Kaimu
Afisa Uhamiaji Mfawidhi wa Kituo cha mpakani Tunduma/Nakonde, Bw.
Tabaran Mzee, (aliyevaa sare za uhamiaji), akieleza namna idara hiyo
ilivyoanza utekelezaji wa uanzishwaji wa Kituo cha Pamoja cha Forodha
kati ya Tanzania na Zambia, ambapo wafanyakazi wa idara hizo kutoka nchi
hizo mbili wanafanyakazi katika jengo moja kila upande wa nchi ili
kuboresha ufanyaji biashara mpakani.
Maafisa
Forodha na Idara ya Uhamiaji katika Mpaka wa Tunduma/Nakonde (Tanzania
na Zambia), wakiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe wa Serikali
uliotembelea mpaka huo ili kukagua uanzishwaji rasmi wa Kituo cha pamoja
cha Forodha kati ya nchi hizo mbili. Waliosimama mstari wa kwanza
kuanzia kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji,
Prof. Adolf Mkenda, Mkuu wa Wilaya ya Momba-Mbeya, Bw. Juma Irando,
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Balozi Hassan Simba
Yahya na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis
Shaaban.
Katibu
Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji (anayeshughulikia
biashara na uwekezaji), Prof. Adolf Mkenda, akionesha kibao chenye namba
za simu kilichowekwa Idara ya Forodha katika mpaka wa Tunduma/Nakonde
zitakazotumiwa na wadau endapo watakuwa na malalamiko yoyote, lengo
likiwa ni kuboresha huduma katika mpaka huo ambapo huduma ya pamoja ya
forodha kati ya Tanzania na Zambia imeanza kutolewa rasmi tangu Februari
mosi mwaka huu.
Makatibu
Wakuu wa Wizara ya Fedha, Viwanda, na Mambo ya Ndani, wakizungumza na
Afisa Forodha wa Zambia aliyeko katika Kituo cha Forodha cha Tunduma
upande wa Tanzania, baada ya Ujumbe huo wa Serikali kutembelea mpaka huo
kukagua shughuli za biashara ikiwa ni siku kadhaa baada ya kuanza rasmi
kwa huduma ya Kituo cha Pamoja cha Forodha katika mpaka huo wa
Tunduma/Nakonde (Tanzania na Zambia).
Mkuu
wa Wilaya ya Momba mkoani Mbeya Bw. Juma Irando (aliyenyoosha kidole)
akieleza jambo baada ya ujumbe wa Serikali ukiongozwa na Naibu Katibu
Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban, ulipotembelea
mpaka huo kukagua shughuli za biashara baada ya kuanza rasmi kwa huduma
za Kituo cha Pamoja cha Forodha mpakani Tunduma/Nakonde.
Makatibu
Wakuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Viwanda, Biashara na
Uwekezaji, na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, pamoja na maafisa
waandamizi kutoka Ofisi ya waziri Mkuu, Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA,
Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Idara ya Uhamiaji na vyombo vya ulinzi na
usalama, wakikagua shughuli za biashara katika mpaka wa Tanzania na
Zambia (Tunduma/Nakonde)
Meneja
wa Mamlaka ya Mapato Zambia, Bw. Nase Lungu (Kulia) akitoa maelezo kwa
Ujumbe wa Tanzania namna shughuli za Kituo cha Pamoja cha Forodha
Mpakani, upande wa Nakonde (Zambia) zilivyoanza kwa mafanikio na
kupunguza usumbufu ambao watumiaji wa mpaka huo wakiwemo wafanyabiashara
walikuwa wakiupata kabla ya kuanzishwa kwa huduma hiyo
Ujumbe
wa Tanzania ukidodosa mambo mawili matatu namna shughuli za Kituo cha
Pamoja cha Forodha Mpakani, upande wa Nakonde (Zambia) kinavyo fanyakazi
pamoja na changamoto wanazokumbana nazo katika siku za mwanzo za utoaji
wa huduma ya forodha kwa pamoja katika mpaka huo wa Tunduma/Nakonde,
mapema mwezi Februari, 2017.
Kituo
cha Uhamiaji na Forodha cha Tanzania kilichoko kwenye jengo la Zambia
upande wa Nakonde, baada ya kuanzishwa kwa Kituo cha pamoja cha Forodha
cha Mpakani mwa Tanzania na Zambia (Tunduma/Nakonde)
Meneja
wa Mamlaka ya Mapato Zambia, Bw. Nase Lungu (Kushoto) akiusindikiza
Ujumbe wa Tanzania uliotembelea Kituo cha Forodha cha Zambia (Nakonde),
uliokwenda kukagua huduma ya pamoja ya forodha baada ya huduma hiyo
kuzinduliwa rasmi mapema mwezi Februari, 2017.
Katibu
Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji (anayeshughulikia
Biashara na Uwekezaji) Prof. Adolf Mkenda, akifanya mahojiano na dereva
wa lori lililokuwa likivuka mpaka kuelekea nchini Zambia, ili kubaini
changamoto zinazo wakabili wasafirishaji hao wa shehena, ambapo
walipongeza kuanza kwa utaratibu wa pamoja wa utoaji huduma mpakani na
kuomba mfumo huo usaidie kuwapunguzia muda wa kukaa mpakani.
………………………………………………………………..
Benny Mwaipaja, WFM, Tunduma
KITUO
cha Pamoja cha Forodha cha mpaka kati ya Tanzania na Zambia
(Tunduma/Nakonde) kimeanza rasmi kutumika licha ya kukabiliwa na
msongamano mkubwa wa magari unaotakiwa kupatiwa ufumbuzi wa haraka.
Kituo
hicho kimeanza kufanyakazi tangu Februari mosi mwaka huu, ambapo
watumiaji wa mpaka huo watakuwa wakihudumiwa upande mmoja wa mpaka
badala ya utaratibu uliokuwa ukitumika awali ambapo watumiaji
walilazimika kukaguliwa mizigo yao kila upande hatua iliyokuwa
ikichelewesha biashara katika mpaka huo
Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban,
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda
na Naibu Waziri wa mambo ya Ndani ya Nchi, Balozi Hassan Simba Yahya,
wameeleza kuridhishwa na kazi inayofanyika mpakani hapo kupitia mfumo
huo mpya.
Hata
hivyo baadhi ya madereva wanaosafirisha bidhaa kupitia mpaka huo wa
Tunduma na Nakonde, pamoja na kupongeza utaratibu huo mpya, wameiomba
Serikali iwasiliane na upande wa Zambia, ili waongeze kasi ya kuruhusu
malori kuendelea na safari yanapofika mpakani hapo bila kucheleweshwa
ili kwenda sambamba na kasi ya upande wa Tanzania, ambao umeboresha kwa
kiwango kikubwa utoaji wa huduma.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda,
amesema kuwa makubaliano yaliyofikiwa kati ya Serikali na watoa huduma
katika mpaka huo yalikuwa ni kuwahudumia wadau wanaotumia mpaka huo kwa
muda usiozidi siku moja na kuwataka madereva wa malori wanaokwazwa
kuwasiliana na mamlaka zinazohusika.
Prof.
Mkenda amewaonya mawakala wa Forodha katika mipaka yote nchini watakao
bainika kwa namna moja au nyingine kuwachelewesha wenye malori kwa
makusudi watafutiwa leseni zao za kufanya biashara hiyo
“Tunataka
mpaka huu wa Tunduma na Nakonde ufanye kazi kwa ufanisi na ubora wa
hali ya juu ili kuiwezesha bandari yetu ya Dar es Salaam kufanyakazi kwa
kiwango cha juu ili kukuza biashara nchini” Alisisitiza Prof. Mkenda
Amesema
kuwa Serikali imeunda timu ya wataalam wanaopitia kero mbalimbali za
mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji hapa nchini, itakayo peleka
mapendekezo namna ya kuboresha mazingira hayo kwa kuwa mchango wa sekta
binafsi wakiwemo wawekezaji, unatambuliwa na Serikali
Kwa
upande wao, Afisa Mfawidhi wa Forodha , Idara ya Forodha na Ushuru wa
Bidhaa-Tunduma, Bw. Magori Magori, na Mbunge wa Jimbo la Tunduma, Frank
Mwakajoka, wameelezea kukithiri kwa vitendo vya magendo mpakani na kero
ya vizuizi lukuki kwenye njia kuu ya Dar es salaam hadi Tunduma, hatua
inayokwaza biashara kati ya Tanzania na Zambia.
Kwa
upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina
Khamis Shaaban, ameiagiza Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kuchunguza na
kuishauri Serikali namna ya kuboresha matumizi ya pesa ya Zambia
(kwacha) ili kupunguza changamoto ya ufanyaji holela wa biashara ya
kubadilisha fedha hiyo katika mpaka wa Tunduma/Nakonde upande wa
Tanzania na Zambia na mpaka wa Kasumulu/Songwe, upande wa Tanzania na
Malawi.
Maagizo
hayo yanafuatia kuwepo kwa biashara holela ya ubadilishaji fedha hiyo
mpakani huku Benki Kuu ikieleza kuwa fedha hizo (kwacha) haziko kwenye
orodha ya fedha za kigeni zinazotambulika rasmi hapa nchini hivyo kuwa
vigumu kudhibiti mwenendo wake.
Naye
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Balozi Hassan Simba
Yahya, ameahidi kuwa wizara yeke itaifanyia kazi changamoto ya uwepo wa
vizuizi vingi vya malori yaendayo masafa marefu kwakuwa vinasababisha
adha isiyo ya lazima na kukwamisha biashara nje ya nchi.
“Kwa
kuwa malori mengi yaendayo masafa marefu kutoka Bandari ya Dar es Salaam
yanafungwa vifaa maalumu vya ufuatiliaji mwenendo wake, hakuna sababu
ya trafiki kuyasimamisha kila wakati, tunataka lori likikaguliwa Dar es
Salaam lisafiri bila kusimamishwa hadi litakapofika mpakani ambapo
litafanyiwa ukaguzi wa mwisho” aliongeza Balozi Yahya.
Kuanza
kufanyakazi kwa kituo cha pamoja cha Forodha cha mpaka wa
Tunduma/Nakonde kunafuatia maagizo yaliyotolewa na Marais Dkt. John
Pombe Magufuli na Edgar Lungu wa Zambia, alipofanya ziara ya kikazi
nchini Tanzania hivi karibuni ili kurahisisha biashara katika ya nchi
hizo nan chi wanachama wa Jumuiya ya Madola-SADC, na kama mambo yatabaki
kama yalivyopangwa, kitazinduliwa rasmi na Mawaziri wa kisekta mwezi
Machi, mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment