RAIS
wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesema uchaguzi mkuu visiwani humo
ulishamalizika na hakuna mpango wa kuwepo kwa serikali ya mpito.
Amesema
uchaguzi umekwisha kabla ya mwingine utakaofanyika mwaka 2020; hivyo
kazi kubwa inayofanywa sasa ni kusimamia na kutekeleza Ilani ya Chama
Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015-2020 kwa ajili ya kuwaletea wananchi
maendeleo.
Alisema
hayo jana wakati akihutubia Baraza la Iddi na kusisitiza kuwa
atapambana na watu ambao wamekuwa wakifanya mbinu serikali ishindwe
kutekeleza mipango yake.
Alisema
wapo watu wamekuwa wakijaribu kufanya mbinu na vituko serikali ishindwe
kutekeleza mipango yake, ikiwemo kusimamia ilani ya chama na bajeti ya
serikali kwa mwaka 2016/2017.
Dk
Shein aliwapongeza wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa kupitisha
bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2016/2017, ambayo kazi kubwa
itakayofanywa ni kusimamia mapato na kupata fedha za kutekeleza mipango
hiyo.
“Wananchi
napenda kusema tena kwamba uchaguzi umekwisha na utafanyika mwingine
ifikapo mwaka 2020...wanaotaka kuwepo kwa serikali ya mpito wasahau,” alisema.
Alisema
hakuna sababu ya kuwepo kwa serikali ya mpito kwa sababu CCM ilishiriki
katika uchaguzi wa marudio na kushinda kwa kishindo.
Aliwataka
wananchi kupuuza propaganda zinazotolewa na wapinzani kwa ajili ya kile
alichosema ni kuwazubaisha wananchi washindwe kufanya kazi zao vizuri.
Alikemea matukio yanayojitokeza zaidi katika kisiwa cha Pemba, yakiashiria uvunjifu wa amani na utulivu.
Alivitaka
vyama vya siasa kufanya kazi zao bila ya kukiuka sheria zilizopo.
Alisema vitendo vya chuki na ufisadi ni kinyume na maagizo ya Mungu.
“Nimesikitishwa
sana na matukio yote ambayo yamelitia aibu kubwa taifa letu kwani
hayaendani na mafunzo tuliyoyapata katika kipindi cha
swaumu...tunatakiwa kuacha kujenga kiburi na ufisadi,” alisema.
Wakati
huo huo, alikemea matukio ya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia
ikiwemo vya kuwadhuru watoto, ikiwemo baadhi vilivyofanyika katika
kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Alisema
serikali imejizatiti kupambana na matukio hayo, ikiwemo kuanzishwa kwa
mahakama ya watoto, itakayosikiliza kwa haraka kesi zinazohusu kundi
hilo.
Alitaka jamii kuwa tayari kutoa ushahidi mbali ya vyombo vya sheria ikiwa ndiyo njia muafaka ya kukomesha matukio hayo.
“Serikali
tumejipanga kupambana na matukio ya vitendo vya udhalilishaji wa
kijinsia lakini jamii nayo iwe tayari kutoa ushahidi mbele ya vyombo vya
sheria,” alisema.
Kwa
upande wake, Mufti wa Zanzibar, Shehe Mkuu Saleh Kabi alimpongeza rais
kwa ustahimilivu katika kuongoza visiwa vya Unguja na Pemba kwa utulivu
mkubwa na hekima.
“Huo ndiyo uongozi bora uliotukuka wa kuongoza nchi kwa kutumia busara na hekima japo unajua wapo watu wanaofanya vitimbi,” alisema.
Sherehe
za baraza la Iddi zilihudhuriwa na viongozi mbali mbali, akiwemo Makamu
wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Makamu wa Rais mstaafu, Dk Mohamed
Gharib Bilal.
0 comments:
Post a Comment