Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF)
Maalim Seif Sharif Hamad amesema Jeshi la Polisi kama lina nia ya
kumkamata na kumweka ndani lifanye hivyo kwa kuwa yeye yupo nchini.
Akizungumza katika Baraza la Eid el Fitri lililofanyika katika ukumbi wa
Wakfii wa Ngazija mjini Zanzibar, tofauti na jingine lililofanyika ukumbi
wa Baraza la Wawakilishi la zamani na kuhutubiwa na Rais wa Zanzibar, Dk
Ali Mohamed Shein, Maalim Seif alisema nchi inapita katika kipindi
kigumu kutokana na dhuluma inayotendwa na watawala dhidi ya raia
wasiokuwa na hatia.
“Huwezi kuamini kuwa dhuluma hii inatendwa na
watawala Waislamu. Hali ni mbaya, wananchi wanapata hilaki kubwa baada
ya hao wanaojiita Serikali kubaini kuwa hawakubaliki.
"Mambo hayo
yanafanywa kutokana na kushindwa kuzigeuza nyoyo za wananchi ndiyo maana
wanafanya hujuma, vitendo vya kikatili na kuwatisha wananchi,” alisema
Maalim Seif.
Maalim Seif alieleza kusikitishwa na hali ya kamatakamata
dhidi ya viongozi mbalimbali wa CUF katika ngazi za wilaya na majimbo
na kuwekwa ndani huku wakiteswa, kuadhibiwa na kulazimishwa kukubali
kushiriki katika vitendo vya uhalifu ambavyo hawakuvitenda.
Alibainisha
kuwepo mwendelezo wa kauli zinazoashiria azma ya kutaka kumkamata
yeye, zinazotolewa na baadhi ya wakuu wa vyombo vya dola.
“Hakuna haja
ya kuwatesa watu, iwapo wanayo azma ya kunikamata, mimi nipo waje tu
wanikamate,” alisema Maalim Seif.
Maalim Seif alisema vitendo vyote
hivyo ni mwendelezo wa dhuluma aliyoitenda Mwenyekiti wa Tume ya
Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Jecha Salim Jecha, tarehe 28 Oktoba 2015
wakati akifuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu kabla ya kuitisha ule wa marudio
wa Machi 20.
Hii ni mara ya kwanza mpasuko wa kisiasa unawaathiri
Wazanzibari hata wakati wa Sikukuu ya Eid -El Fitr inayoadhimishwa baada
ya kumalizika mfungo ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Akihutumia Baraza
lililofanyika katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani, Dk
Shein aliendelea kukazia kuwa Zanzibar haitakuwa na uchaguzi mwingine
mpaka mwaka 2020 kwa kuwa Serikali iliyochaguliwa na wananchi
imeshaundwa.
Katika hotuba hiyo ya takriban dakika 35, alisema
hakutakuwa na Serikali ya mpito na kueleza kuwa hayo “yanayosemwa
mitaani ni maneno ya wababaishaji.”
0 comments:
Post a Comment