https://play.google.com/store/apps/details?id=com.blog.ya.watanzania


.

.

.
  • Latest News

    .

    Ushindi wa Kilimanjaro Queens usitumike kama kichaka cha kuficha uozo TFF



    Mara nyingi wabongo tumekuwa tunatafuta kichaka cha kujifichia, sasa hivi kuna siasa zinataka kutumiwa nyuma ya kichaka cha Kilimanjaro Queens kuchukua ubingwa wa CECAFA kwa upande wa wanawake kama sehemu ya kujificha au daraja la kuwapeleka nchi ya ahadi.
    Kila mtu anakumbuka hii timu ilivyoondoka kwenda Uganda, wachezaji, benchi la ufundi pamoja na viongozi walisafiri kwa basi kutoka Dar hadi Bukoba mkoani Kagera ambako waliweka kambi ndogo kabla ya kusafiri tena kwa basi kuelekea nchini Uganda.
    Lakini baada ya kuchukua ubingwa timu ileile inarudi nyumbani kwa ndege, huu ni unafiki. Waliondoka kwa kuungaunga na basi lao, wakacheza mashindano kwasababu watu wanaandaa sherehe wanataka kutumia daraja la timu kuchukua ubingwa ndio maana wakawapandisha ndege kutoka Mwanza hadi Dar ili waonekane wamefanya kitu kikubwa.
    Kwanini hili halikufanyika wakati timu inaenda Uganda? Pesa ya kuwarudisha kwa ndege imetoka wapi na mwanzo ilikosekana vipi? Sitoshangaa kama wachezaji hawa wakisema wanadai posho kibao kutoka TFF, sasa kwanini hizo pesa za kuwasafirisha kwa ndege wasingepewa kama posho zao na hamasa baada ya kuchukua ubingwa halafu warudi tu kwa basi kama walivyoenda?
    Lazima tukubali kuwa wakweli, hivi ile tafrija ya kujipongeza ilikuwa na maana gani? Tujiulize tumechukua ubingwa mbele ya kina nani? Wenzetu ndio kwanza wanaanza kuokota wachezaji kutengeneza timu za wanawake.
    Mfano mzuri ni ndugu zetu wa Zanzibar, waliondoka na rundo la magoli kwenye mashindano hayo sisi leo hii tunafanya sherehe ya kujipongeza lazima tujiulize swali hapa timu hii imetoka wapi?
    Hakuna miundo mbinu ya soka la wanawake, nitajie vilabu ambavyo tunavishuhudia vinacheza ligi ambavyo tunapata wachezaji wa kuunda timu ya taifa ya wanawake na kupata matokeo. Timu imeokotwa-okotwa imepambana na kutwaa ubingwa tunakaa tunafanya sherehe kujipongeza, kwa kipi tulichokifanya?
    Kocha wa zamani wa Twiga Stars Rogasian Kaijage amewahi kuzungumzia namna nchi yetu isivyokuwa na mipango lakini inapotokea bahati watu wanasahau mambo yote. Alitoa mfano kwamba, ni sawa na mtu ambaye ametoka Mbeya amebeba magunia ya mahindi kwenye gari kwenda Dar. Wakati gari likisafiri njiani baadhi ya punje za mahindi zinaanguka njiani, kuna sehemu zinaanguka mahali mvua iliponyesha na mahindi yale yakaota.
    Mwisho wa siku mahindi yale yakakua na kumea vizuri, baada ya muda watu wakaja kuvuna na mwisho wa siku wanajipongeza wamepata mazao bora wakati hata hawajui yalipotokea na nani aliyeyalea hadi yakafikia wakati yamekomaa na kuvunwa.
    Mfano huu naufananisha na namna Kilimanjaro Stars ilivyochukua ubingwa, timu hii haikuandaliwa kwa ajili ya kutwaa ubingwa kule Jinja, Uganda imetokea tu kama bahati lakini cha kushangaza watu wanaipongeza utadhani kuna juhudi zilifanyika kuhakikisha timu inapata mafanikio kumbe hakuna kilichofanyika.
    Kuna taarifa zinadai kwamba, baada ya wachezaji kufika Kagera kwa basi wakitokea Uganda, walitaka wapewe pesa ambazo zilipangwa kulipia safari yao ya ndege kutoka Mwanza hadi Dar halafu wasafiri kwa basi kama walivyosafiri wakati wa kwenda.
    Wachezaji wasingethubutu kutaka wapewe nauli za safari ya ndege kama walilipwa vizuri, hii inaonesha ni jinsi gani dada zetu walivyo na njaa na hii ni hadi kwa wadogo zetu Serengeti Boys ambao walikuwa wanakula chakula cha mama ntilie pale kwenye hostel za TFF.
    Serengeti Boys wanacheza na kufanya vizuri lakini ni nani ambaye anajua kama hawa watoto hawapati posho? Wanakakomaa uwanjani na kupata matokeo Watanzania wanashangilia na viongozi wanafanya sherehe, lakini wadogo zetu wako kwenye wakati mgumu. Baada ya kuonesha dalili za kufuzu, ndio wanapewa fursa ya kuweka kambi Afrika Kusini, Rwanda na Kwingineko.
    Sipingi kwamba dada zetu wa Kilimanjao Queens wamefanya vizuri, lakini mafanikio yao yasitumike kama kichaka cha watu fulani kujificha ili kufanya mipango yao huko mbele waonekane walifanya mambo ya maana.
    https://play.google.com/store/apps/details?id=com.blog.ya.watanzania

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Post a Comment

    Item Reviewed: Ushindi wa Kilimanjaro Queens usitumike kama kichaka cha kuficha uozo TFF Rating: 5 Reviewed By: news
    Scroll to Top