CHACHA AKIELEZEA KUHUSIANA NA GAZETI LA DIMBA.... |
Uongozi wa Yanga ambao ni mabingwa wapya wa Tanzania
Bara umetangaza kufungua kesi ya madai dhidi ya gazeti la Dimba ukitaka kulipwa
fidia ya bilioni 3.
Yanga inataka kulipwa fedha hizo kufidia
usumbufu mkubwa ilioupata baada ya gazeti hilo katika toleo lake la leo Aprili
29 namba ISSN 0856-2698 lililoandika kichwa kikubwa cha habari “Manji kufuru
Yanga.”
Sehemu ya stori hiyo kubwa ilikuwa ikielezea
uamuzi wa Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji kutoa nyumba na magari kwa wachezaji
wake.
Mwanasheria wa Yanga, Frank Chacha amezikanusha
habari hizo na kusisitizi hakuna chochote kuhusiana na suala hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya Yanga jijini Dar es Saaam leo, Chacha
amesema gazeti hilo limekuwa likiwanukuu vibaya au kunukuu ambacho hajasema
viongozi wa klabu hiyo.
“Mara kadhaa, hali hii imekuwa ikitokea.
Magazeti kadhaa ya nyuma pia yamefanya hivyo (alisema huku akionyesha baadhi ya
magazeti ya Dimba).
“Hatuoni kama hili ni sahihi, hivyo pia
tunawazuia Dimba kuandika habari zetu hadi hapo watakapoanza kuziandika kwa
usafaha,” alisisitiza Chacha.
Hata hivyo, alisisitiza Yanga wanahitaji ushirikiano kutoka kwa vyombo vya habari huku akiamini kilichofanywa na Dimba hakikuwa sahihi na kinalenga kuvuruga umoja wa Yanga na Wanayanga kwa ujumla.