Serikali
imeagiza wafungwa 280 katika gereza la Kitengule wilayani Karagwe,
wahamishwe katika kipindi cha wiki moja kupelekwa gereza la Mwisa.
Watahamishwa baada ya mabweni yao kuharibiwa kwa tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera wiki iliyopita.
Agizo
hilo lilitolewa jana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu
Nchemba kwa Mkuu wa Magereza Mkoa wa Kagera, Jeremiah Nkonda.
Mwigulu
aliagiza hilo baada ya kufanya ziara mkoani hapa na kutembelea taasisi
zilizo chini ya wizara yake kwa lengo la kuona uharibifu uliojitokeza
kutokana na tetemeko hilo, lililoripotiwa kusababisha vifo vya watu 17,
majeruhi, nyumba kubomoka na uharibifu mkubwa wa majengo na miundombinu
ya barabara.
“Nimetembelea
magereza yetu, lakini gereza la Kitengule limeharibika sana, kuta
zimeanguka, mabweni yameharibika kwa kiwango kikubwa kiasi kwamba
hawapaswi kuishi watu. Kwa hiyo, naagiza mkuu wa magereza hapa
kuwahamishia wafungwa hawa katika gereza la Mwisa lenye mabweni manne
yaliyo wazi,” aliagiza Mwigulu.
Alisema
katika kipindi cha wiki moja, kazi hiyo iwe imekamilika kwa sababu
wakiendelea kuwaacha wafungwa hao katika gereza hilo lililoharibika ni
hatari, kwani wanaweza kudondokewa na kuta zinazoning’inia na
kusababisha maafa mengine.
Mwigulu
alisema kutokana na tukio hilo, Wizara inaandaa mpango wa muda mrefu wa
kujenga bweni kubwa, litakalokuwa na uwezo wa kubeba wafungwa 400 kwa
wakati mmoja kwa kuwa hilo ni gereza la kikazi linalobeba watu wengi.
Kwa
upande wake, Nkonda alisema kilichochangia zaidi kushuka kwa kuta hizo
ni kwamba matofali yaliyojenga kuta hizo yanaonekana yalikuwa mabichi.
Alisema kwa hali hiyo haitawezekana kufanya ukarabati, bali ni kuhakikisha wanabomoa mabweni hayo na kujenga upya.
Alisema
gereza hilo, lilikuwa na uwezo wa kubeba wafungwa 380 kati ya hao 100
wako kwenye kambi ndogo na 280 ndio watakaohamishiwa kupelekwa katika
gereza la Mwisa.
0 comments:
Post a Comment