Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa “Green house” ya Bopwe Wete, ikiwa ni miongoni mwa Green House 10 za Jimbo la Gando.
Na: Hassan Hamad, OMKR
Makamu wa
Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amewataka
wakulima kuongeza juhudi katika kilimo cha kisasa ili waweze kuongeza
kipato chao.
Akizindua
mradi wa kilimo cha mbogamboga kinachotumia teknolojia ya kisasa “green
house” huko Bopwe jimbo la Gando, Maalim Seif amesema iwapo wakulima
watatumia vyema elimu wanayopewa na wataalamu wa kilimo hicho, wanaweza
kuongeza tija na kupata mafanikio kwa kipindi kifupi.
Kilimo
hicho cha kisasa kimo katika mpango wa wajasiriamali wa jimbo la Gando
(GEP), unaowahusisha wajasiriamali wapatao mia tisa wa Jimbo hilo.
Ameuhimiza
uongozi wa Jumuiya hiyo kukuza mashirikiano na wadau wanaowaunga mkono,
ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati ya kurejesha madeni wanayokopa.
Maalim
Seif ambaye ni mlezi wa Jumuiya hiyo ya wajasiriamali jimbo la Gando,
amewashukuru wadau wa mradi huo wakiwemo benki ya CRDB, na kuahidi kuwa
Serikali itatoa ushirikiano unaohitajika ili kuhakikisha kuwa malengo ya
jumuiya hiyo yanafanikiwa.
Mapema
akisoma risala ya wajasirimali hao, Bw. Salim Said Khalfan amesema mradi
huo unaojumuisha vikundi 53 vya wajasiriamali wa jimbo la Gando,
umepata mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwake.
Hata
hivyo amesema bado wanakabiliwa na changamoto kadhaa zinazohitaji
kupatiwa ufumbuzi ikiwa ni pamoja na mtaji mdogo wa kuendeshea mradi huo
pamoja na vitendea kazi vya kisasa.
Akitoa
taarifa ya kitaalamu kuhusu kilimo hicho cha kisasa cha mboga mboga,
Mkurugenzi wa kampuni ya Affordable Green House ya nchini Kenya bw.
Timothy Nyuguna kutoka nchini Kenya, amesema kilimo hicho kinaweza kuleta tija kubwa iwapo masharti yaliyowekwa yatazingatiwa.

