https://play.google.com/store/apps/details?id=com.blog.ya.watanzania


.

.

.
  • Latest News

    .

    JKT na Jeshi la Magereza Wamkera Rais Magufuli

    RAIS John Magufuli, amelishukia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na la Magereza kwa kutengeneza idadi ndogo ya madawati kutokana na Sh. bilioni nne zilitolewa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Aprili, mwaka huu.

    Akizungumza wakati wa shughuli ya makabidhiano ya madawati hayo kwenye viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam jana, Rais Magufuli alieleza kushangazwa kwake na majeshi hayo kutengeneza madawati 53,450 tu katika kipindi cha miezi mitatu (siku 90) tangu fedha hizo zilipotolewa wakati wana nguvu kazi ya kutosha.

    Hata hivyo, taarifa iliyotolewa jana jioni na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa, ilieleza kuwa, madawati 61,385 ndiyo ambayo yametengenezwa katika awamu ya kwanza kutokana na fedha hizo za Bunge, ikiwa ni idadi tofauti iliyosemwa na Rais mapema kwenye hafla hiyo.

    Taarifa ya Ikulu ilifafanua kuwa, madawati mengine 60,000 yatatengenezwa kwenye awamu ya pili.

    Rais Magufuli aliongeza kuwa, ukigawa idadi ya siku 90 kwa vyombo viwili vya JKT na Magereza, maana yake kila chombo kimetengeneza madawati 30,000.

    Rais Magufuli alisema JKT ina kambi nyingi na kutolea mfano za Oljoro, Makutupora, Mafinga, Mpwapwa, Mlale na kwamba ukigawa kwa idadi ya kambi hizo kwa madawati 30,000 unapata wastani wa madawati 30 kwa siku, ambayo yametengenezwa na kila kambi.

    Kutokana na hali hiyo, amewataka wakuu wa JKT na Magereza kuchukua jukumu hilo la utengenezaji madawati kama vita, kwa kuwatumia wafungwa na nguvu kazi zilizopo katika vikosi kuharakisha utengenezaji wa madawati.

    Katika shughuli hiyo alikabidhi madawati hayo kwa wabunge wa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi, Unguja, Pemba na Tanga.

    Madawati hayo yalitengenezwa kutokana na hundi ya Sh. bilioni nne iliyotolewa na Bunge na kukabidhiwa Rais Magufuli Aprili 11, mwaka huu kama mpango wao wa kubana matumizi.

    “Natoa wito kwa vyombo vya ulinzi, JKT na Magereza japokuwa mmetengeneza madawati lakini mjipange katika hili, haiingii akilini, nimekaa JKT mwaka mzima najua hamuwezi kutengeneza madawati machache hivi,” alisema Magufuli.

    “Niwaombe, chukueni hili kama jukumu la haraka, tunahitaji madawati, ninahitaji madawati leo na Waziri Mwinyi (Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Hussein Mwinyi) yupo hapa na kwa bahati mbaya hajaenda JKT hajui shida tunazozipata kule, labda siku mumpeleke siku akaone, sisi tunafahamu kule ni kazi tu,” alisema Rais Magufuli.

    Alisema JKT na Magereza wana nguvu kazi kubwa wakiwamo wafungwa ambao hawahitaji fedha yoyote kufanya kazi kwani ni wajibu wao, na kwamba kila mkoa kuna magereza hivyo askari waliopo katika magereza hayo wakafanye kazi.
     
    Alisema wafungwa waliofungwa katika magereza wanapewa chakula kutoka katika bajeti kuu, hivyo wanapaswa kufanya kazi.

    Rais Magufuli alisema hata fedha anazotarajia kuzipata kwa ajili ya utengenezaji wa madawati mengine kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na PPF anasita kuvipatia vyombo hivyo vya ulinzi na usalama kwa kuogopa kuchukua muda mrefu.

    “Kama mmeshindwa mniruhusu niwa ‘involve’ wakuu wa mikoa, nina uhakika nikimwambia Makonda akiwahusisha vijana wa vijiweni mwezi mmoja madawati yataisha. Sasa mnisaidie ndugu zangu makamanda mkatengeneze madawati. Nimeona bora niongee hapa ili nisitoke na kiungulia, ila nyie ndiyo mtoke na kiungulia,” alisema Magufuli
     
    Rais Magufuli alisema anahitaji madawati haraka ili kuondoa uhaba unaozikabili shule za sekondari na msingi wa madawati 1,400,000.

    Alisema hadi sasa zaidi ya madawati 1,000,000 sawa na asilimia 88 ya madawati yaliyohitajika kwa shule za msingi na asilimia 95.8 kwa shule za sekondari yamepatikana.

    Rais Magufuli alisema kwa sasa kwa shule za msingi imebaki asilimia 11.2 kumaliza tatizo la madawati, huku kwa shule za sekondari imebaki asilimia 4.2,

    Alisema tangu atoe agizo kwa wakuu wa wilaya na mikoa ya kutengeneza madawati, halmashauri 25 zimefikia malengo kwa upande wa shule za msingi na halmashauri 46 kwa shule za sekondari.

    Katika mgawanyo wa madawati hayo, mkoa wa Dar es Salaam ulipata madawati 5,370, mikoa mingine na idadi yao katika mabano ni Pwani (4,833), Morogoro (5,907), Lindi (4,295), Mtwara (5,370), Ruvuma (4,833), Iringa (3,757), Njombe (3,222), Mbeya (3,759), Songwe (3,222), Rukwa (2,285), Katavi (2,683) Unguja (3,200), Pemba (1,800) na Tanga (6,444).

    Kadhalika, Rais Magufuli alisema baada ya kuanza kutekeleza ahadi ya kuondoa ada kwa shule za msingi na sekondari, idadi ya wanafunzi waliojiandikisha kuanza darasa la kwanza imeongezeka kutoka wanafunzi 1,282,100 hadi kufikia wanafunzi 1,896,584 sawa na ongezeko la asilimia 84.5 hali iliyosababisha upungufu wa madawati 1,400,000
    https://play.google.com/store/apps/details?id=com.blog.ya.watanzania

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Post a Comment

    Item Reviewed: JKT na Jeshi la Magereza Wamkera Rais Magufuli Rating: 5 Reviewed By: news
    Scroll to Top