Kufuatia tetesi nyingi ambazo zimezidi kuongezeka miongoni mwa vyombo vya habari vya nchini Hispania na England kuhusu mustakabali wa muda mrefu wa beki wa Hispania Sergio Ramos uongozi wa klabu yake umeendelea kushikilia msimamo wake wa kutokuwekwa katika hali ya utata na beki huyo .
Uongozi wa rais Florentino Perez umesisitiza kuwa hautalazimika kutekeleza masharti ya beki huyo na badala yake atapaswa kuwa mtiifu kwa kuwa ana mkataba halali ambao lazima autumikie .
Sergio Ramos ameripotiwa kuwa karibu kuihama klabu hiyo baada ya kutoridhishwa na hali ya kutopewa ofa mpya wakati mkataba wake ukiwa umesaliwa na miaka miwili huku pia akihitaji kuongezewa mshahara .
Hadi sasa Ramos analipwa Euro Milioni 6 kwa mwaka na anahitaji ongezeko la mpaka kufikia euro milioni 10 kwa mwaka baada ya makato ya kodi jambo ambalo Madrid wamesisitiza kuwa hawatalitekeleza.
Ripoti nyingine nchini England zimedai kuwa Ramos ametajwa kuwa kwenye orodha ya usajili ndani ya klabu ya Manchester United ambayo inataka kumtumia katika usajili wa David De Gea ambaye anatakiwa na Real Madrid .
United imewaambia Real kuwa kama wanamtaka De Gea basi wawe tayari kumuachia Ramos katika dili lolote la usajili wa kipa huyo hali ambayo imezua hofu miongoni mwa mashabiki wa Real Madrid .
Katika misimu miwili iliyopita Real imewapoteza wachezaji wawili muhimu Angel Di Maria na Mesut Ozil ambao walikuwa wanadai nyongeza ya mshahara na matokeo yake walisajiliwa na timu za England .