Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
*Asema wanaotaka fedha wataipata shambani
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa Ruangwa na mkoa mzima wa Lindi
wachangamkie fursa ya kulima mihogo na alizeti kwa sababu mazao hayo
yana uhakika wa soko.
Alitoa
wito huo wakati akizungumza na wananchi wa vijiji mbalimbali vya wilaya
ya Ruangwa, mkoani Lindi ambako anapita kuwasalimia wananchi wa jimbo
lake na kuhimiza kazi za maendeleo. Waziri Mkuu yuko Ruangwa kwa siku nne kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka.
“Nimekuja
na fedha, wangapi wanataka kupata fedha?” alihoji Waziri Mkuu katika
mikutano yake na kuitikiwa “Sisi” na umati wa watu walionyoosha mikono
juu kuonesha kuwa wako tayari kupokea fedha hizo. Mikutano hiyo
ilifanyika kwenye vijiji vya Namilema, Mbuyuni, Nandandara, Namkonjera,
Muhuru, Chikundi, Chibula na Matumbu.
“Mnataka
fedha siyo? Fedha iko shambani! Nimewaletea fursa ya mwekezaji
anayetaka kununua mihogo yote katika mkoa huu,” alisema Waziri Mkuu na
kusababisha kicheko kwa watu waliokuwa wakinyoosha mikono yao.
“Limeni
mtu mmoja mmoja au jiungeni kwenye vikundi ili mpate ekari tatu hadi
nne kwa sababu mna uhakika wa soko. Mwekezaji huyu anataka kununua
mihogo yote na ya wilaya hii peke yake haitoshi kiasi ambacho anataka.
Kwa hiyo tumekubaliana na wabunge wenzangu kwamba kiwanda hiki
kitajengwa Nanjilinji ambako ni katikati ya mkoa ili iwe rahisi kusomba
na kupeleka mazao hayo,” alisema.
Waziri
Mkuu alisema eneo la Nanjilinji lililoko wilayani Kilwa, linafikiwa kwa
urahisi na wakazi wote kutoka Kilwa, Nachingwea, Ruangwa, Lindi
Vijijini na Liwale.
Akifafanua
zaidi, alisema mwekezaji aliyepatikana (bado ni mapema kumtaja) yuko
tayari kufuata mazao waliko wakulima na atakuwa akiwalipa hukohuko.
“Yeye anachotaka ni mihogo ya kutosha, ndiyo maana nawasisitizia muanze
kulima zao hili kwa wingi cha msingi mfuate kanuni bora za kilimo,”
aliongeza.
Wakati huohuo, Waziri
Mkuu amewataka wakazi hao walime zao la alizeti kwa wingi kwa sababu
amekwishapatikana mwekezaji wa kununua zao hilo na kwa bei nzuri.
“Nilipokwenda
Singida nilikutana na mmiliki mmoja wa kiwanda cha kusindika mafuta ya
alizeti akasema anahitaji kununua zao hilo kwa wingi kwa sababu
inayozalishwa kule haitoshi. Ameshakuja hapa na kuangalia ardhi ya hapa
amesema inafaa kwa zao hilo,” alisema.
“Yeye
atawaletea mbegu na kila ekari moja inahitaji kilo tano. Ukivuna kila
ekari unapata magunia 20 na kila gunia lina uwezo wa kutoa lita 20. Bei
ya dumu mojala lita 20 ni sh. 60,000 kwa hiyo katika ekari yako moja una
uhakika wa kupata sh. milioni 1.2. Hata ukitoa gharama ya kulima na
palizi, bado huwezi kukosa walau sh. milioni moja kwa kila ekari.”
Alimwagiza
Mkuu wa Idara ya Kilimo (Umwagiliaji na Ushirika) wa wilaya hiyo, Bi.
Violeth Byanjweli afanye kazi ya kuratibu ni wakazi wangapi wana
mashamba ya alizeti na wangapi wako tayari kuanzisha kilimo hicho ili
mbegu zitakapoletwa iwe ni rahisi kuwasambazia huko waliko.
“Hiki
kilimo ni cha miezi mitatu tu na palizi yake ni mara moja tu. Kwa hiyo
mvua za Januari zikianza, changamkieni hiyo fursa na baada ya miezi
mitatu kila mtu atakuwa na hela yake badala ya kusubiria korosho ambazo
mnavuna mara moja kwa mwaka,” alisisitiza.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, DESEMBA 29, 2016
0 comments:
Post a Comment