Watu wawili wamefariki dunia
kutokana na mafuriko ya mvua kubwa iliyonyesha kwa saa kadhaa leo
jijini Mwanza, akiwamo mwanafunzi wa kidato cha nne aliyesombwa na
maji wakati akiwahi kufanya mitihani ya mwisho lakini mwili wake
haujapatikana mpaka sasa.
Mvua hiyo iliyoanza kunyesha saa 12
asubuhi, ilikatika saa 4:30 asubuhi na kusababisha baadhi ya barabara
kuziba kutokana na maji kuporomoka kutoka milimani.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana, Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo, amethibitisha
kutokea kwa vifo hivyo ingawa hadi wakati anatoa taarifa hizo, mwili
mwanafunzi wa kidato cha nne wa shule ya sekondari Nyamanoro, ulikuwa
haujapatikana.
“Mvua kubwa ilinyesha kwa masaa
manne katika maeneo mbalimbali ya jiji iliyosababisha maporomoko
kutoka milimani na kusababisha watu kukosa sehemu ya kupita hasa eneo
la Kirumba ambako mwendesha bodaboda namba MC861 AHK aliyewapakiza
wanafunzi wawili wa kidato cha nne, kusombwa na maji na dereva huyo
kufariki lakini wanafunzi wakiokolewa,” alisema Mkumbo.
Kamanda Mkumbo amemtaja mwanafunzi
wa shule ya sekondari Nyamanoro ambaye mwili wake haujapatikana ni,
Zainabu Shabani (18) aliyekuwa na wenzake wawili waliokuwa wakivuka
daraja llilopo maeneo ya Nyamanoro wilaya ya Ilemela.
“Wenzake walifanikiwa kuvuka
daraja salama, lakini Zainabu hakumaliza safari yake na kusombwa na
maji mpaka na sasa hajulikani kama amekufa ama yupo hai kutokana na
mwili wake kutoonekana,” alisema.
Mkumbo aliwataka wananchi kuacha
tabia ya kuvuka mitaro na maeneo yaliyojaa maji pindi wanapoona mvua
kubwa inanyesha ili kuepuka vifo na mataizo yanayoweza kuepukika.
0 comments:
Post a Comment