https://play.google.com/store/apps/details?id=com.blog.ya.watanzania


.

.

.
  • Latest News

    .

    TUPIGE KURA, TUPOKEE MATOKEO KWA AMANI NA UTULIVU, KUNA MAISHA BAADA YA UCHAGUZI

    Bendera na ramani ya Tanzania
    JUMAPILI ya Oktoba 25, 2015, Tanzania inafanya Uchaguzi Mkuu wa madiwani, wabunge pamoja na kumpata Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Uchaguzi ni nini? Zipo tafsiri mbalimbali lakini mojawapo na iliyo wazi ni kwamba, hii ni njia ya kidemokrasia inayotumiwa na watu katika kuchagua viongozi wa kuwaongoza kwa kipindi fulani kwa mujibu wa Katiba au utaratibu waliojiwekea wenyewe. Huu ni Uchaguzi Mkuu wa Tano kufanyika tangu mfumo wa vyama vingi ulipoanza tena mwaka 1992, lakini ni wa 11 tangu Tanganyika na Zanzibar zilipoungana mwaka 1964. Uchaguzi wa mwaka huu una umuhimu wa kipekee kwa sababu kadha wa kadha, mojawapo ikiwa umri wa miaka 23 tangu mfumo wa vyama vingi ulipoanza. Huu ni umri mkubwa, na kwa hakika vijana wengi waliojitokeza kujiandikisha safari hii ni wenye umri wa kati ya miaka 18-35, ikimaanisha kwamba wengi wao walizaliwa kuanzia mwaka 1992. Hawa wanatengeneza asilimia 57 ya wapigakura wote. Umuhimu mwingine ni kwamba, kulinganisha na uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, safari hii demokrasia imekua na kupanuka kiasi cha kushuhudia wapigakura 22.75 milioni, idadi ambayo ni kubwa zaidi kuwahi kutokea nchini tangu tupate Uhuru. Kwa upande mwingine, hamasa imeongezeka, upinzani umeimarika zaidi na uhuru wa habari umepanuka ukiwamo ukuaji wa sekta ya habari na mawasiliano, hususan mitandao ya kijamii. Haya yote yanatokea kutokana na kuwapo kwa amani na utulivu, sifa ambazo zimeendelea kuitambulisha vyema Tanzania hata katika jumuiya za kimataifa. Uchaguzi Mkuu ni gharama kubwa kifedha, rasilimali watu na muda, na kama mambo yatakwenda mrama maana yake nchi itakuwa imeingia hasara kwa kupoteza fedha, lakini pia itaingia kwenye machafuko ambayo yatatowesha amani iliyodumu kwa miaka mingi. Madhara ya machafuko au vita – kama tulivyoshuhudia kwa majirani zetu Rwanda na Kenya ni vifo, ulemavu wa kudumu, kutengana na familia, ukimbizi na kuvurugika kwa uchumi, jamii na siasa kwa ujumla. Kwa miaka yote tangu Uhuru, licha ya uchanga na umaskini kama taifa, Watanzania hatujazoea maisha ya vurugu na machafuko na ndiyo maana tuna wajibu wa kuhakikisha uchaguzi huu unapita salama. Wajibu wa kulinda amani ya nchi yetu ni wa kila Mtanzania bila kujali rangi, dini, kabila ama nafasi yake katika jamii. Tunaposema hivyo tunamaanisha kwamba, vyombo vya dola vinapaswa kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria na kuhakikisha Watanzania wanapiga kura kwa amani kuchagua viongozi wao kwa utaratibu waliojiwekea. Kimsingi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ndio wasimamizi wa chaguzi zote, hivyo wana dhamana kubwa kuhakikisha kila aliyejiandikisha na kujitokeza siku hiyo anatumia haki yake ya kikatiba kupiga kura bila kubughudhiwa. Ili kuondoa utata huo, NEC pia inapaswa kuhakikisha kunakuwa na uwazi kuanzia hatua ya kupiga kura mpaka wakati wa kutangaza matokeo, ambayo pia yanatakiwa kutolewa kwa wakati ili kuondoa mashaka miongoni mwa wagombea na wananchi kwa ujumla. Wanasiasa, hususan wagombea ama wapambe wao, wanapaswa kutoa kauli za kuhamasisha amani na utulivu kwa siku hizi chache zilizosalia kuelekea uchaguzi mkuu, siku ya uchaguzi na baada ya kutangazwa kwa matokeo. Wanasiasa wanaaminika kwa wananchi, kwa hiyo kauli yoyote watakayoitoa ama inaweza kujenga au kubomoa amani iliyopo, hivyo kuondoa utulivu na kuisambaratisha Tanzania ya sasa iliyotukuka ulimwenguni kote kama kisiwa cha amani na utulivu. Vyombo vya habari navyo vina wajibu mkubwa zaidi kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa usalama na amani na hata baada ya matokeo kutangazwa viendelee kudumisha amani hiyo. Hilo litawezekana tu iwapo vyombo vya habari vitaandika au kutangaza habari kwa kufuata sheria za nchi, miiko na maadili ya taaluma na fani ya uandishi wa habari ikiwa ni pamoja na kutoegemea upande wowote, kuepuka lugha za uchochezi na ushabiki wa kisiasa, kabla na wakati wa kutangaza matokeo. Kutokana na umuhimu huo, sisi wamiliki wa mitandao ya kijamii nchini Tanzania (Bloggers) tumejadiliana na kukubaliana kwa pamoja kuhusu hatma na mustakabali wa taifa letu kuhakikisha amani na utulivu vinadumishwa wakati na baada ya uchaguzi huu wa kidemokrasia na kwa kauli moja tumetoa msimamo wetu kuhusu amani ya nchi hii. Kwa ujumla, hakuna anayeweza kujisifu kuwa ana uhalali zaidi wa taifa hili kuliko mwingine, taifa hili ni letu sote, hivyo wajibu wa kulinda na kudumisha amani na usalama wa nchi ni wa kila mmoja. Tunaomba Watanzania wote wenye sifa wajitokeze kupiga kura kwa amani na utulivu, wasubiri matokeo kwa amani na utulivu, wapokee matokeo kwa amani na utulivu, maisha yaendelee kwa amani na utulivu, tusonge mbele kwa amani na utulivu huku tukijua kwamba kuna maisha baada ya uchaguzi, na hilo ndilo muhimu zaidi. MUNGU IBARIKI TANZANIA!
    https://play.google.com/store/apps/details?id=com.blog.ya.watanzania

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Post a Comment

    Item Reviewed: TUPIGE KURA, TUPOKEE MATOKEO KWA AMANI NA UTULIVU, KUNA MAISHA BAADA YA UCHAGUZI Rating: 5 Reviewed By: Unknown
    Scroll to Top