Dodoma. Kumekucha na Hapatoshi mjini Dodoma. Hivyo ndivyo unavyoweza kuelezea hali ilivyo mjini hapa, wiki mbili kabla ya vikao vya juu vya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuanza kazi ya kumtafuta mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Hekaheka za maandalizi ya vikao hivyo kuanzia vya maadili, Sekretarieti, Kamati Kuu, Halmashauri Kuu ya Taifa na Mkutano Mkuu wa Taifa, zimeanza kuonekana wazi huku nyumba zote za kulala wageni na hoteli zikiwa zimekwishajaa kwa muda wote wa vikao hivyo.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi kwenye maeneo ya katikati ya mji wa Dodoma, umebaini kuwa nyumba za kulala wageni na hoteli zimejaa kuanzia Julai 8 hadi 12, mwaka huu.
Hali hiyo imewafanya watu wanaotaka kupanga katika nyumba hizo kuulizwa wataondoka lini, ili tarehe za ‘booking’ zisigongane.
“Utaondoka lini, maana CCM wamechukua nyumba zote hapa kati ya Julai 8 hadi 12,” alisema mmoja wa wahudumu katika nyumba ya kulala wageni ya Kiramiya.
Chanzo cha habari kutoka katika ofisi ya CCM, kimesema wajumbe wote 2,448 wa mkutano mkuu wamepata maeneo ya kulala kwa siku watakazokuwa mjini hapa.
Hata hivyo, chanzo hicho kimedokeza kuwa changamoto imekuwa katika kupata malazi ya wageni 600 waalikwa, watakaokuja kuhudhuria mkutano mkuu huo utakaofanyika katika ukumbi mpya wa chama hicho.
“Katika maeneo mengi tuliyokwenda tulikuta hoteli zimechukuliwa na wapambe wa wagombea wa urais ambao tayari wamelipia siku watakazokaa mjini hapa,” alisema mmoja wa wanakamati ya maandalizi ya CCM na kuongeza:
“Hivi sasa wenzangu wako mtaani wanatafuta nyumba nyingine.”
Alisema hali imekuwa ngumu kutokana na wapambe wa wagombea ambao hadi sasa wamefikia 39 kuchukua vyumba vingi na kuvilipia kabisa, tofauti na CCM iliyopanga kuanza kulipia malazi hayo leo.
Ukarabati
Katika hatua nyingine, mafundi wameonekana wakifanya marekebisho katika majengo ya makao makuu ya chama hicho hasa jengo maarufu la ‘White House’ ulipo ukumbi wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho.
“Hujaingia humo ndani lakini ukumbi unafanyiwa marekebisho makubwa ili mjumbe atakayekaa mwisho aweze kuona mbele kwa urahisi, siyo kama ilivyokuwa zamani,” alisema mmoja wa makada wa chama hicho.
Nje ya ofisi hizo, wafanyabiashara wanaouza sare za chama hicho na bidhaa nyingine za kumbukumbu za chama, wamekwishaanza kupanga biashara zao kandokando ya ukuta wa jengo hilo wakisubiri kunufaika na wingi wa wageni mjini hapa.
Jumla ya wagombea 39 wamejitokeza hadi sasa kuomba nafasi ya kuipeperusha bendera ya CCM katika kiti cha urais, kwenye uchaguzi mkuu Oktoba 25 na wengi wao wanaendelea na kazi ya kukusanya wadhamini katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa hivi karibuni na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, Kamati ya Usalama na Maadili itafanya kikao chake Julai 8, mwaka huu kuangalia utaratibu wa kanuni kama haukuvunjwa.
Alisema kikao hicho kitafuatiwa na Kamati Kuu itakayofanyika Julai 9 ambayo inatarajiwa kuchuja wagombea hadi watano, kisha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) itakayofanyika Julai 10 ambayo itapunguza zaidi na kubakiza wagombea watatu watakaopigiwa kura na mkutano mkuu.
Mkutano Mkuu wa chama utafanyika Julai 11 na 12 na kumchagua mgombea atakayepeperusha bendera ya chama hicho.
Kwa upande wa mgombea urais wa Zanzibar, Nape alisema Kamati ya Usalama na Maadili ya Zanzibar, itafanya kikao chake Julai 4, ikifuatiwa na Kamati Maalumu Julai 5.