Chile
imetoa kipondo cha mbwa mwizi kwa Bolivia baada ya kuichakaza kwa jumla
ya bao 5-0 ikiwa ni mchezo wa kundi A kwenye michuano ya kombe la
Mataifa ya bara la America
Kusini almaarufu kama Copa America mchezo
uliomalizika alfajiri ya leo huko nchini Chile.
Charles Aranguiz alianza kuipatia
Chile bao la mapema ikiwa ni dakika ya tatu tangu mchezo huo kuanza
kabla ya winga wa Arsenal Alexis Sanchez kufunga goli la pili dakika ya
37 na kuifanya Chile iende mapumziko ikiwa mbele kwa goli 2-0 dhidi ya
Bolivia.
Kipindi
cha pili kilikuwa kibaya zaidi kwa Bolivia kutokana na Chile kulisakama
lango lao kwa muda mwingi wa mchezo hali iliyopelekea wafanye makosa
mengi kwenye safu yao ya ulinzi na kutoa mianya kwa Chile kufunga mabao.
Aranguiz alipachika pao la tatu
kwa Chile dakika ya 66 lakini likiwa ni bao lake la pili kwenye mchezo
huo, kabla Gary Medel hajatupia nyavuni goli la nne dakika ya 80. Zikiwa
zimebaki dakika nne ili mwamuzi amalize pambano hilo, Raldes wa Bolivia
alijifunga na kuufanya mchezao huo kumalizika kwa wenyeji wa mashindano
(Chile) kuibuka na ushindi mnono wa goli 5-0.
Aturo Vidal alikuwepo kwenye
kikosi kilichoifanyia mauaji Bolivia akitokea kwenye sekeseke la ajali
ambayo aliipata kutokana na kuendesha gari kwa spidi kali huku akiwa
amelewa. Lakini tofauti na matarajio ya wengi, Vidal bado alipata sapoti
kubwa kutoka kwa mashabiki wa Chile ambao wamefurahia pia timu yao
kusonga mbele kwa hatua ya robo fainali kwenye michuanon hiyo.
Kwenye
mchezo wa awali uliozikutanisha Mexico dhidi ya Ecuador kwenye mchezo
wa kundi A, timu ya Mexico imetupwa nje ya mashindano ya Copa America
baada ya kukubali kichapo cha goli 2-1 kutoka kwa Ecuador kwenye mechi
ya mwisho ya timu za kundi A.
Miller Bolanos alianza kuipatia
Ecuador bao la kuongoza dakika ya 26 kabla ya mshambuliaji wa West Ham
Enner Valencia kuongeza goli la pili dakika ya 57 kwa upande wa Ecuador.
Mexico walipata goli lao la kufutia machozi dakika ya 64 kwa mkwaju wa
penati uliowekwa kambani na Raul Jimenez.