https://play.google.com/store/apps/details?id=com.blog.ya.watanzania


.

.

.
  • Latest News

    .

    FRANK DOMAYO, MECHI MBILI, BAO MOJA, PASI YA BAO KATIKA SIFA ZA KIUNGO-MSHAMBULIZI…

    Ni kama uko nyikani, jua kali, huna maji ambayo yangeweza kukusaidia kulainisha ‘ koo’ ili kupunguza ‘ kiu’ ya maji katika mwili wako. Wataalamu wa mambo ya afya wan
    ema kuwa kiu ya maji inapomshika binadamu ni sawa na kuweka hatarini maisha yako kwa kuwa kiu ni kielelezo cha upungufu wa maji mwilini.
    DOMAYO
    Maji ni kila kitu, lakini makala haya hayana lengo la kuzungumzia mambo hayo ya kiafya badala yake najaribu kufikiria namna mchezaji wa nafasi ya kiungo, Frank Domayo alivyorejea uwanjani
    baada ya miezi saba. Domayo ndiye mchezaji ghali katika ligi ya Tanzania Bara na hakuwa amecheza mchezo wowote hadi alipopangwa kwa mara ya kwanza katika mchezo wa mzunguko wa tisa dhidi ya Stand United katika uwanja wa Kambarage, Shinyanga siku ya Jumamosi iliyopita.
    Mchezaji huyo alivuna zaidi ya milioni 90 wakati alipoondoka Yanga SC kwa uhamisho huru baada ya kuichezea timu hiyo kwa misimu miwili na kushinda ubingwa wa Bara mara moja. Kwa mara ya kwanza Domayo aliichezea Azam FC katika mchezo wa kombe la Mapinduzi dhidi ya Mtende huko Zanzibar. Alipangwa pamoja na Himid Mao, Mudhamir Yahaya katika mchezo wa robo fainali dhidi ya Mtibwa Sugar.
    BAO LA KWANZA AZAM FC,
    Domayo alifunga goli pekee lililowapa pointi tatu mabingwa hao watetezi katika mchezo mgumu ugenini dhidi ya Stand. Achana na bao hilo, mazingira ambayo mchezaji huyo alikuwepo kabla ya kukutana na mpira uliopoteza uelekeo na kufunga yanamaanisha kuwa, Domayo sasa ndiye atabeba majukumu mapya kama kiungo-mkuu-mchezesha timu akitokea katikati ya uwanja.
    Tofauti na alivyokuwa akitumika klabuni Yanga ambako alipangwa zaidi kama kiungo wa pili wa ulinzi mbele kidogo ya Athumani Iddi ‘ Chuji’, Domayo ambaye alikuwa mchezesha timu mkuu katika timu ya JKT Ruvu, ndani Yanga majukumu hayo yalibebwa kwa kiasi kikubwa na Mnyarwanda, Haruna Niyonzima ambaye alipewa uhuru mkubwa na kocha Ernie Brandts.
    Timu ilipochukuliwa na Hans Van der Pluijm mwanzoni mwa mwaka uliopita, Domayo alichezeshwa zaidi katika eneo la kiungo-namba-sita na aliweza kufanya vyema licha ya wakati mwingine kutowafurahisha wapenzi wa timu yake kutokana na kupoteza mipira huku akicheza mchezo wa taratibu. Katika timu ya Taifa, Taifa Stars kocha, Kim Poulsen alipendelea kumpanga mchezaji huyo mwenye miaka 21 kama kiungo wa ulinzi, huku mbele yake wakichezeshwa Amri Kiemba na Salum Abubakary ‘ Sure Boy Jr’.
    Lakini katika michezo minne akiwa na Azam FC, Domayo amechezeshwa kiungo wa mashambulizi akitokea kati mwa uwanja. Ni nafasi ambayo alikuwa huru kuicheza ndani ya JKT Ruvu na tayari Joseph Omog ametambua hadhina kubwa aliyonayo kikosini mwake tangu alipompanga Frank kwa mara ya kwanza dhidi ya Mtende katika ushindi wa Azam FC 1-0 Mtende, Januari 6.
    Katika mchezo huo, Omogo alimpanga Domayo pamoja na Mudathir Yahya na Himid Mao, timu ilicheza mchezo wa taratibu sana huku ikikosa nguvu katikati ya uwanja. Katika mchezo dhidi ya Mtibwa, Januari 8, Omog alifanya mabadiliko katika idara nyingine, lakini watatu hao walipangwa tena kuongoza safu ya kiungo katika mchezo huo uliomalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1. Azam ilishambuliwa sana katika mchezo huo, lakini safu ya ulinzi ikiwa na Shomary Kapombe, Erasto Nyoni, Aggrey Morris na Paschal Wawa iliweza kufanya kazi nzuri hadi timu hiyo ilipokuja kutolewa kwa changamoto ya mikwaju ya penalti.
    John Bocco, Didier Kavumbagu na Brian Majwega walianza katika safu ya mashambulizi lakini hakukuwa na nafasi rahisi iliyopatika kufuatia wachezaji wa Mtibwa kuziba njia zote za kupitisha mpira na viungo hao watatu hawakuwa na mbinu mbadala hadi Kipre Tchetche alipotokea benchi na kufunga bao la kusawazisha kwa juhudi binafsi.
    ALETA MABADILIKO KATIKA TIMU,
    ndivyo ilivyo, katika mchezo na Stand, Domayo alicheza ‘ dimba la juu’ huku namba’-6 akicheza Erasto Nyoni, na kando yao alipangwa chipukizi, Yahya ambaye amepangwa kikosi cha kwanza katika michezo sita mfululizo. Mazingira ya mchezo huo ndiyo yalimfanya Omog kumpanga Nyoni katikati ya uwanja na kumuweka benchi, Himid.
    Ukitoa uzoefu wake, Nyoni hukaba vizuri na huanzisha pasi sahihi kwa wachezaji wa mbele, mchango wake katika kukaba ulimsaidia Domayo kuichezesha timu akiwa huru na kutawanya mipira mingi katika wingi huku mara kadhaa akijaribu kupiga pasi za kupenyeza. Sure Boy hajaonekana katika michezo yote tangu kurudi uwanjani kwa Domayo, mchezesha timu huyo wa muda mrefu wa Azam anaweza kurudi uwanjani katika mchezo ujao lakini atapaswa kupambana ili kumshawishiwi kocha wake kumpanga pamoja na Domayo ili kukumbusha ‘ muunganiko wao’ uliojengwa na KIM katika timu ya Taifa.
    Katika mchezo wa Jumanne hii dhidi ya Kagera Sugar, Domayo alitengeneza bao la kuongoza lililofungwa na Kipre Tchetche na aliweza kuichezesha vizuri timu yake akishirikiana na Bolou Kipre na Yahya. Azam imefanikiwa kuondoka na pointi sita Kanda ya Ziwa ndani ya siku tatu, bila shaka Domayo amerudi kukata kiu ya mashabiki wake, klabu yake, huku Omog akimrudishia majukumu ya kiungo mchezesha timu mkuu, Frank Domayo ni namba-8 timilifu, sasa ni mchangamfu zaidi, umecheza mpira? Kiungo namba 8 hucheza kama anavyocheza sasa Domayo ndani ya Azam FC
    https://play.google.com/store/apps/details?id=com.blog.ya.watanzania

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: FRANK DOMAYO, MECHI MBILI, BAO MOJA, PASI YA BAO KATIKA SIFA ZA KIUNGO-MSHAMBULIZI… Rating: 5 Reviewed By: Unknown
    Scroll to Top