Dereva wa bajaji, Alphonce Maurus, aliyebeba watu wanaodhaniwa kuwa watuhumiwa wa ugaidi, Kidatu wilayani Kilombero, ameweka hadharani namna alivyomfahamu mmoja wao.
Amesema
mtuhumiwa ambaye aliuawa na wananchi baada ya kumjeruhi polisi, Hamad
Makwendo, alijihusisha na mchezo wa kareti na masuala ya dini ya
Kiislamu.
Dereva
huyo huyo aliwaeleza waandishi wa habari waliofuatilia taarifa za kina
za tukio hilo jana kwamba Makwendo alikuwa hana kazi maalumu ya
kumwingizia kipato.
Maurus
alitoa taarifa hizo katika kata ya Chikago, Kidatu wilayani Kilombero
ambapo watu 11 walikamatwa na polisi msikitini wakiwa na silaha,
milipuko na sare za jeshi.
Alisema
siku ya tukio, saa tatu usiku, akiwa katika eneo lake la kufanyia
kazi, walitokea watu 11 ambapo watano pamoja na mwenyeji ambaye ni
marehemu, walipanda katika bajaji yake na wengine sita walipanda katika
bajaji ya mwenzie.
Alisema
watu hao walitaka kufikishwa katika msikiti wa Suni na kwamba wakati
wote wa safari, mwenyeji wao ndiye alikuwa akizungumza lugha ya
Kiswahili huku wenzake wakisikiliza bila kujibu kitu.
‘’Tuliwafikisha
hadi eneo walilotaka na kisha tuligeuza na yule mwenyeji wao, ambapo
tulipofika manyasini tulisimamishwa na polisi wakitaka kujua tumetoka
wapi na tunakwenda wapi.
“Yule mwenyeji alishuka na kuanza kukimbia jambo lililofanya askari kuanza kumkimbiza huku na sisi tukifuatilia nyuma,’’ alisema.
Alisema
Makwendo alipofika mbele alimkata polisi mmoja na jambia na ndipo
polisi walifanikiwa kumpiga risasi na wakamchukua na walimchukua na
kumpandisha katika gari lao.
Maurus
alisema wananchi walifika katika eneo hilo na kuzingira gari hilo na
kumshusha mtu huyo huku wakitishia kuchoma moto gari la polisi.
Akizungumzia
mwonekano wa watu hao, dereva huyo alisema walivalia mavazi ya jamii ya
Kihindi, maarufu kama Punjabi, huku umri wao ukionekana kati ya miaka
20 na 25 tofauti na mwenyeji wao alieyonekana na umri wa takribani zaidi
ya miaka 30.
Kwa
upande wake, askari aliyejeruhiwa, Koplo Nasoro Dabi, ambaye amelazwa
katika zahanati ya Polisi Mkoa wa Morogoro, alisema siku ya tukio, akiwa
na askari wenzake walisimamisha bajaji aliyopanda Makwendo.
Alisema
baada ya bajaji hiyo kusimama, mtuhumiwa huyo alikimbia, hali
iliyoashiria kuwa ni mhalifu hivyo kuwalazimu askari watatu, akiwemo
yeye kumfukuza.
‘’Wakati
tukimkimbiza, nilikuwa mbele na kwamba tulipofika katika giza alichomoa
jambia na kunishambulia. Askari wenzangu waliokuwa nyuma yangu
walifyatua risasi na zingine kupiga juu hali iliyosababisha wananchi
wengi kujitokeza kumpiga na kumchoma moto,’’ alisema.
Alisema
wakati tukio hilo likiendelea askari wengine walifanya mawasiliano na
Mkuu wa Kituo cha Ruhembe kwa ajili ya kuwaongezea nguvu.
Naye Mganga Mkuu Zahanati ya Polisi Morogoro, Mrakibu Thomas Kawala, alisema walimpokea askari huyo anaendelea na matibabu.
Kawala alisema askari huyo alifika zahanati hapo akiwa na maumivu makali lakini kwa sasa anaendelea vyema na matibabu.
Mmoja
wa Kiongozi wa Msikiti wa Masjid Salah Al – Fajih , Mohamed Manze,
alisema wakiwa viongozi na waumini, hawakuwa na taarifa zozote za ujio
wa watuhumiwa hao na kwamba katika msikiti huo wako vijana wanne ambao
huwa wanalala na kujisomea hapo.
Alisema
siku ya tukio watuhumiwa hao walifika msikitini hapo saa nne ambapo
ibada ya mwisho ilikwishafanyika na waumini kutawanyika, ambapo walikuwa
wamebakia vijana hao peke yao.
Manze
alisema walitumia mwanya huo kuingia na kujihifadhi bila taarifa
zozote kwa uongozi wa msikiti, jambo ambalo ni kinyume cha utaratibu za
msikiti huo.
Hata
hivyo, alisema wakiwa waumini wa msikiti huo, hawakupendezwa na suala
hilo kwa kuwa limewachafua na kuwaharibia sifa na kwamba Makwendo hakuwa
muumini wao.
Alisema
hawana nasaba na kikundi chochote kinachojihusisha na uhalifu na
kwamba wanalaani vibaya watu wanaotumia dini katika masuala hayo ya
uhalifu.