BAADA ya kutajwatajwa vipindi tofauti kuwa anashawishiwa kuingia katika siasa ili afikiriwe kumrithi
Rais Jakaya Kikwete anayemaliza muda wake wa uongozi Oktoba, hatimaye Jaji Augustino Ramadhani amechukua fomu za Chama Cha Mapinduzi (CCM). Wanaandika Waandishi Wetu … (endelea).
Jaji Ramadhani mwenye umri wa miaka 70 akiwa ni mzaliwa wa Kisimamajongoo, mjini Zanzibar, anakuwa mwanachama wa 36 kujitokeza kuchukua fomu za kusaka urais kupitia chama hicho kinachotafuta namna ya kukabiliana na ushindani mkubwa kutoka kwa kambi ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
UKAWA unaoundwa na vyama vya Chadema, Civic United Front (CUF), National League for Democracy (NLD) na NCCR-Mageuzi, haujateua mgombea wake, lakini utaratibu wa vyama hivyo kuteua wagombea unaendelea.
Kwa mujibu wa sheria, mgombea anayetaka wadhifa wa urais katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni shuruti awakilishe chama cha siasa. Jana gazeti hili lilielezwa na wenyeviti wa UKAWA kuwa wako imara na hawajatetereka licha ya kufahamu mbinu chafu za kutaka kuwasambaratisha.
Jaji Ramadhani ambaye alistaafu ujaji mkuu tarehe 27 Disemba 2010, amechukua fomu kwenye makao makuu ya CCM mjini Dodoma, huku akitoa ahadi kuwa yeye haogopi mtu kwa sababu ni mwanajeshi mahiri mstaafu.
Aliiambia hadhira mara baada ya kuchukua fomu kwamba anavyo vigezo vyote vya kushika wadhifa huo kikiwemo cha uzoefu wa uongozi kwa kuwa alitumikia jeshi kufikia ngazi ya Brigedia Jenerali.
“Chema chajiuza, kibaya chajitembeza. Nina sifa zote za kuongoza Tanzania,” alisema na kuwatambulisha watoto wake na ndugu wa familia yake akisema, “nimekuja nao hawa tu sitaki mbwembwe kama wengine wanavyofanya.”
Jaji Ramadhani ameahidi atakapokuwa rais, atakuwa kiongozi mtiifu kwa mamlaka kwa mujibu wa katiba ya nchi, na atatekeleza manifesto ya chama kilichompitisha kugombea.
Amesema yeye aliingia katika CCM mwaka 1969 wakati akiwa mwanafunzi wa shahada ya sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Alipomaliza alijiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania Zanzibar (JWTZ) ambako alitumikia mpaka alipostaafu akiwa na cheo cha brigedia jenerali.
Jaji Ramadhani aliwahi kuwa anatajwa kuwa amekuwa akishawishiwa kugombea urais mara tu baada ya kustaafu ujaji mkuu nchini, lakini ilisemekana alikataa hata aliposhikiliwa mara ya pili.
Amefichua siri kuwa alipotakiwa na Rais Kikwete kuongezewa muda wa mkataba wa kazi ya ujaji mkuu mwaka 2010, alikataa akisema hawezi kuvunja katiba ya nchi kwa kung’ang’ania nafasi hiyo kinyume na utaratibu uliowekwa.
Akiwa mwanasheria nguli aliyewahi pia kuwa jaji mkuu wa Zanzibar, kiongozi wa majaji waliomchunguza jaji wa Kenya aliyetuhumiwa kuvunja sheria, Jaji Ramadhani anasema atafuata sheria katika kuongoza na moja ya mambo atakayoyawekea mpango madhubuti kukoma ni mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino).
Jaji Ramadhani alikuwa ndiye makamu mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba akimsaidia Jaji mstaafu Joseph Warioba. Anasema kazi ile ni historia kwake kwa vile waliikamilisha na kukabidhi kwa rais kama sheria ilivyotaka.
Kuna malalamiko ya nguvu kwamba CCM imevuruga rasimu ya katiba mpya iliyoandaliwa na Tume ya Warioba. Mara nyingi amekuwa akikwepa kueleza hasa msimamo wake kuhusiana na hilo.
Kuingia kwake katika kinyang’anyiro cha kusaka urais, kumeongeza mvuto huku wachambuzi wakitoa maelezo yanayoonesha kuwa huyo ni tishio kwa makada waliotangulia kuchukua fomu.
Kabla ya ujio wake, tayari kulikuwa na majina makubwa yakiwemo ya Edward Lowassa, aliyejiuzulu uwaziri mkuu kwa kashfa ya mkataba tata wa kufua umeme, waziri mkuu mstaafu kabla yake, Frederick Sumaye na mawaziri 12 waliopata na wanaoendelea kutumikia serikali ya Rais Kikwete.
Lakini kwa upande mwingine kuingia kwa Jaji Ramadhani kunaelezewa kama kunakozidisha ushindani kwa sababu nje ya makundi mawili yanayoongozwa na Lowassa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bernard Membe, makada wanaoonekana kuwa na mvuto kwa nafasi hiyo ni Charles Makongoro Nyerere, Waziri Mkuu wa sasa, Mizengo Pinda, Mkurugenzi Mstaafu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Dk. Augustine Mahiga aliyemaliza kuwa Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa masuala ya Somalia.
CREDIT MWANAHALISI