
Mtendaji
Mkuu wa Ofisi ya Rais-Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Miradi (PDB)
inayosimamia utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), Omari
Issa amewashauri Wakuu wa Nchi za Ukanda wa Kati wa Uchukuzi kuwa
mifumo ya ufuatiliaji na utekelezaji itakayoharakisha ukamilishaji wa
miradi iliyoko katika nchi zao.
Alisisitiza
kuwa bila kuwa na mifumo ya ufuatiliaji, baadhi ya nchi zinaweza
kumaliza kwa wakati miradi yake; huku nchi nyingine zikichelewa
kukamilisha miradi iliyo upande wake. Hali hii inaweza kuzivunja moyo
nchi ambazo zitakuwa zimekamilisha miradi yake, hasa ikizingatiwa kwamba
miradi yote ya Uchukuzi ya Nchi za Ukanda wa Kati inategemeana.
Akizungumza
jijini Dar es Salaam jana wakati wa Majadiliano ya Wakuu wa Nchi za
Mpango wa Uharakishaji wa Ujenzi wa Miundombinu katika Ukanda wa Kati,
Bw. Issa alisema Tanzania imetekeleza miradi mbalimbali katika mwaka wa
kwanza wa BRN kuliko ilivyotarajiwa kwa kutumia bajeti kidogo kutokana
na nidhamu ya utekelezaji chini ya mfumo huo wa BRN, unaosisitizia
katika kuweka vipaumbele, ufuatiliaji madhubuti na utatuzi wa
changamoto. Nidhamu hiyo imesaidia kutatua changamoto zilizokuwa na
zinazooendelea kujitokeza; na kuifanya Tanzania iweze kutekeleza kwa
ufanisi miradi yake ya kipaumbele ikiwemo ile iliyo katika sekta ya
uchukuzi.
Aidha,
Bw. Issa alisema kuwa utekelezaji wa Miradi ya Uchukuzi ya Ukanda wa
Kati nchini Tanzania unaofanyika chini ya uangalizi wa BRN, umeleta
mafanikio makubwa. Hii inajumuisha kuongeza ufanisi katika Bandari ya
Dar es Salaam, kuhuisha usafiri wa reli ya kati, barabara na miradi ya
umeme katika maeneo ya ukanda huo wa kati.
Viongozi
mbalimbali wa Serikali kutoka nchi za Ukanda huo walionesha nia ya
kuuchukua mfumo wa utekelezaji wa BRN katika sekta zao za uchukuzi ili
kusaidia kuharakisha utekelezaji wa miradi iliyo katika nchi zao.
Mpango
wa Kuharakisha Utekelezaji wa Ujenzi wa Miundombinu katika Ukanda wa
Kati ulizinduliwa Januari, 2014, kwa lengo la kuhakikisha ujenzi wa
reli, barabara, kuboresha usafiri wa majini na anga ili kuiunganisha Dar
es Salaam na nchi zisizofikika kwa bahari za Uganda, Burundi, Rwanda na
Jamhuri ya Kidemorasi ya Congo (DRC).
Wakati
miradi ya miundombinu ikiharakishwa nchini Tanzania, Serikali pia
imeanza kuchukua hatua madhubuti za mageuzi katika sekta ya uboreshaji
wa mazingira ya biashara ili kuvutia uwekezaji zaidi na hali bora ya
uendeshaji wa biashara nchini. Sekta Sita za Kitaifa za Kipaumbele
(NKRAs) ziliingizwa katika mfumo wa BRN kwa nia ya kuboresha mazingira
ya biashara; ambazo ni:- Kuoanisha Taratibu na Taasisi; Upatikanaji wa
Ardhi na Umiliki; Kodi: Kuoanisha Tozo, Ada na Makato; Kupambana na
Rushwa, Sheria za Kazi na Ujuzi; Utekelezaji wa Mikataba, Sheria na
Usalama.

