Dar es Salaam. Mwanasiasa mkongwe na kada wa CCM, Kingunge Ngombare Mwiru (Pichani) amesema anahisi kuna mchezo mchafu unapangwa kwenye mchakato wa kupata mgombea wa urais wa chama hicho tawala, akitaja idadi kubwa ya waliojitokeza kuwa ni ishara mbaya.
Mwanasiasa huyo mkongwe aliyefanya kazi na marais
wa awamu zote nne, pia, bila kumtaja jina, alitumia muda mwingi kwenye
hotuba yake kujibu kauli ya makamu mwenyekiti wa CCM, Phillip Mangula
aliyekaririwa akisema kuwa mgombea wa chama hicho hatakiwi kujinadi.
Kingunge, ambaye amejitokeza hadharani kumpigia
debe Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa alionyesha hofu hiyo jana
wakati mbunge huyo wa Monduli alipokuwa akihitimisha kazi ya kusaka
wadhamini mkoani Dar es Salaam kwenye ofisi za CCM Mkwajuni wilayani
Kinondoni.
Hadi sasa, makada waliochukua fomu kuwania urais
kwa tiketi ya CCM ni 41 baada ya mwanachama mmoja kuchukua fomu jana
akisema atamudu kupata wadhamini kwa njia ya mtandao katika siku tano
zilizosalia. Akizungumza katika mkutano wa kusaka wadhamini ulioandaliwa
kwa ajili ya Lowassa wilayani Kinondoni jana, Kingunge alipingana na
kauli ya Mangula kuwa mgombea wa CCM atanadiwa na chama, si kujinadi
mwenyewe akisema chama hicho kinataka mgombea anayekubalika ndani na
nje.
Siku tatu zilizopita, Mangula alihojiwa na kituo
cha televisheni cha Shirika la Utangazaji Tanzania(TBC) na kusema
mgombea wa chama hicho hatakiwi kujinadi mwenyewe, kusisitiza kuwa
anatakiwa kunadiwa na chama.
Lakini Kingunge aliikosoa kauli hiyo jana akisema
chama hicho kimeweka utaratibu na hakuna sababu ya kuuacha na kuanza
kuwahukumu wagombea kabla ya vikao na kusisitiza kuwa CCM haikuwahi
kuwahukumu wagombea kabla katika chaguzi zilizopita.
“Mchakato ufuate taratibu zilizowekwa,” alisema
Kingunge ambaye aliibuka Kinondoni ambako Lowassa alimalizia shughuli
zake jijini Dar es Salaam.
“Nimemsikia kiongozi wetu mmoja tena juzi juzi
hapa, nikamuona kwenye televisheni anasema mtu hawezi kwenda kujinadi
yeye binafsi, ananadiwa na chama.
“Nikasema eh! hilo hilo. Lakini nataka nimweleze
yeye na wenye fikra kama hizo kuwa kuna ngazi mbili katika utaratibu
wetu; kwanza, mwanachama anayetaka kuwania ubunge, udiwani, urais lazima
ajinadi ndani ya chama, ndivyo tulivyofanya miaka yote kwa mujibu wa
katiba na taratibu zetu. Ndivyo wanavyofanya sasa wakina Lowassa.”
Alisema pili, wagombea wakishajinadi chama kitamteua mmoja ambaye kitamnadi na yeye ataendelea kujinadi.
“Si vizuri watu ambao tumewapa vyeo katika chama
wakaanza ama wakaendelea kukitumia chama chetu kwa mambo yao binafsi.
Kama wana mashaka tupo tunaojua mambo ya chama,” alisema Kingunge huku
akishangiliwa na mamia ya watu.
Kingunge alisema mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya
Kikwete akiwa Dodoma alisema chama kinatafuta mgombea anayekubalika
ndani na nje ya chama hicho ili kuweza kushindana na vyama vingine.
“CCM inamtafuta mtu ambaye anakubalika ndani na nje ya chama.
Wale wanaofanya jitihada za kuunda mazingira ya kukitafutia chama
kushindwa, wanataka historia iliyotukuka ya CCM iishe katika awamu ya
nne,” alisema.
”Tunapozungumzia suala la urais kwa sababu
linahusu watu, tusianze kukaa kwenye mizengwe. Kwanza tuwaulize watu
wanamtaka nani atayeweza kuwatatulia matatizo yao.”
Kingunge alisema idadi ya wagombea nafasi ya urais
waliojitokeza kwa tiketi ya CCM ni wengi na kwamba idadi hiyo ambayo
alisema haijapata kutokea katika historia ya chama, inaashiria kuwa kuna
jambo linataka kufanyika.
“Nasema hao wagombea wapo wengi, sasa wenye macho
wanaona watu wanasema nini. Matumaini yangu ni kwamba watu watatuliza
vichwa kukubali ukweli na kuachia utaratibu wetu uendelee unavyotakiwa,”
alisema.
Aliwataka viongozi ndani ya CCM kutokiuka taratibu
za chama hicho za kumteua mgombea, kuwataka kutumia utaratibu
uliozoeleka na ambao ulitumiwa katika chaguzi zilizopita.
Alisema Watanzania wana changamoto nyingi na
kwamba tangu mwanzo chama hicho kimekuwa kikilia na umasikini
unaolikabili taifa, huku akisisitiza kuwa mwarobaini wa kuondoa hali
hiyo ni Lowassa.
Kingunge alisema licha ya marais wa awamu zote kufanya mambo mengi, nchi kwa sasa inahitaji kiongozi atakaye ondoa umaskini.
“Na linawezekana hilo, nasema tunapozungumzia
suala zima la urais tunazungumzia hatma ya Watanzania. Tusifanye mchezo
nalo, hatuwezi kukaa tukasema yeyote tu anaweza. Hiyo sio lugha ya watu
makini. Kauli hiyo itasemwa na walionacho, lakini wasionacho hawawezi
kusema hivyo,” alisema Kingunge.
Kauli ya Lowassa
Akizungumza kwa nyakati tofauti akiwa wilayani
Ilala, Temeke na Kinondoni jijini Dar es Salaam, Lowassa alirejea kauli
iliyotolewa na Mwalimu Julius Nyerere ya mwaka 1995, kwamba watu
wanataka mabadiliko na wakiyakosa ndani ya CCM, watayatafuta nje ya
chama hicho.
“Mimi nitayaleta haya mabadiliko nikiwa ndani ya
CCM. Nagombea urais kwa sababu nauchukia umasikini na nitaunda serikali
ya kusaidia wanyonge, kuwafukuza machinga, mamantilie na waendesha
bodaboda ni upuuzi. Watu wanatafuta riziki tunawafukuza inatakiwa
tuwawekee mazingira mazuri,” alisema na kushangiliwa kwa nguvu.
Alisema anauchukia msongamano wa magari jijini Dar
es Salaam na iwapo atakuwa Rais atalimaliza tatizo la foleni katika
jijini Dar es Salaam kwa miezi sita.
“Kutakuwa na waziri anayeshughulika na jiji la Dar es Salaam tu
kama ilivyo kwa nchi jirani ya Kenya. Yeye akiamka tu akili yake yote ni
kushughulikia changamoto za jiji hili,” alisema Lowassa ambaye mara kwa
mara alikuwa akiwaimbisha wananchi wimbo wa ‘mchakamchaka’, huku
akisisitiza kuwa ataiongoza serikali yake kwa mtindo wa mchakamchaka
akisema ambaye hataweza atakaa pembeni.
Aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi
kujiandikisha katika Daftari la Wapigakura ili wapate fursa ya kumchagua
iwapo atapitishwa na chama hicho kugombea urais, huku akiwataka
wamuombee kwa maelezo kuwa Mungu ndiye anayepanga kila kitu.
“Mrema (Augustine) alikuwa maarufu sana mwaka 1995
mpaka gari lake likawa linasukumwa na wananchi, lakini katika kura za
urais hakushinda. Jiandikisheni ili tufanikishe safari ya matumaini,”
alisema.
Lowassa alisema kutokana na idadi kubwa ya
wananchi wanaomuunga mkono anaona kama tayari ameshashinda huku
akisisitiza kuwa ameshawafunga goli wagombea wenzake kama anavyofanya
mchezaji wa timu ya soka ya Real Madrid, Cristiano Ronaldo.
“Kati ya wagombea wote hakuna mwenye uzoefu ndani ya CCM kama mimi. Kumbukeni rais ndiye mwenyekiti wa CCM,” alisema.
Aiteka Dar
Lowassa aliwasili katika uwanja wa ndege wa zamani (Terminal 1), saa 2:00 asubuhi akitokea mkoani Arusha.
Mwenyekiti wa CCM wa Dar es Salaam, Ramadhani
Madabida alisema wanachama wa mkoa huo waliojitokeza kumdhamini ni
212,150, kati yao kutoka Kinondoni ni 95,251, Temeke (72,100) na Ilala
(44,799).
Afananishwa na mtume, Yesu
Akimkaribisha Lowassa Dar es Salaam, Madabida
alimfananisha waziri mkuu huyo wa zamani na Mtume Muhammad ambaye
alikuwa akitangaza dini lakini alikuwa akipingwa na watu wake wa karibu
na kufafanua kuwa kutokana na hali hiyo Mungu alimueleza kuwa hatamuacha
na atakuwa pamoja naye
Credit: mwananchi
0 comments:
Post a Comment