Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
kuendeleza eneo la viwanda vya usindikaji mazao la Mkulazi Morogoro ili
liwe kielelezo kikuu cha ukanda maalum wa kiuchumi (SEZ) unaoambaa
sambamba na reli ya TAZARA.
Amesema
wizara hiyo inapaswa ishirikiane kwa karibu na Mamlaka ya Uendelezaji
Kanda Maalum za Kiuchumi (EPZA) pamoja na Kituo cha Uwekezaji Tanzania
(TIC).
Ametoa
agizo hilo leo (Jumatano, Agosti 10, 2016) wakati akizungumza na
watendaji wa EPZA na wafanyakazi wa kiwanda cha kushona nguo cha Tooku
kilichopo eneo la Benjamin William Mkapa, Mabibo External jijini Dar es
Salaam.
Pia
amewataka wakuu wa mikoa sita ya Pwani, Morogoro, Iringa, Njombe, Mbeya
na Songwe kufanya kazi kwa karibu na EPZA kwa kuainisha maeneo
yanayohitaji kuendelezwa kiuchumi ambayo yanafikika kwa urahisi kwa reli
ya TAZARA.
“Wekeni
mipango yenu kwa umakini ya kuanzishwa kwa kanda maalum za kiuchumi
katika maeneo yenu ya kiutawala na mipango hii ijitokeze kwenye mipango
ya maendeleo ya mikoa yenu, onesheni mikakati ya uendelezaji viwanda
inayoendana na Mpango wa Pili wa Miaka Mitano wa Maendeleo wa Taifa,”
amesema.
Amewataka
wakuu hao wa mikoa kuhakikisha wanaweka mfumo utakaoimarisha ulinzi wa
miundombinu ya reli hiyo ili isiharibiwe na watu wenye nia mbaya.


0 comments:
Post a Comment