Mkuu
wa Wilaya ya Kinondoni Mh. Ally Hapi leo amekutana na kuzungumza na
waandishi wa habari kuhusiana na tatizo la uhujumu wa miundombinu ya
Mwendokasi.
Katika
taarifa yake Mh. Hapi ameeleza kuwa katika kipindi cha siku mbili watu
49 wamekamatwa na polisi wilayani Kinondoni wakiwemo wamiliki wa magari,
bajaji na bodaboda kwa makosa ya kuingilia miundombinu ya Mwendokasi
kinyume cha sheria.
Kati
yao watuhumiwa 43 watapelekwa mahakamani siku ya jumatatu ijayo hali
inaowafanya kuyatumia mapumziko ya Juma wakiwa mahabusu.
Mh. Hapi amewataka wananchi wa Kinondoni na hasa madereva kufuata sheria, vinginevyo watakabiliana na rungu la dola.
Aidha,
Mh. Mkuu wa Wilaya ameagiza Polisi wilayani Kinondoni kuendelea na
zoezi la kuwakamata wale wote wanaogeuza vivuko vya barabara za DART
kuwa sehemu za kulala na kujisaidia.
"Tumewaagiza
Polisi kuwakamata wote wanaolala na kujisaidia kwenye vivuko vya
barabara. Hata wale ambao wamesimama kule juu saa za usiku bila kazi
yoyote wakamatwe na washitakiwe kwa sheria za uzembe na uzururaji.
Wengine hawa ni vibaka na wengine ndio wanaolala na kujisaidia huko
usiku." Alisema Hapi.
Raisi
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Magufuli akizungumza na
wasomi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam alizungumzia juu ya uhujumu wa
miundombinu ya mwendokasi na kuagiza watu hao kushughulikiwa ipasavyo.
Katika
hatua nyingine Mkuu huyo wa wilaya aliutaka uongozi wa DART kuchukua
tahadhari za kiusalama katika vituo vya mabasi ili kuzuia uwezekano wa
kutokea tishio la usalama.
Hapi
aliwataka DART kuweka utaratibu wa kuwakagua abiria kwa mashine za
mikono za ukaguzi ili kuhakikisha usalama wa wananchi wanaopanda mabasi
hayo.



0 comments:
Post a Comment