ALIYEKUWA nahodha wa Simba,
Mganda, Joseph Owino amerejea kwao Uganda kwa madai ya kutofautiana na
kiongozi mmoja wa juu wa Simba.
Taarifa kutoka chanzo makini
zinaeleza kuwa Owino aliingia kwenye mgogoro na viongozi wa Simba Oktoba
25 mwaka jana baada ya kumuamuru kipa kinda Peter Manyika alale chini
dakika za majeruhi katika mechi ya ligi kuu Tanzania bara waliyotoka
sare ya 1-1- na Tanzania Prisons uwanja wa Sokoine.
Manyika kwa kufuata maelekezo ya
nahodha wake Owino, alilala chini, lakini akajishitukia na kutaka
kusimama na ndipo akakutana na mpira wa juu ambao alishindwa kupangua na
kufungwa goli rahisi.
Manyika alipoulizwa kwanini
alilala, alimjibu kocha Patrick Ackson Phiri na viongozi wa Simba
akisema aliaambiwa na Owino alale chini.
Viongozi wa Simba walikasirika
ikikumbukwa walikuwa na ugonjwa wa ‘sare sare maua’ na walitaka kuvunja
mkataba wa Owino, lakini kocha Phiri alimtetea sana na kusema bado
anamhitaji.
Phiri aliwahi kukiri kuwepo kwa
mvutano wa Owino na viongozi, lakini alisema kutokana na kumtetea beki
huyo wa kati wakakubali kwa shingo upande na kuagiza asajiliwe beki
mwingine na ndipo akaletwa Juuko Mursheed.
Viongozi wa Simba hawakutaka Owino acheze, badala yake walihitaji Mursheed na Isihaka wasimame katika ngome ya ulinzi.
Baada ya kuondoka kwa Phiri kumemaliza kila kitu na kuna uwezekano mkubwa Owino asicheze tena Msimbazi.