Ligi Kuu Bara imezidi kuwa nzuri kwa Yanga ambayo imerudi kileleni baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Ndanda FC, Azam FC watazidi kujutia sare yao dhidi ya African Sports
Yanga imerejea kileleni mwa msimamo wa Ligi ya Vodacom kwa mara ya kwanza tangu kuanza mwaka 2016,baada ya leo kuifunga Ndanda Fc ya Mtwara bao 1-0, katika pambano lililopigwa uwanja wa taifa Dar es salaam.
Penalti iliyopigwa dakika ya 60 na nahodha Kelvin Yondani ilitosha kumaliza presha ya mashabiki wa Yanga kuiona timu yao ikirejea kileleni kwa kufikisha pointi 36 sawa na Azam lakini yenyewe ikiwa na idadi kubwa ya mabao ya kufunga.
Kocha Hans van der Pluij aliwaanisha kwa mara ya kwanza kwenye kikosi cha kwanza wachezaji Oscar Joshua na Salum Telela ambao walijitahidi kushirikiana vyema na wenzao.
Yanga pamoja na ushindi huo haikuwafuraisha mashabiki wake kutokana na kiwango kibovu iligochokionyesha leo huku tatizo la kukosa penati likiendelea kuiandama timu hiyo.
Ndanda pamona na kutopewa nafasi ya kushinda mchezo huo walionyesha kuwabana Yanga kipindi cha kwanza kiasi cha kuzua hofu kwa mashabiki wa timu hiyo ambao walikuwa wakisubiri bao kwa hamu.
Hadi mapumziko timu hizo zilikuwa sare licha ya yanga kutengeneza nafasi tano za mabao lakini washambuliaji wake walishindwa kuzitumia ipasavyo kama ilivyokuwa kwa wenzao wa Ndanda.
Kipindi cha pili yanga waliuanza mchezo kwa kasi kwa kumtumia winga wake Simon Msuva ambaye dakika ya 48 aliangusha ndani ha eneo la hatari na beki Salvator Ntebe na Mwamuzi Metheu Akrama kuamuru ipigwe penati lakini Amissi Tambwe alikosa baada ya shuti lake kugonga mwamba wa juu na kurudi uwanjani.
Kukosa penati hiyo hakukuwakatisha Yanga tamaa walizidi kuliandama lango la wapinzani wao Ndanda na kupoteza nafasi kadhaa walizozipata.
Ndanda ambao hawapo ķwenye nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi ya Vodacom walijitahidi kupambana na dakika ya 53 Atupelee Green nusura aifungie timu hiyo bao la kuongoza baada ya shuti alilopiga kupaa juu ya lango.
Mambo yaliendelea kuwa magumu kwa wenyeji Yanga ambao walionekana kukosa mipango ya ushindi baada ya kila shambulizi walilokuwa wakilipanga kuvurugwa na mabeki wa Ndanda.
Mashabiki wa Yanga walilazimika kusubiri hadi dakika ya 60 kushangilia bao hilo pekee lililowarudisha kwenye uongozi wa ligi ya Vodacom likifungwa kwa penati baada ya winga Deusi Kaseke kuangushwa ndani ya eneo la hatari na beki Kassian Penera.
Nahodha Kelvin Yondani ndiye alikwenda kupiga penati hiyo na kufunga bao ambalo liliifanya timu yake kuondoka na pointi zote tatu.
Ndanda Fc baada ya kufungwa bao hilo walizinduka na kulisogelea lango la Yanga lakini walishindwa kusawazisha bao hilo kutokana mipira mingi aliyopiga kuishia mikononi mwa kipa Deogratius Munish.
0 comments:
Post a Comment