KIKOSI
cha Simba SC baada ya mazoezi ya leo jioni uwanja wa CCM Kambarage,
Shinyanga, kimetembelea kituo Jumuishi cha Walemavu kilichopo mjini
Shinyanga.
Katika kituo hicho chenye watoto zaidi ya 300 kinajumuisha walemavu wa ngozi, Albino, viziwi na walemavu wa macho.
Katika ziara hiyo ya kwanza kihistoria katika kituo hicho, mkuu wa
idara ya habari na mawasiliano ya Simba, Hajji Manara ambaye pia ni
mlemavu wa ngozi ‘Albino’ amesema wameamua kufanya jambo hilo kwasababu
Simba inapinga vikali mauaji ya Albino yanayoendelea nchini.
Wakati akiendelea kuongea, ghafla Hajji alishikwa na uchungu na kuanza kumwaga machozi,
kitendo kilichosababisha mwalimu mkuu wa kituo hicho Peter Ajali aendelee na utaratibu mwingine.
Naye kocha mkuu wa Simba, Gorani Kopunovic alisema ni jambo la furaha kuangana na ‘Albino’ hawa na wanapinga vikali kuuawa kwao.
“Ni siku kubwa kwangu, kwa wachezaji wangu na timu yangu. Msemaji wa
klabu ni albino, ni rafiki yako mkubwa, nina furaha naye mno”. Alisema
Kopunovic.
Katika ziara hiyo, Simba wametoa zawadi ya vinywaji na kiasi cha fedha shilingi milioni 1.
Pia katika mechi yao ya kesho dhidi ya Kagera Sugar watawapa ofa ya
bure baadhi ya walemavu kutazama moja kwa moja ndani ya uwanja CCM
Kambarage.