Waandishi wetu
Kweli hii ni
kali! Kile kikosi kazi cha Oparesheni Fichua Maovu (OFM) kinachomilikiwa
na Global Publishers, kimenasa tukio la aina yake la kilimo cha mmea
haramu wa bangi kandokando ya kituo cha daladala na kuibua mshtuko
mkubwa.
Bangi hiyo ikiwa imestawi vilivyo.
NI SINZA AFRIKA SANA, DAR
Tukio hilo lililotafsiriwa kuwa ni
kumchokoza Rais John Pombe Magufuli ambaye ametangaza vita dhidi ya
matumizi na biashara ya madawa ya kulevya lilinaswa hivi karibuni katika
eneo la Afrika Sana jijini Dar, mbele ya soko jirani kabisa na Kituo
cha Daladala cha Afrika Sana kwenye Barabara ya Shekilango.
Eneo ilipopandwa bangi hiyo, Afrika Sana jijini Dar.
OFM YATIMIZA MAJUKUMU YAKE
Ikiwa kazini kutimiza majukumu yake
majira ya mchana, OFM iliona kijani kibichi kilichostawi vizuri eneo
hilo lenye mtaro mkubwa wa maji taka ndipo machale yakawacheza makachero
wake na kuamua kuuchunguza mmea huo.
Wakati
wakiangazaangaza, OFM walishuhudia mimea miwili mikubwa ambayo iko
tayari kuvunwa iliyokuwa imestawi vilivyo ikionekana kupata matunzo ya
kutosha ikiwa ni pamoja na kumwagiliwa vizuri.
Katika kuuchunguza mmea huo, ndipo wakatokea vijana ‘wataalam wa mambo hayo’ ambao walithibitisha kuwa mmea huo ni bangi.
Hata hivyo, walipobanwa juu ya mmiliki
wa shamba hilo la bangi wakati ni kinyume na sheria, vijana hao walikana
kumjua mhusika hivyo kutoa nafasi kwa OFM kuripoti tukio hilo katika
Kituo cha Polisi cha Kijitonyama almaarufu Mabatini jijini Dar.
YAVUNWA USIKU
Baada ya kuripoti kituoni, askari aliyekuwa zamu alichukua maelezo na kuahidi kulishughulikia suala hilo mara moja.
“Kwa maeneo hayo mnayoelekeza sisi
tunayajua vizuri sana. Tunalishughulikia mara moja msijali,” alisema
polisi mmoja aliyekuwa zamu.
Katika kufuatilia, siku iliyofuata, OFM
ilifika eneo la tukio na kukuta bangi hiyo hasa ile mimea mikubwa
iliyostawi na kuwa tayari kuvunwa ilikuwa imeng’olewa usiku wake na
kwamba haikujulikana ni nani aliyeiondoa.
SERIKALI YAVAMIA
Pamoja na kuvunwa huko lakini kwa kuwa
shamba hilo lilisheheni mimea hiyo bado mzigo ulikuwa umebaki wa kutosha
hivyo OFM ikafikia hatua ya kwenda kuripoti tukio hilo Ofisi za
Serikali za Mitaa Kata ya Kijitonyama jijini Dar.
Baadhi ya viongozi waliokutwa kwenye
ofisi hizo walitoa ushirikiano wa kutosha ambapo waliambatana na OFM
kisha kwenda kulisafisha eneo hilo kwa kuing’oa mimea hiyo ya bangi na
kuchukua uthibitisho na kwenda nao kwenye ofisi zao huku wakiahidi
kuripoti polisi na kuwakamata wahusika ili sheria ichukue mkondo wake.
Imeandikwa na Chande Abdallah, Issa Mnally na Mayasa Mariwata.
0 comments:
Post a Comment