RAIS
John Magufuli amemwahidi kwa utani kumpatia kazi Meya wa Jiji la Dar es
Salaam, Isaya Mwita, endapo atafukuzwa na Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) kutokana na kusifia kazi inayofanywa na Serikali ya
Chama Cha Mapinduzi.
Akizungumza
na wageni waalikwa waliofika katika viwanja vya Karimjee, jijini Dar es
Salaam jana, kushuhudia shughuli ya makadhibiano ya madawati ambayo
yalitokana na Sh. bilioni nne ambazo zilitolewa na Bunge la Jamhuri ya
Muungano ikiwa ni mpango wake wa kubana matumizi, Rais Magufuli alisema
amekuwa akivutiwa na ‘statement’ (kauli) ambazo zimekuwa zikitolewa na
meya huyo.
Alisema
hata alipompatia nafasi ya kuwasalimia wananchi waliofika kwenye hafla
hiyo, meya huyo aliongelea masuala muhimu yenye kuleta maendeleo kwa
taifa.
Rais Magufuli alisema amekuwa akifuatilia kauli za Meya Mwita na kueleza hotuba zake zimekuwa zenye dhamira ya kuleta maendeleo.
Alisema
kwa mzaha, ikiwa meya huyo atafukuzwa katika chama chake yeye
atamkumbuka kwa sababu bado amebakiwa na nafasi nyingi za uteuzi.
“Ninafurahi
Meya Mwita, ninakupongeza sana kwa sababu nimekuwa nikisikiliza sana
`statement’ zako za maendeleo, sasa sijui nikisema hivi watakubakiza au
watakufukuza, ila wakikufukuza mimi nitakukumbuka kwa sababu nina nafasi
nyingi bado za uteuzi,” alisema Rais Magufuli kwa utani na kusababisha watu kucheka.
Alisema viongozi wanapaswa kulenga kutatua matatizo ya wananchi na siyo kuingiza masuala ya itikadi za vyama katika kila jambo.
Awasifu Dr Tulia na Mchungaji Msigwa
Katika
hatua nyingine, Rais Magufuli aliwapongeza Mbunge wa Iringa (Chadema),
Peter Msigwa na Naibu Spika wa Bunge, Dk. Ackson Tulia, kwa kukaa pamoja
katika meza kuu wakati wa hafla hiyo.
Wabunge
kutoka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
walitangaza kususia vikao vya bunge vinavyoongozwa na Dk. Ackson au
shughuli yoyote itakayoongozwa naye kwa madai amekuwa akiendesha vikao
vya bunge kwa upendeleo na kutaka avuliwe wadhifa huo.
Rais Magufuli alisema inapofika masuala ya kuleta maendeleo ya taifa, viongozi wanapaswa kuweka kando masuala ya vyama.
Alisema
hata yeye wakati akipiga kampeni za uchaguzi mkuu mwaka jana,
aliwaahidi Watanzania kuwa atawatumikia wote bila ya kuangalia vyama,
kabila, dini wala rangi.
“Mmeacha
vyama vyenu pembeni, mnaunga mkono maendeleo, leo unapomwona Msigwa na
Tulia wapo jirani inatia moyo, ndicho tunachokitaka, nchi hii ni yetu
sote, tukifanya hivyo nchi yetu itakuwa ya mfano,” alisema Rais Magufuli.
Alipoulizwa
kwa kitendo chake cha kuhudhuria shughuli hiyo na kukaa meza moja na
Dk, Ackson, Msigwa alisema wamefika katika hafla kama wajumbe wa Tume ya
Utumishi ya Bunge.
Alisema
pia walihudhuria hafla hiyo kwa sababu ni suala la maendeleo na
walipaswa kushiriki ili kuhakikisha fedha hizo zinatumika kama
zilivyopangwa.
“Hii shughuli haiendeshwi wala kuandaliwa na Tulia, ni shughuli iliyoendeshwa na tume yetu na ndiyo maana tupo hapa,” alisema Msigwa.
Pia
Rais Magufuli alimtaka Mbunge wa Kaliua(CUF), Magdalena Sakaya,
kutoogopa kupeleka maendeleo katika jimbo lake kwa sababu maendeleo
hayana chama
Mbunge huyo alisema hafla hiyo ni ya maendeleo hivyo hawakuwa na sababu ya wao kugomea.
Wabunge
wa Ukawa waliwahi kukaririwa wakilalamikia kitendo cha uongozi wa Bunge
kurejesha Sh. bilioni nne serikalini ili kubana matumizi.
Rais
Magufuli, ambaye alikabidhiwa hundi ya fedha hizo Aprili 11, mwaka huu,
alielekeza zitumike kutengeneza madawati, huku akizitaka ofisi na
taasisi zingine za serikali kuiga mfano huo.
0 comments:
Post a Comment