TAMKO
LA UONGOZI WA SERIKALI ZA WANAFUNZI WA VYUO VIKUU DODOMA KULAANI
KUHUSISHWA KWA WANAFUNZI WA VYUO VIKUU VYA DODOMA NA KUMUOMBA MH.
LOWASA KUGOMBEA URAIS.
Ndugu Waandishi wa habari,
Tunapenda kutanguliza shukrani za dhati kwenu kwa kufika katika eneo
hili kutusikiliza.Mbele yenu ni viongozi wa serikali za wanafunzi kutoka
Vyuo vikuu mbalimbali vilivyopo mkoani Dodoma.Ndugu waandishi wa
habari,si kawaida na wala mazoea kwa marais na viongozi wa serikali za
wanafunzi kutoka vyuo tofauti kukutana kwa pamoja na kuzungumza na nyie
wanahabari kama inavyotokea hii leo.
Ndugu wanahabari,siku ya
Jumapili ya tarehe 22 mwezi huu wa 3,kundi la watu waliojitambulisha
kama ni wanafunzi wa vyuo vikuu vya Dodoma walijikusanya nyumbani kwa
mh; Lowasa na kutoa matamko mbalimbali ikiwa pamoja na kuutangazia uma
wa watanzania kuwa sisi wanafunzi wa vyuo vikuu vya Dodoma tunamuunga
mkono na tunahitaji Lowasa awe rais wetu sambamba kumchangia pesa.
Ndugu wanahabari,Tunapenda
kukanusha kuwa wanafunzi wa vyuo vikuu vya Dodoma kwa ujumla wetu
hatukuhusika na jambo lile na kama viongozi wa serikali za wanafunzi
kutoka vyuo vikuu vya mkoa huu wa Dodoma,Tunapinga na kulaani kitendo
cha watu wachache kwenda kutuingiza sisi wanafunzi wa vyuo vikuu vya
Dodoma katika jambo ambalo halituhusu na wala si lililotuleta hapa
Dodoma.
Sisi kama wasomi ambao jamii
inatutegemea kama kioo hatuwezi kuandamana na kujikusanya kwenye nyumba
ya kiongozi na kumuomba agambee urais, wakati tunajua fika sisi
hatuhusiki na uteuzi wa wagombea ndani ya taasisi yao.Kilichofanyika ni
kuudanganya uma wa watanzania na taasiasi yake kupitia kivuli cha vijana
wachache kutoka vyuo vya hapa Dodoma,waliolipwa pesa ili waweze kuwa
kava la tukio lile.
Ndugu wanahabari,Mkoa wa
Dodoma unavyuo vikuu visivyopungua 8,Na jumla ya wanafunzi wote
tunaosoma katika vyuo vya Dodoma ni zaidi ya wanafunzi 35,000.Chuo
kikuu cha Dodoma (UDOM) pekee yake kinawanafunzi wasiopungua
22,000.Idadi ya watu waliojikusanya nyumbani kwa Mh: Lowasa siku ya
tarehe 22-03-2015 haizidi watu 230 wakiwemo Wamachinga na Wenyeviti wa
Jumuiya za wazazi, kama vyombo vya habari vilivyoripoti. Ukiwatoa
Wamachinga na Wenyeviti wa Jumuiya za wazazi waliotoka mikoa
mbalimbali,idadi ya wanafunzi waliokuwepo kwenye tukio lile hawazidi
150.Idadi hii ni sawa na asilimia 0.4 ya wanafunzi wote wanaosoma vyuo
vikuu vya Dodoma.
Ndugu wanahabari,kwa akili ya
kawaida kabisa asilimia 0.4 ya wanafunzi wa vyuo vikuu ndio waliokuwa
pale.Tunashangazwa na dhambi tusiyoitenda tunayobebeshwa wanafunzi wa
vyuo vikuu vya Dodoma ambao kwa sasa tupo bize na msimu mpya ya masomo
wenye changamoto mbalimbali.
Ndugu wanahabari,sisi kama
vijana wasomi na watu tunaotegemewa na jamii zetu tutakusanyika katika
kujadili na kuchambua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii yetu na
sio kukusanyika kwa ajili ya mwanasiasa ambaye sifa zake na uhadilifu
wake unatiliwa shaka katika jamii.Tunaomba mlijulishe Taifa, kuwa
wanafunzi wa vyuo vikuu vya Dodoma hatujahusika na tukio lile isipokuwa
wanafunzi wachache walitumika kwa kupewa pesa na wahusika wa tukio lile.
Tunataka Taifa lijue hatupo
tayari kutumia elimu zetu kulitia upofu taifa letu.Waambieni mama zetu
na baba zetu huku vijijini kwetu kuwa tumekuja kutafuta elimu ili
ituwezeshe kuwakomboa wao na sio kutumika na Wanasiasa kwa malengo
yao.Tunatambua haki ya mwanafunzi kuamua na kufanya shughuli za kisiasa
nje ya maeneo ya vyuo, lakini hatukubaliani na wanafunzi wachache
kuchafua na kuwapaka matope maelfu ya wanafunzi wa vyuo vikuu vya Dodoma
ambao hawajahusika na tukio lile.Hii sio haki na haikubaliki.
Vilevile tungependa kutumia
fursa hii kuwaasa wanafunzi wenzetu popote pale nchini, makundi
mbalimbali ya kijamii (wakulima, wafugaji, wavuvi, wamachinga, wasanii,
n.k), zikiwemo taasisi za dini kwamba watu wachache kuzungumza kwa niaba
ya makundi juu ya mambo yanayogusa maamuzi ya mtu binafsi.
Mwisho tunatoa wito kwa
wanafunzi wenzetu wote kujitambua na kutumie muda wetu kwa mambo ya
msingi na muhimu kwa ustawi wa Nchi yetu. Na kuonesha jinsi wanafunzi wa
Vyuo Vikuu vya Dodoma walivyokasilishwa na jambo hili, Tamko hili
limesainiwa na wanafunzi 7821 toka vyuo mbali mbali vya Dodoma.Majina ya
sahihi za wanafunzi zimeambatanishwa. Tusikubali kutumika na wanasiasa
wa aina hii..
Asanteni
Mungu ibariki Tanzania,Mungu vibariki vyuo vikuu vya Dodoma.
Kwa niaba ya wawakilishi wa
serikali za Wanafunzi Chuo cha Mipango,Chuo cha Madini, Chuo cha
Hombolo,Chuo kikuu cha Dodoma(UDOM) na CBE.
DANIEL DANIEL -Rais wa Saint Jonh’s University
26/03/2015

