Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imetoa siku saba kwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paulo Makonda, kuwasilisha utetezi wake dhidi ya kesi ya madai iliyofunguliwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM, Dar es Salaam, John Guninita.
Guninita
na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Mgana Msindai wamefungua kesi
hiyo, wakiiomba Mahakama imwamuru Makonda awaombe msamaha na kuwalipa
kila mmoja Sh milioni 100.
Kesi
hiyo ilitajwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Hellen Riwa ambapo Wakili wa
Makonda, Lusiu Peter aliomba aongezewe muda ili awasilishe utetezi wao.
Akiwasilisha
ombi hilo, wakili Lusiu alidai kuwa amepokea madai hayo Machi 27 mwaka
huu na walitakiwa kuwasilisha utetezi wao leo lakini aliomba waongezewe
muda ili wawasilishe.
Hakimu
Riwa alikubali ombi hilo na kuwataka wawasilishe utetezi wao ndani ya
siku saba, ambayo itakuwa Aprili 23. Kesi hiyo itatajwa tena Aprili 27
mwaka huu.
Kwa
mujibu wa Kesi hiyo Namba 68 ya 2015, Msindai na Guninita wanadai fidia
ya fedha hizo, kutokana na maneno ya kuwadhalilisha aliyoyatoa Makonda
katika mkutano na waandishi wa habari wakati akiwa Katibu Uhamasishaji
Chipukizi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).
Wanaiomba
Mahakama itoe zuio la kudumu kwa Makonda kuzungumza tena maneno ya
kashfa wala kuyasambaza kama alivyofanya awali pia alipe riba pamoja na
gharama za kesi na nafuu nyingine.
Wanadai
maneno aliyoyatoa Makonda kuwa “Msindai na Guninita ni vibaraka
wanaotumiwa kuharibu CCM kwa nguvu ya pesa”, yamewadhalilisha na
kuwafanya waonekane ni viongozi ambao hawafai kuongoza CCM.
Katika
hati hiyo, wanadai Makonda alipelekewa barua iliyomtaka kuomba msamaha,
lakini alisema hataomba msamaha kwa kuwa aliyatamka kwa nafasi yake
katika Chama na kwa mujibu wa Katiba, Mwongozo na Kanuni za Chama.