Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa
ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa akizungumza leo na waandishi wa habari
kuhusu mkutano wa siku tano ambao umekutanisha watalaam wa takwimu
kutoka nchi mbalimbali barani Afrika kujadili Mfumo wa Uongozi Bora
katika Ofisi za Takwimu pamoja na Uboreshaji wa Mitaala ya Ufundishaji
wa Masomo ya Takwimu. Mkutano huo unafanyika katika hoteli ya Golden Tulip iliyopo Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa Ofisi
ya Taifa ya Takwimu Afrika Kusini Risenga Maluleke akizungumza leo na
waandishi wa habari kuhusu madhumuni ya mkutano wa watalaam wa takwimu
kutoka nchi mbalimbali barani Afrika ambapo wamekutana kujadili Mfumo wa
Uongozi Bora katika Ofisi za Takwimu pamoja na Uboreshaji wa Mitaala ya
Ufundishaji wa Masomo ya Takwimu. Mkutano huo ni wa siku tano na
unafanyika katika hoteli ya Golden Tulip iliyopo Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu
wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa akizungumza leo Jijini
Dar es Salaam wakati wa mkutano wa watalaam wa takwimu kutoka nchi
mbalimbali barani Afrika ambao wamekutana kujadili Mfumo wa Uongozi Bora
katika Ofisi za Takwimu pamoja na Uboreshaji wa Mitaala ya Ufundishaji
wa Masomo ya Takwimu. Kushoto kwake ni Mtakwimu kutoka Kamisheni ya
Uchumi Afrika Bw. Andry Andriantseheno.
Baadhi ya wakuu wa Ofisi za
Takwimu kutoka barani Afrika wakifuatilia kwa makini majadiliano wakati
wa mkutano wa kujadili Mfumo wa Uongozi Bora katika Ofisi za Takwimu
pamoja na Uboreshaji wa Mitaala ya Ufundishaji wa Masomo ya Takwimu.
Mkutano huo ni wa siku tano na unafanyika katika hoteli ya Golden Tulip
iliyopo Jijini Dar es Salaam. (PICHA ZOTE NA VERONICA KAZIMOTO)
………………………………………………………………………….
Na: Emmanuel Ghula
Dar es Salaam.
VIONGOZI wa Ofisi za Takwimu
barani Afrika leo wamekutana kujadili Mfumo wa Uongozi Bora katika Ofisi
hizo pamoja na Uboreshaji wa Mitaala ya Ufundishaji wa Masomo ya
Takwimu katika nchi za Afrika.
Wakizungumza katika mkutano wa
wataalam wa takwimu ulioanza leo Jijini Dar es Salaam, viongozi hao
wamesema ili takwimu bora zipatikane kwa wakati, ni lazima kuwepo na
mfumo bora wa uongozi pamoja na wataalamu waliobobea katika fani ya
takwimu.
Akizungumza katika mkutano huo,
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dkt. Albina Chuwa amesema
lengo la mkutano huo ni kujadili mfumo wa uongozi bora katika Ofisi za
Takwimu pamoja na namna ya kuboresha mitaala ya ufundishaji wa masomo ya
takwimu barani Afrika.
“Leo tupo hapa wataalamu wa
takwimu kutoka zaidi ya mataifa 25 barani Afrika ili kujadili namna ya
kuboresha mifumo yetu ya uongozi katika Ofisi za Takwimu pamoja na
kujadili mbinu bora za kuimarisha utoaji wa mafunzo kwa watakwimu vijana
hasa kupitia upya mitaala ya ufundishaji,” amesema Dkt. Chuwa.
Dkt. Chuwa amesema kuimarishwa
kwa mfumo wa uongozi pamoja na kuboresha mafunzo kwa wakwimu kutasaidia
katika ukusanyaji wa takwimu bora zitakazotumika katika kupanga mipango
mbalimbali ya maendeleo.Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu
Msaidizi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu wa Afrika ya Kusini, Risega
Maluleke amesema mataifa mengi ya Afrika yanakabiliwa na changamoto
kubwa ya kutokuwa na uwezo wa kujitegemea kifedha kitu ambacho
hukwamisha upatikanaji wa takwimu kwa wakati.
Amesema licha ya changamoto
hiyo, kwa kiasi kikubwa kazi ya ukusanyaji wa takwimu imekuwa ikifanyika
kwa ufanisi mkubwa kutoka kwa watalaam hao wa takwimu na hivyo kupitia
mkutano huu, wataweza kujadili namna ya kuboresha uimarishaji wa Ofisi
za Takwimu.
Maluleke amesema ni vyema
Serikali zikaziwezesha ofisi za ukusanyaji wa takwimu ili ziweze
kujitegemea kibajeti na kuboresha utendaji kazi wake katika kuhakikisha
takwimu bora zinapatikana kwa wakati muafaka.
Mkutano huo wa siku tano
unatarajia kumalizika tarehe 06 Novemba, 2015 ambapo wataalam takribani
30 wamekutana kujadili Mfumo wa Uongozi Bora katika Ofisi hizo pamoja na
Uboreshaji wa Mitaala ya Ufundishaji wa Masomo ya Takwimu katika nchi
za Afrika.
0 comments:
Post a Comment