Kwa
mujibu wa kifungu cha 40 (6) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya
343, Tume ilipokea Rufaa moja ya kupinga Uteuzi wa Mgombea wa Chama cha
Wananchi (CUF) katika Uchaguzi Mdogo wa Bunge Jimbo la Dimani –
Zanzibar.
Rufaa
hiyo ilikatwa na Mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bwana Juma Ali
Juma akipinga Maamuzi ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Dimani
aliyemthibitisha Mgombea wa Chama Cha Wananchi (CUF) Bwana Abdul Razak
Khatib Ramadhani kuwa ni mgombea halali.
Rufaa
hiyo ilikuwa na sababu mbili ambazo ni:- (i) Hakurudisha Fomu za Uteuzi
kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa na sheria na (ii) Hakudhaminiwa na
Chama cha Siasa kugombea Ubunge. Katika kikao chake cha leo tarehe 30
Desemba, 2016, Tume imepitia Rufaa hiyo na kuona sababu zilizotolewa na
mkata Rufaa hazina nguvu ya kisheria, kwa kuwa, Mgombea wa CUF
amerudisha Fomu za Uteuzi kwa mujibu wa sheria na taratibu.
Pia, Fomu
zake za Uteuzi zimesainiwa na kugongwa muhuri wa Katibu wa Wilaya ya
Magharibi B. Kwa mantiki hiyo, Tume imekubaliana na Uamuzi wa Msimamizi
wa Uchaguzi Jimbo la Dimani – Zanzibar. Hivyo, Mgombea wa CUF amekidhi
vigezo na uteuzi wake ni halali na aendelee na kampeni za kugombea
nafasi ya Ubunge wa Jimbo hilo.
Aidha,
kwa mujibu wa kifungu cha 44 (5) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za
Mitaa, Sura ya 292, Tume imepokea Rufaa tatu; kutoka Kata ya Kijichi –
Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Mkoa wa Dar es Salaam, Kata ya
Misugusugu – Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Mkoa wa Pwani na Kata ya
Ihumwa – Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma, Mkoa wa Dodoma.
Kata ya
Misugusugu Halmashauri ya Mji Kibaha, Rufaa ilikuwa ni ya Mgombea wa
CHADEMA Bwana Gasper Melkiory Ndakidemi dhidi ya mgombea wa Chama cha
Mapinduzi CCM Bwana Bogasi Hussen Ramadhani.
Katika
Kata ya Kijichi, Rufaa ilikuwa ni ya mgombea wa CUF Bi. Khadija Abdallah
Shamas dhidi ya mgombea wa CHADEMA Bwana Fredrick Felician Rugaimukamu.
Kata ya
Ihumwa Rufaa ilikuwa ni ya Mgombea wa CHADEMA Bwana Magawa Edward Juma
dhidi ya maamuzi ya Msimamizi wa Uchaguzi.Tume katika kikao chake cha
leo tarehe 30 Desemba, 2016 imepitia Rufaa zote na imeamua ifuatavyo:
Rufaa ya
mgombea wa CHADEMA Bwana Gasper Melkiory Ndakidemi katika Kata ya
Misugusugu Halmashauri ya Mji Kibaha na ya mgombea wa CUF Bi. Khadija
Abdallah Shamas katika Kata ya Kijichi, hazina mashiko ya kisheria na
zimekataliwa. Hivyo, Tume inakubaliana na Maamuzi ya Wasimamzi wa
Uchaguzi wa Halmashauri hizo na wagombea waendelee na Kampeni kwa mujibu
wa Ratiba.
Kuhusu
Rufaa ya Mgombea wa CHADEMA kutoka Kata ya Ihumwa, Halmashauri ya
Manispaa ya Dodoma. Tume, imepokea barua ya Msimamizi wa Uchaguzi,
Manispaa ya Dodoma, ikiwa imeambatishwa na barua ya Mgombea wa CHADEMA
kuiondoa Rufaa yake na kwamba anakubaliana na maamuzi ya Msimamizi wa
Uchaguzi ambayo yalimuengua. Pia, leo Tume imepokea barua za kujitoa
Ugombea za wagombea wa CHADEMA na ACT - WAZALENDO katika Kata ya Ihumwa.
Kwa maana hiyo Rufaa iliyokuwa imekatwa na mgombea wa CHADEMA Kata ya
Ihumwa imeondolewa kwa kuwa mkata Rufaa ameiondoa na amejitoa ugombea
kabla haijasikilizwa.
Mwisho,
Tume inavisisitiza Vyama vya Siasa, Wagombea na Wananchi wote wa maeneo
yenye Uchaguzi Mdogo kufanya Kampeni za kistaarabu kwa mujibu wa Sheria,
Kanuni na Maadili ya Uchaguzi.
Imetolewa na:-
Jaji Mkuu (Mst. Znz) Hamid M. Hamid
MAKAMU MWENYEKITI
TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI
30/12/2016
0 comments:
Post a Comment