Mbunge wa Mbeya Mjini kwa ‘leseni’ ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Joseph Osmund Mbilinyi ‘Sugu’ amemfikisha kortini aliyekuwa mkewe, Faiza Ally akitaka apewe mtoto wao, Shaa (2) ili amlee kwa vile mama yake huyo si mwadilifu.
Ijumaa iliyopita, saa 2:00 asubuhi, Faiza alipanda kwenye kizimba cha Mahakama ya Mwanzo, Manzese/ Sinza iliyopo Sinza-Makaburini jijini Dar kwa ajili ya kukabiliana na madai hayo.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, Mheshimiwa Sugu alifikia hatua hiyo baada ya kuchukizwa na tabia mbaya za mwanamke huyo hasa ya kuvaa nguo zinazomuacha nusu utupu na kupiga picha za aibu, akiamini kuwa, tabia hizo zinaweza kuathiri makuzi ya mtoto huyo.
Chanzo hicho kiliendelea kusema kuwa, kwa kipindi kirefu, Sugu amekuwa akimvumilia Faiza, lakini hivi karibuni uzalendo ulimshinda baada ya picha zake akiwa amevaa kigauni kifupi na makalio nje kusambaa mitandaoni.
Faiza alivaa kivazi hicho hivi karibuni kwenye hafla ya ugawaji wa Tuzo za Kili Music iliyofanyika Ukumbi wa Mlimani City, Dar.
Akizungumza mbele ya hakimu mfawidhi wa mahakama hiyo, Patrick Vaginga, Mheshimiwa Sugu alidai kuwa mbali na mzazi mwenzake huyo kuwa na tabia ya kuvaa nusu utupu pia ana mtindo wa kupiga picha zisizo na maadili na kuziweka mtandaoni yeye mwenyewe.
Sugu alikwenda mbele zaidi kwa kudai kwamba, pia mwanamke huyo amekuwa na tabia ya kumpiga picha mbaya mtoto wao na kuzimimina humohumo mitandaoni jambo ambalo alisema linamharibu mtoto huyo.
Mbali na sababu hizo, pia Sugu aliongeza kuwa, Faiza hana kipato kizuri cha kuweza kumlea mtoto na mara kwa mara amekuwa akisafiri jambo ambalo husababisha mtoto huyo kutopata malezi ya mama kwa muda mrefu hivyo kuiomba mahakama impe haki yeye ya kuishi na mwanaye.
Naye Faiza akijibu mapigo katika utetezi wake alisema kuwa, Sugu hafai kumlea mtoto huyo kwa sababu naye ana tabia ya kusafiri kwa muda mrefu hivyo kuishi mbali na mtoto ambapo aliiomba mahakama hiyo isimruhusu baba mzazi huyo kuishi na mtoto kwa kuwa atamharibu.
Mheshimiwa Hakimu Vaginga akasema kwa vile kesi hiyo ndiyo imeanza kusikilizwa kwa mara ya kwanza aliiahirisha hadi baadaye mwezi huu ambapo hukumu itatolewa.