Salum Mayanga
BENCHI la ufundi la timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars limekiri kuwepo kibarua kizito katika mechi ya kesho ya kuwania kucheza fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani, CHAN, dhidi ya timu ya Taifa ya Uganda, ‘The Cranes’.
Akizungumza jioni hii kwenye Ofsi za Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFA), Kocha msaidizi wa Stars, Salum Mayanga amesema Uganda inawazidi Tanzania kwa kiwango na ndio nchi yenye timu ngumu zaidi kwa ukanda wa Afrika Mashariki, lakini hakuna njia ya mkato zaidi ya kupambana nao kwa lengo la kufuzu fainali za CHAN zitakazofanyika Rwanda mwakani.
“Lazima tukubali, lazima tukiri kwamba kuna timu ambazo zipo ukanda mmoja na sisi kama Uganda zinatuzidi kiwango, wenzetu kiufundi wapo juu, lakini hatuna njia ya mkato zaidi ya kupambana nao ili tufikie kiwango cha juu.” Amesema Mayanga.
Kutokana na Shirikisho la soka Tanzania (TFF) kumpa kocha mkuu wa Stars, Mart Nooij mechi mbili za kushinda kuanzia ya kesho ili anusuru kibarua, Mayanga amesema kama benchi la ufundi hawana tatizo, hawafikirii hayo zaidi ya kuangalia namna ya kupata ushindi.
“Tunaangalia zaidi mchezo wa kesho, sisi kwetu hakuna matatizo kwasababu tunajua Watanzania wanataka matokeo”. Ameongeza Mayanga.
“Kesho jukumu letu kubwa ni kuhakikisha tunashinda na kurudisha imani kwa Watanzania ambao wamekata tamaa na timu yao. Taifa Stars ni timu ya Watanzania, tutakwenda kucheza popote pale, kikubwa ni kukidhi matakwa ya Watanzania, kesho tutacheza kwa nguvu, tutajituma, tutacheza kwa maarifa ili kuona tunashinda mchezo wa kesho, tunajua tuna kazi nzito kufuzu mashindano haya”.