Wakati zoezi la usajili likizidi
kushika kasi huku kukiwa na taarifa kwamba klabu ya Simba inataka
kumsajili mshambuliaji wa zamani wa Azam FC Gaudence Mwaikimba, uongozi
wa klabu hiyo umekanusha taarifa za kutaka kumsajili mshambuliaji huyo
licha ya kuwa na uwezo mkubwa.
Afisa habari wa klabu ya Simba
Hajji Manara amesema, Gaudence Mwaikimba ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa
lakini hayupo kwenye mipango wala mahitaji ya klabu hiyo. Manara
aliongeza kuwa, Simba inafanya usajili kutokana na mapendekezo ya benchi
la ufundi na mahitaji kwa ajili ya msimumu husika.
“Simba inasajili kwa matakwa ya
benchi la ufundi kutokana na mapendekezo ya mwalimu aliyeondoka na
mahitaji ya ‘next season’, Gaudence Mwaikimba ni mchezaji mzuri lakini
hayupo kwenye mipango ya klabu ya Simba”, Manara amesema.
“Simba inataratibu zake, kwenye
mambo ya usajili mwenyekiti wa usajili huwa anazungumza. Rais wa klabu
ni msemaji mkuu wa klabu na mimi ndiyo msemaji wa klabu ya Simba, hakuna
mahali popote hilo jambo limewahi kusemwa wala kuhisiwa. Gaudence
Mwaikimba sijui nani wanataja kilasiku wachezaji wapya, hatujawahi hata
kuwafikiria, wachezaji wote tuliowahitaji kwa next season tumewasajili”,
ameeleza.
Alipoulizwa juu ya usajili wa
mkongwe Musa Hassan ‘Mgosi’ wakati wao sera yao ni kutumia wachezaji
vijana na chipukizi, Manara alisema “hebu tuwe ‘realistic’ mtu anatia
goli nane, tisa kwenye ligi na ku-assist halafu mnamwita mzee wakati
vijana hawa mnawasajili kwa milioni 30, 25 unakuta anagoli sita na
assist moja. Gaudence Mwaikimba hatumuhitaji ni mchezaji mzuri sana
lakini si kwa mahitaji ya klabu ya Simba”, Manara alifafanua.
“Hawa wachezaji mnaosema ni
vijana bure kabisa, Mgosi ni ‘legend’ wa klabu ya Simba amecheza kwa
zaidi ya miaka 10 na yupo kwenye kipindi chake cha mwisha kabisa cha
kumaliza soka, ni ‘culture’ ya klabu ya Simba kuwaenzi wachezaji
walioipa mafaniko klabu,” alimaliza Manara.
Wakati klabu ya Simba ikihusishwa
kutaka kumsajili Mwaikimba, tayari mkongwe huyo ameshasajiliwa na klabu
ya JKT Ruvu ya Mlandizi mkoani Pwani tangu juma lililopita na atakipiga
kwenye klabu hiyo ya maafande wa jeshi la kujenga Taifa kwa msimu ujao.