Naibu
Inspekta Jenerali wa Polisi, Abdulrahmani Kaniki akisalimiana na baadhi
ya Wakufunzi wa chuo cha Polisi Moshi (CCP) wakati alipokuwa katika
ziara ya kikazi kukagua mafunzo yanayoendelea chuoni hapo.Kushoto ni
Mkuu wa Chuo hicho, Kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi (SACP)
Matanga Mbushi.
(Picha na Frank Geofray wa Jeshi la Polisi)
Naibu
Inspekta Jenerali wa Polisi, Abdulrahmani Kaniki (kushoto) akiwasili
katika chuo cha Polisi Moshi (CCP) wakati alipokuwa katika ziara ya
kikazi kukagua mafunzo yanayoendelea chuoni hapo.Katikati ni Mkuu wa
Chuo hicho, Kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi (SACP) Matanga Mbushi
na Mkuu wa Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Naibu Kamishna Omar Rashid.
Na Frank Geofray-Jeshi la Polisi, Moshi.
Wakufunzi
wa Chuo cha Polisi Moshi (CCP) wametakiwa kuendelea kutoa mafunzo kwa
weledi ili kuweza kupata askari bora ambao watashirikiana na jamii
katika kupambana na uhalifu hasa katika kipindi hiki ambapo kumeibuka
uhalifu mpya kwa njia ya mitandao na unaovuka mipaka.
Wito
huo umetolewa jana mjini moshi na Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi,
Abdulrahman Kaniki wakati alipokuwa katika ziara ya kikazi chuoni hapo
ambapo alizungumza na wakufunzi hao na kuweka mikakati mbalilmbali ya
kuboresha mafunzo katika chuo hicho.
Naibu
IGP Kaniki alisema, askari wakipata mafunzo bora wataongeza mbinu
zitakazowezesha kukabiliana na uhalifu huo na hivyo kuendelea
kuimarisha usalama wa raia na mali zao kwa kushirikiana na jamii ambayo
imekuwa msaada mkubwa wa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu.
“Ili
kuhakikisha kwamba raia wa Tanzania na mali zao wanalindwa ipasavyo,
Jeshi la Polisi hatuna budi kuendelea kubuni mbinu mpya za kukabiliana
na uhalifu wa kila aina unaobadilika mara kwa mara na hilo linawezekana
kwa kuendelea kuwapatia askari wetu mafunzo yenye viwango vya kupambana
na uhalifu unaokua kwa kasi”alisema Kaniki.
Kwa
upande wake Mkuu wa Chuo cha Polisi moshi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi
wa Polisi (SACP) Matanga Mbushi alisema wanaendelea na juhudi za
kuhakikisha kuwa mafunzo wanayotoa yanalenga katika mitaala ambayo
wamekuwa wakiiboresha mara kwa mara ili kuendana na wakati kulingana na
mazingira ya uhalifu unaotokea katika jamii.
Alisema,
mbinu za uhalifu zimekuwa zikibadilika kila siku hivyo, na wao kama
chuo wamejikita kuhakikisha kuwa askari wanaopita katika chuo hicho
wanazipata mbinu mpya na hivyo kuwa zaidi ya wahalifu ili waweze
kupambana nao.

