadili ya dini.
Baraza
la Eid el-Fitr pia limehudhuriwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa,
Rais Mstaafu wa awamu ya pili Alhaji Ali Hassan Mwinyi, mabalozi na
wabunge.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
0 comments:
Post a Comment