RAIS Jakaya Kikwete amefafanua msimamo wa Serikali katika mjadala unaoendelea wa Mahakama ya Kadhi, na kuweka wazi kuwa Serikali haina mpango wa kuianzisha, wala kuiendesha.
Mbali
na hiyo, Rais Kikwete ambaye jana alizungumza na Kamati ya Amani ya
Viongozi wa Dini mkoani Dar es Salaam, pia alielezea kusikitishwa kwake
na tamko la Jukwaa la Wakristo Tanzania, lililowaelekeza waumini wao
kupigia Katiba Inayopendekezwa kura ya Hapana.
Mahakama ya Kadhi
Akifafanua suala la Mahakama ya Kadhi, Rais Kikwete alisema Serikali ina msimamo wa mambo mawili katika mahakama hiyo.
Kwanza,
alisema Serikali haina mpango wa kuianzisha na kuiweka katika Katiba na
pili, haihusiki kuiendesha na badala yake, Waislamu wenyewe ndio
watakaoiendesha.
Alisema kimsingi, mahakama hiyo ilikuwepo kabla ya Uhuru na kinachotakiwa kuzungumzwa ndani ya Bunge, ni Sheria ya Kutambua Uamuzi Unaofanywa na Kadhi.
Alifafanua
zaidi kuwa Mahakama hiyo ya Kadhi, haihusiki na mambo ya jinai,
isipokuwa mambo ya kijamii ikiwemo talaka, mirathi na mengine ya aina
hiyo.
Alitoa
mfano wa Sheria ya Kiislamu, iliyokuwepo tangu zamani, ambayo inatambua
chombo hicho na kusisitiza kuwa kinazungumzwa, ni uamuzi unaofanywa na
Kadhi utambulike tu.
Katika
mfano huo, alisema Muislamu ukigombana na mke wake, kuna mabaraza ya
usuluhishi ambayo huyo mwanamke atapaswa kwenda, ila wakishindwa na
ataomba talaka ambayo inaidhinishwa na Kadhi, ambaye ndiye msajili wa
vyeti vya ndoa kwa Waislmau.
Baada
ya kutoa ufafanuzi huo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Shehe Alhad Musa,
alimshukuru Rais Kikwete kwa ufafanuzi alioutoa na kusema Wakristo na
Waislamu siku zote ni wamoja na wataendelea kuishi kwa amani, furaha na
ushirikiano.
Katika
hilo, Shehe Alhad alinukuu Biblia katika Kitabu cha Mathayo tano,
mstari wa 25, ambao unasema; “Patana na mshitaki wako, mngali njiani,
asije akakupeleka kwa Kadhi na Kadhi akakukabidhi kwa Polisi na Polisi
akakutupa korokoroni.”
Katiba Pendekezwa
Akizungumzia
Katiba Inayopendekezwa, ambayo inasubiri kupigiwa kura na wananchi,
Rais Kikwete alisema Katiba hiyo imewakilisha vitu vingi kuliko Katiba
iliyopo.
Alifafanua
kwamba Katiba Inayopendekezwa, imeweka haki za makundi mbalimbali ya
jamii, kuliko iliyopo na kuongeza kuwa yeye binafsi ameisoma na kurudia
kuisoma, lakini hajaona mahali popote ambapo ina kasoro.
Alisema
isingekuwa rahisi kuweka maoni ya kila mtu katika Katiba, na kufafanua
kuwa yale ambayo hayajawekwa sasa hivi, utafika wakati wake na
yatawekwa.
Alibainisha
kuwa haikuwa rahisi kwa maoni ya kila mtu kuingia katika Katiba
Inayopendekezwa, kwani hata CCM ilikuwa na mambo 60 waliyopendekeza,
lakini kati ya hayo ni 12 tu yaliyoingia.
Rais
Kikwete alisema Katiba sio Msahafu au Kurani, ambayo haiwezekani
kubadilishwa hata nukta. Alitoa mfano wa Zanzibar, kwamba wakati kuunda
Muungano, yapo mambo yalionekana ni muhimu kubakia katika Muungano,
lakini kadri muda ulivyokwenda yameondoka.
Jukwaa la Wakristo
Akizungumzia
tamko la Jukwaa la Wakristo Tanzania, Rais Kikwete alisema
amehuzunishwa na kufadhaishwa na tamko hilo la viongozi wa dini la
kutaka waumini wao wajiandikishe kwa wingi, lakini wapige kura ya Hapana
kwa Katiba Inayopendekezwa.
Tamko
hilo lilitolewa na jukwaa hilo linaloundwa na Jumuiya ya Kikristo
Tanzania (CCT), Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Baraza la
Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT).
Rais
Kikwete alisema, tamko hilo litakuwa pia limekwaza waumini, kwa
kuwawekea mipaka ya kidemokrasia na kukwaza hata viongozi wenyewe.
Alitoa
mfano kwamba kwa tamko hilo, muumini hataweza kusimama na kumwambia
kiongozi wa dini asiwaingilie katika uamuzi, kwa kuwa kupiga kura ni
haki ya kikatiba ya kila mtu, na ikitokea hivyo, hata kiongozi husika
atakwazika.
Subira kwa NEC
Kuhusu
uwezekano wa Kura ya Maoni kufanyika Aprili 30 kama ilivyotangazwa na
Serikali, huku kazi ya kuandikisha wapigakura ikiendelea kusuasua, Rais
Kikwete alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), inayoratibu
uandikishaji wa wapigakura, itazungumza kuhusu walipofikia wakati
muafaka ukifika.
Amani
Kuhusu amani ya nchi, Rais Kikwete alisema viongozi wa dini pia wa jukumu kubwa la kuimarisha amani ya nchi.
Katika
utekelezaji wa jukumu hilo, Rais Kikwete aliwataka viongozi hao
wajaribu kuepuka kutumiwa na watu wenye nia mbaya, kwa sababu wanafahamu
kuwa viongozi wa dini wana ushawishi katika jamii na wana watu wengi
nyuma yao.
Alisema
machafuko yatakayotokana na mvurugano wa kidini, hakuna mtu atakayeweza
kuyazuia, hivyo ni vyema viongozi hao waendeleze mshikamano.