Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania anaekipiga kwenye klabu ya TP Mazembe ya Congo DR, Mbwana Samatta amedhihirisha kwamba anataka kucheza soka barani Ulaya baada ya kuikataa ofa ya miamba ya soka la Afrika timu ya Zamalek ya Misri ambao walikuwa wakimtaka lakini nyota huyo amesema mtazamo wake kwa sasa ni kucheza soka Ulaya.
Meneja wa mchezaji huyo Jamal Kisongo amethibitisha kupokea ofa kutka klabu ya Zamalekh wakitaka kumsajili mchezaji wake Mbwana Samatta lakini wao hawako tayari kumwachia mchezaji huyo aendelee kucheza soka barani Afrika na badala yake wanataka akacheze barani Ulaya.
“Maombi hayo yalikuwepo lakini sisi tulikataa kwasababu tuliona ni vyema kama ataenda nje ya Afrika na yeye mwenyewe (Samatta) hakuwa tayari kwenda kucheza huko ingawa walikuwa wamefika pesa nzuri tu kutaka kuwalipa Mazembe”, amesema Kisongo.
“Kuna timu nyingi sana za Ulaya zinazomtaka lakini Katumbi hataki aondoke mpaka amalize michuano ya vilabu bingwa imalizike, sisi tunasubiri michuano hiyo imalizike na baadae anaweza kuondoka kama mchezaji huru maana mkataba wake unaelekea ukingoni”, ameongeza.
Mkataba wa Samatta na TP Mazembe unamalizika Aprili 2016 lakini ikifika mwezi Oktoba mwaka huu, na hapo atakuwa huru kufanya mazungumzo binafsi na klabu yoyote ambayo itaonesha nia ya kuhitaji huduma yake.
Samatta alipata fursa ya kwenda kufanya majaribio kwenye klabu ya CSKA Moscow ya Urusi lakini alipata majeraha wakati akiendelea na majaribio hivyo kushindwa kumaliza muda wa majaribio uliokuwa umepangwa.
0 comments:
Post a Comment