Mzazi
aliyejifungua watoto watatu kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH),
lakini akazuiwa wodini kutokana na kudaiwa gharama za matibabu, jana
aliruhusiwa kuondoka baada ya Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kuingilia
kati suala hilo.
Mzazi huyo, Stella Nnko (38) aliyefikishwa Muhimbili kwa rufaa akitokea Hospitali ya Mnazi Mmoja, alikuwa akidaiwa Sh540,595.
Waziri
wa Afya, Ummy Mwalimu ndiye aliyeingilia kati suala hilo na kuagiza
mama huyo apewe watoto wake na kuruhusiwa ambapo jana asubuhi katibu
mkuu wa wizara, Dk Mpoki Ulisubisya alimtembelea mzazi huyo kabla ya
kuondoka hospitalini hapo.
Akizungumzia
tukio hilo, Stella alimshukuru Waziri kwa kuingilia kati suala hilo na
kuwaomba wasamaria wema kumsaidia katika matunzo ya watoto hao kwa kuwa
uwezo wake kiuchumi si mzuri.
Alisema hajawahi kuonana na baba wa watoto hao tangu alipompa ujauzito, na yeye hana uwezo wa kuwatunza.
“Ninayaendesha
maisha yangu kwa kukaanga mihogo, shughuli ambayo kwa sasa nitashindwa
kuendelea kuifanya kwa sababu ya kuwahudumia hawa watoto,” alisema Nnko.
“Nyumbani nimemwacha mwanangu wa miaka miwili na nusu na sina msaidizi wala ndugu.”
Stella
anaishi Kivule, Ilala jijini Dar es Salaam. Kabla ya kuondoka
Muhimbili, watoto hao watatu walipewa chanjo ya kupooza, BCG ya kifua
kikuu na matone ya vitamin A.
Mtoto
mmoja kati yao ni wa kiume na alizaliwa akiwa na uzito wa kilogramu 2.8
wakati wa kike wawili walikuwa na uzito wa kilo 2.5 na 2.1.
Akizungumzia
sakata hilo, mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma cha MNH, Aminiel
Aligaesha alisema Stella alifikishwa hospitalini hapo Juni 29 mwaka huu
kwa dharura akitokea Mnazi Mmoja na kufanyiwa upasuaji Juni 30.
Lakini
alikanusha taarifa kwamba MNH ilimzuia kutoka, bali alipewa hati ya
malipo ili ajiandae kulipa, kinyume na kauli ya Stella kwamba
aliruhusiwa kuondoka na kupewa hati ya malipo na alipoeleza kuwa hana
uwezo, alizuiwa mpaka atakapochangia huduma.
“Wakati
Stella akipewa huduma na kusubiri kuruhusiwa, alipelekewa gharama ya
jumla ya Sh477,131 ikiwa ni gharama ya kujifungua kwa upasuaji na huduma
zote alizozipata tangu alipopokelewa, zikiwemo dawa na vitendanishi.
Hakuzuiwa, ila alipewa hati ya malipo ili ajiandae kulipa,” alisema Aligaesha.
Alisema pamoja na hayo, Nnko amesamahewa kulipa gharama zote za matibabu na tayari amesharuhusiwa kwenda nyumbani.
Kuhusu
suala la tozo kwa mama wajawazito, Aligaesha alisema ni utaratibu ambao
uliwekwa na hospitali wa kuchangia huduma kwa kuwa tangu wameanza mfumo
huo dawa na vitendanishi vimekuwa haviadimiki ikilinganishwa na hapo
awali.
“Dhamira
yetu ni kuhakikisha kila mgonjwa anayekuja kutibiwa MNH anapata dawa na
huduma zote kwa gharama nafuu. Tunawaomba wananchi kuchangia huduma
zote za afya ili tuweze kupata fedha na kutoa huduma kwa mfumo
endelevu.Ndiyo maana ndani kuna duka la MSD,” alisema
Alisema
iwapo akitokea mgonjwa hana uwezo wa kuchangia huduma, utaratibu wa
kumuombea msamaha unatumika na atapata huduma bila malipo.
Maiti iliyozuiliwa
MNH
pia ilidaiwa kuzuia mwili wa marehemu Hilda Mbawala aliyefariki Juni 26
kutokana na ndugu zake kushindwa kulipia gharama za Sh1.4 milioni,
lakini Aligaesha alikanusha madai hayo.
“Wakati
marehemu akitibiwa, ndugu walikuwa wanapewa taarifa na mwenendo wa
matibabu ya ndugu yao, ikiwamo kuhimizwa kuchangia huduma,” alisema Aligaesha.
“Baada ya kifo hicho, ndugu wa marehemu walipewa hati ya gharama ya matibabu ya Sh1.4 milioni ili wakajipange jinsi ya kulipa.”
Alisema
ndugu hao walisema hawana uwezo wa kulipia kiasi hicho cha fedha na
Juni 30 waliwasiliana na Ofisi ya Ustawi wa Jamii ili wasaidiwe na baada
ya majadiliano pande zote mbili zilikubaliana kuwa walipe Sh800,000.
“Wakati
makubaliano hayo yakiwa kwenye hatua za kuidhinishwa na mamlaka husika,
ndipo ndugu walipokimbilia kwenye vyombo vya habari na kulalamika kuwa
hospitali imezuia mwili.
"Ukweli ni kwamba wamelipa kiasi hicho cha Sh800,000 na wamesamehewa deni la Sh 623,747.64 na mwili waliuchukua Julai 5,” alisema.
0 comments:
Post a Comment